
Dar es Salaam. Dhana ya “fursa sawa kwa wote,” iliyowekwa katika misingi ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sasa inakabiliwa na mmomonyoko wa taratibu lakini wenye mizizi ya kimfumo.
Unapotembea katika maeneo mbalimbali ya nchi, kuanzia kata zenye pilikapilika za Kinondoni, Dar es Salaam hadi tambarare za ukame za Bahi, Dodoma utaona ukuta wa wazi na usioonekana ukijengwa ndani ya shule za msingi za umma.
Upande mmoja wa ukuta huo kuna mkondo wa shule ulioboreshwa wa masomo kwa lugha ya Kiingereza (English Medium).
Upande wa pili, kuna mkondo wa kawaida wa Kiswahili ambao unaendelea kuelemewa na hali inayotia huzuni ya elimu ya umma; hali inayodhihirishwa na majengo chakavu, uhaba wa madarasa na msongamano mkubwa wa wanafunzi.
Uchunguzi huu unaonyesha kuwa kasi ya Serikali katika kupanua shule za umma zinazotumia Kiingereza kama lugha ya kufundishia, si tu mabadiliko ya kimfumo ya ufundishaji yanayowasilishwa kama hatua ya maendeleo, kama mamlaka zinavyodai.
Badala yake, hali hii inaashiria mgogoro mkubwa wa kiutawala na kifedha uliozalisha mfumo wa elimu wa ngazi mbili, ambao kivitendo umehalalisha mgawanyiko wa kitabaka ndani ya sekta ya umma, jambo linalokwenda kinyume na matakwa ya Ibara ya 11 ya Katiba.
Mtego wa “Mipango Maalumu”
Msingi wa kisheria wa sekta ya elimu nchini Tanzania ni Ibara ya 11 (2) na (3) ya Katiba ya mwaka 1977, inayotamka kwamba kila mwananchi ana haki ya kupata elimu, huku dola ikiwa na wajibu wa kuhakikisha kila mtu anapata fursa sawa ya kufikia uwezo wake.
Aidha, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliweka bayana kuwa Kiswahili ndicho kiwe lugha kuu ya kufundishia katika elimu msingi.
Hata hivyo, katika miaka ya karibuni kumekuwa na wimbi la kile kinachoitwa “utaratibu maalumu,” unaoruhusu halmashauri za manispaa kukwepa misingi hiyo ili kukidhi matakwa ya tabaka la kati la mijini, linalotamani elimu kwa lugha ya Kiingereza.
Utekelezaji wa sera ya elimu bila ada ya mwaka 2016 ulikuwa na dhamira ya kupunguza pengo la fursa katika elimu. Lakini hali halisi inaonyesha kuwa Serikali imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya upangaji hafifu wa bajeti na ucheleweshaji wa utoaji wa fedha.
Ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha, katika eneo la miundombinu ya shule za msingi, Serikali mara nyingi hushindwa kutoa fedha zote zilizotengwa kwenye bajeti, hali inayosababisha utegemezi mkubwa kwa miradi ya wafadhili ambayo nayo huchelewa kutekelezwa.
Ndani ya ombwe hilo la kifedha, shule za umma za Kiingereza zimeibuka kama vyanzo vya mapato vinavyofanana na shule binafsi nusu rasmi.
Katika Shule ya Msingi ya Serikali ya Bahi English Medium iliyopo Dodoma, wazazi wanatakiwa kulipa Sh250, 000 kama mchango wa chakula na Sh250,000 nyingine kama ada ya kujiunga.
Kwa ujumla nchini, michango hiyo maalumu huanzia Sh300,000 hadi Sh600,000.
Kwa wazazi kama Sophia Amoni wa Sinza, gharama hizi zinaonekana kuwa nafuu ukilinganisha na shule binafsi za gharama kubwa. Lakini kwa jirani yake Juma, mfanyabiashara mdogo wa mtaani, hiyo ni ngazi isiyopandikika.
Kikwazo hicho cha kifedha kinazifanya familia za kipato cha chini kushindwa kufikia ubora wa elimu ambao sekta ya umma ilipaswa kuwapatia, hivyo watoto wao kulazimika kubaki katika shule za Kiswahili zenye uhaba mkubwa wa rasilimali.
Kwa kuruhusu utozwaji wa michango hiyo, mamlaka zimeonekana kuhamishia mzigo wa utoaji wa elimu bora kwa mzazi mmoja mmoja, huku zikijiondoa katika wajibu wake wa kikatiba.
Simulizi ya viwango viwili
Pengo la uwajibikaji si suala la mjadala wa kisera pekee; linaonekana wazi katika tofauti kubwa zilizobainishwa na ripoti za Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT).
Kwa mujibu wa Ukaguzi wa Kiutendaji wa mwaka 2021 uliofanywa na CAG, wastani wa kitaifa wa uwiano wa darasa moja kwa wanafunzi ulikuwa 1:76, karibu mara mbili ya kiwango kinachotakiwa cha 1:40.
Takribani wanafunzi milioni 5.38 nchini walilazimika kukaa nje ya madarasa kutokana na uhaba wa nafasi.
Hali hiyo inapolinganishwa na shule mpya za umma za Kiingereza, tofauti inaonekana wazi. Katika maeneo ya Kinondoni na Ubungo, mikondo iliyoboreshwa ya Kiingereza ina wastani wa wanafunzi 47 kwa darasa, huku mikondo ya Kiswahili ndani ya shule hizo hizo ikiwa na uwiano unaofikia wanafunzi 72 kwa darasa.
Kadhalika, uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi katika mikondo ya Kiingereza ni 1:55, wakati mikondo ya Kiswahili ikiwa na uwiano wa 1:63.
Upendeleo huo unaonyesha kuwa Serikali yenyewe inatoa mazingira bora zaidi ya kujifunzia kwa kundi maalumu la wanafunzi, huku idadi kubwa ya watoto wa Kitanzania – milioni 6.31 kati yao wakiwa hawana hata vyoo vya msingi – wakibaki katika mazingira duni ya kujifunzia.
Katika Manispaa ya Songea, Shule ya Msingi ya Chief Zulu English Medium ilizinduliwa hivi karibuni baada ya kujengwa kwa gharama ya Sh626.4 milioni kutokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Ingawa shule hiyo ina vyumba vya Tehama na hata masomo ya Kifaransa kwa wanafunzi 491, wakosoaji wanaiona kama mfano wa maendeleo yanayotekelezwa kwa mtazamo wa “kisiwa ndani ya bahari ya matatizo.”
Wanahoji: Kwa nini karibu shilingi bilioni moja za kodi za wananchi zielekezwe kwa wanafunzi 500 pekee wakati wilaya nzima inakabiliwa na upungufu mkubwa wa miundombinu ya elimu?
Mtafiti mkongwe wa elimu na mmoja wa waanzilishi wa taasisi ya HakiElimu, Japhet Makongo, anaona “utaratibu maalumu” huo kuwa ni kupotoka kwa hatari kutoka katika wajibu wa kikatiba.
“Tunapaswa kufanya maamuzi kwa kuzingatia masilahi ya wengi,” anasema Makongo. “Kama tunaamini Kiingereza kitamsaidia mtoto wa Kitanzania, basi kifanywe kuwa lugha ya kufundishia katika shule zote za umma, si kwa kundi dogo tu.”
Anasema kwa kuruhusu maboresho ya kuchagua baadhi ya shule, Serikali imeigeuza haki ya umma kuwa bidhaa inayoweza kuuzwa, na hivyo kuunda mfumo ambao “ubora” wake unapatikana kwa wale wenye uwezo wa kulipa.
Wakati Serikali ikiwasilisha hali hiyo kama kutoa “machaguo,” wadau wa elimu wanaona kuwa ni ugawaji wa kibaguzi wa rasilimali za dola.
“Sasa shule za Serikali zinaanza kuwa za kitabaka,” anasema mchambuzi wa elimu, Ben Barka. “Ngazi ya juu ya Kiingereza kwa matajiri, na ngazi ya chini ya Kiswahili kwa maskini.”
Jinamizi la ufundishaji
Wataalamu wanasema chanzo kikuu cha mgogoro huu ni ukosefu mkubwa wa uratibu kati ya Wizara ya Elimu na Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Wakati Wizara ya Elimu ikiandaa sera, Tamisemi ndiyo inayosimamia miundombinu. Halmashauri mbalimbali kama Bahi na Kinondoni zimekuwa zikifanya maamuzi ya kuboresha shule kuwa za Kiingereza bila kuwepo kwa mpango wa kitaifa unaohakikisha kwamba shule nyingi za Kiswahili haziendelei kusahaulika.
Kutokuwapo kwa mshikamano huo wa kiutawala kumezalisha kile anachokiita mchambuzi maarufu wa elimu, Richard Mabala, kuwa ni “jinamizi la kielimu.”
Anaonya shule za sekondari hivi karibuni zitapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza waliotoka katika mifumo miwili tofauti kabisa ya lugha.
“Mwalimu hawezi kwenda kasi sana kwa sababu atawaacha wanafunzi waliotoka shule za Kiswahili, wala hawezi kwenda polepole sana kwa sababu atawachosha waliotoka za Kiingereza,” anaeleza Mabala. “Katika mazingira kama haya, usawa wa fursa utawezekanaje?”
Wanasaikolojia wa elimu na watafiti wanaeleza kuwa “ubora” unaouzwa katika mikondo hiyo ya Kiingereza mara nyingi ni taswira inayoficha udhaifu wa kimfumo.
Utafiti uliofanywa na Lucy Ringo, mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. John’s, unaonyesha kuwa uwezo wa walimu katika matumizi ya Kiingereza bado ni changamoto kubwa; baadhi yao katika shule za umma wakitamka neno “chalk” kama “chaki” na “sentence” kama “sentensi.”
Katika utafiti wake unaohusu umahiri wa walimu katika ufundishaji wa Kiingereza katika shule za msingi Tanzania, Ringo anabainisha kuwa asilimia 87.5 ya walimu waliohojiwa hawajawahi kushiriki mafunzo ya kazini kwa kipindi cha hivi karibuni, jambo linaloonyesha kuwa msingi wa kitaaluma wa shule hizo bado umekwama.
Mwanasaikolojia mashuhuri wa elimu kutoka University of Dar es Salaam, Richard Shukia, anaeleza kuwa mfumo huu wa “ngazi mbili” unadhoofisha kwa makusudi maendeleo ya stadi muhimu za karne ya 21 kama ushirikiano, uwajibikaji wa kijamii na uwezo wa kutatua changamoto kwa pamoja.
“Ushirikiano unahitaji mazingira ya pamoja ambapo wanafunzi kutoka katika malezi na hali tofauti wanajifunza kushirikiana kutatua matatizo,” anasema Shukia.
Anasema kwamba watoto wanapotenganishwa kwa msingi wa uwezo wa wazazi wao kulipa, “mtaala unaotekelezwa kwa vitendo” huwafundisha kuwa thamani yao inategemea tabaka walilotoka badala ya uwezo wao binafsi.
Uchambuzi wa Shukia ulibaini kuwa ni asilimia 3.1 tu ya shughuli zilizomo katika silabasi ya Darasa la Tatu zilihusiana na kujenga ushirikiano, na upungufu huo unazidi kuwa mkubwa kutokana na mgawanyiko wa kimazingira unaofanyika ndani ya viwanja vya shule.
Mpaka Bunge litakapoiwajibisha Serikali kikamilifu kuhusu utekelezaji wa Ibara ya 11 ya Katiba, ukuta wa Sinza na ada za Bahi vitaendelea kubaki kama alama za mfumo wa elimu ulioamua kuwaacha nyuma watoto wa familia maskini zaidi.
