HRW: Mamluki wa Colombia katika vita vya Sudan wanapewa mafunzo UAEHRW: Mamluki wa Colombia katika vita vya Sudan wanapewa mafunzo UAE

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limeripoti kwamba wapiganaji mamluki kutoka Colombia wanapewa mafunzo katika kambi za kijeshi za Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na kisha wanapelekwa Sudan ili kuwasaidia waasi wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF).

Kwa muujibu wa ripoti ya shirika la habari la IRNA, likinukuu tovuti ya habari ya Human Rights Watch, shirika hilo limewahoji wakandarasi wawili wa kijeshi wa Colombia waliotumwa Sudan, mfanyakazi wa zamani wa Kundi la Huduma za Usalama Duniani lenye makao yake Abu Dhabi, wakazi wa el Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini huko magharibi mwa Sudan, na maafisa wa zamani wa jeshi la Colombia.

Human Rights Watch pia imepitia hati na rekodi za wakandarasi hao na kuthibitisha picha na video zilizochapishwa kuhusu suala hilo.

Video hizo zinaonyesha mamluki wa Kicolombia wakifanya mazoezi katika vituo vya kijeshi vya Umoja wa Falme za Kiarabu na wakipigana bega kwa bega na waasi wa RSF nchini Sudan dhidi ya jeshi la taifa la nchi hiyo. Shirika la haki za binadamu la Human Rights Watch limegundua kuwa wapiganaji hao mamluki walitoka katika kambi ya kijeshi ya Emirati.

Human Rights Watch inawashutumu waasi wa RSF kuwa wamehusika na uhalifu wa kivita kote Sudan tangu mwanzo wa vita, ikiwa ni pamoja na wakati wa uvamizi wa mji wa al Fasher, mauaji kinyume cha sheria, ubakaji, ubakaji wa genge, utumwa wa kingono, uporaji na uharibifu wa miundombinu ya raia. HRW imeongeza kuwa: Msaada wa kijeshi wa Umoja wa Falme za Kiarabu kwa Kikosi cha Msaada wa Haraka unajumuisha kusaidia na kushiriki katika kutenda jinai za kivita na uhalifu dhidi ya binadamu.

Shirika hilo limewataka “washirika wa UAE, wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika” kuwataka viongozi wa Imarati kuacha mara moja kutoa silaha, zana, wapiganaji na aina nyingine za misaada kwa RSF.

Uchunguzi uliofanywa na Shirika la habari la Ufaransa (AFP) mnamo Desemba 2025 pia ulifichua kwamba mamia ya wanajeshi wa zamani wa Colombia wamepelekwa Sudan kwa ahadi ya kupewa mishahara mikubwa ili kushiriki katika vita vya ndani nchini humo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *