
Dar es Salaam. Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) kimesema tuzo za mwajiri bora wa mwaka 2026 zitafanyika kwa mfumo mpya utakaoweka ushindani wa kisekta, kuongeza uwazi wa vigezo na kushirikisha sekta rasmi pamoja na isiyo rasmi.
Mfumo huo mpya unalenga kuongeza uwazi, ushindani wa haki na kuendana na mabadiliko ya dunia ya kazi.
Akizungumza leo Alhamisi, Mei 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran amesema mbali na mafanikio ya kibiashara, tuzo hizo zimekuwa zikitambua waajiri wanaozingatia utawala bora, ujumuishi mahali pa kazi, uwajibikaji pamoja na kufuata sheria na viwango vya kazi vya kitaifa na kimataifa.
Amesema tuzo hizo zimeendelea kuwa jukwaa muhimu kwa zaidi ya miaka 20 kwa kutambua taasisi zinazowekeza katika rasilimali watu na ustawi wa wafanyakazi.
“Mwaka 2025 tulisimamisha kwa muda programu hii muhimu si kwa sababu ilipoteza thamani yake, bali tulitaka kufanya maboresho ya kina ili kuhakikisha inaendelea kuwa bora zaidi,” amesema Suzanne.
Amesema baada ya kufanya tathmini kwa kushirikisha wanachama, wataalamu na wadau mbalimbali, ATE ilibaini kuwa tuzo hizo bado zina umuhimu mkubwa lakini zilihitaji kuboreshwa ili ziwe rahisi kueleweka, wazi zaidi na zenye athari chanya kwa taasisi mwaka mzima.
Kwa mujibu wa Suzanne, baadhi ya mapendekezo yaliyotolewa ni pamoja na kuimarisha uwazi wa vigezo vya ushindani, kuipa tuzo hadhi ya kimataifa, kutumia teknolojia katika mchakato mzima na kuanzisha tuzo za kisekta.
Amesema mfumo mpya wa tathmini umeboreshwa ili kuendana na mazingira ya kisasa ya kazi na kwa mwaka huu kutakuwa na vigezo 11 vya ushindani vitakavyopima ubora wa uongozi, ustawi wa wafanyakazi na uendelevu wa taasisi.
Baadhi ya vigezo hivyo ni pamoja na uongozi na utawala bora, utamaduni wa kazi na uzoefu wa wafanyakazi, ujumuishi na usawa, ubunifu katika rasilimali watu, afya na usalama mahali pa kazi pamoja na ustawi na motisha kwa wafanyakazi.
Katika hatua nyingine, ATE imetangazakwa mara ya kwanza waajiri watashindanishwa kwa kuzingatia sekta zao ili kuongeza ushindani wa haki.
“Awali, kulikuwa na malalamiko kwamba sekta tofauti kabisa zinashindanishwa pamoja. Safari hii kila sekta itashindana kivyake,” amesema.
Chama hicho, kimetangaza makundi maalumu kwa ajili ya biashara ndogo na za kati (SMEs), ikiwamo tuzo ya mwajiri chipukizi na ubunifu bora wa mwajiri SMEs ili kuwapa nafasi wafanyabiashara wadogo kujifunza na kuboresha mifumo yao ya kazi.
Pia, sekta isiyo rasmi imejumuishwa katika mashindano hayo kwa lengo la kuwasaidia wajasiriamali na wafanyabiashara wadogo kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za kazi.
Suzanne amesema ATE inalenga kufanya tuzo hizo kuwa programu endelevu ya kuwasaidia waajiri kuboresha sera na mazingira ya kazi badala ya kuwa tukio la siku moja pekee.
“Tuko tayari kushika mkono sekta rasmi na isiyo rasmi ili kuhakikisha kazi zenye staha zinaimarika na biashara zinaendelea kukua,” amesema.
Kutoka Audit Tax International, Dk Straton Makundi amesema mchakato mzima wa kushiriki na kuchaguliwa kwa tuzo hizo utafanyika kidigitali kupitia mfumo mpya wa tathmini wa kidijitali wa AIR.
Amesema hatua hiyo inalenga kurahisisha ushiriki wa waajiri na kuongeza ufanisi katika tathmini, tofauti na miaka iliyopita ambapo waajiri walikuwa wakijaza dodoso na kuwasilisha maombi kwa njia zisizo za kidigitali, safari hii kila hatua itafanyika kwa kutumia mfumo wa mtandao.
“Mfumo huo utawawezesha waajiri kuomba kushiriki, kujaza taarifa pamoja na kuwasilisha nyaraka zinazohitajika kwa njia ya mtandao,” amesema Dk Makundi.
Amesema pamoja na matumizi ya teknolojia, waandaaji wataendelea kufanya mahojiano kwa baadhi ya washiriki na kutembelea maeneo ya kazi pale itakapohitajika kufanya uhakiki wa taarifa ambazo haziwezi kuonekana mtandaoni.
“Tunaweza kufanya mahojiano na wakati mwingine kutembelea maeneo husika kwa ajili ya kukagua baadhi ya mambo ambayo hayawezi kuonekana kupitia mfumo wa kidigitali,” amesema.
Kwa niaba ya Audit Tax International, Dk Makundi amewasihi waajiri nchini kutumia fursa hiyo kushiriki katika mashindano hayo kwa kuwa mfumo mpya umeboreshwa ili kuongeza uwazi na urahisi wa ushiriki.
Amesema matumizi ya mfumo wa kidigitali ni sehemu ya maboresho makubwa yanayofanywa kuhakikisha tuzo hizo zinaendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya sasa ya dunia ya kazi.
