
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Marekani na Israel, ambazo zimeshindwa katika uvamizi wao wa kijeshi dhidi ya Iran, zinapanga njama ya kupandikiza mzozo na fitina ndani ya Iran.
“Mpango na njama ya adui kipofu – baada ya vita vya kulazimishwa, mashinikizo ya kiuchumi, propaganda na mzingiro – ni kupandikiza mizozo na migawanyiko ya kijamii ili kufidia kushindwa kwake katika uwanja wa kijeshi na kulipiza kisasi kwa taifa,” amesema Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei katika ujumbe wake uliotolewa leo Alhamisi.
Ujumbe huo umetolewa kwa mnasaba wa maadhimisho ya kikao cha kwanza cha Majlisi Ushauri la Kiislamu — bunge la kwanza la Iran baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu— ambacho kilizinduliwa rasmi 28 Mei, 1980.
Ayatullah Khamenei ametoa pongezi za Sikukuu ya Eid al-Adh’ha na maadhimisho ya kuanza Majlisi ya kwanza ya Ushauri la Kiislamu kwa watu wote wa Iran na wabunge, akielezea shukrani zake kwa juhudi za wabunge haswa Spika Mohammad Baqer Qalibaf katika njia ya kuinua nchi.
Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amelitaja Bunge la Iran kuwa ni “kiini cha taifa, dhihirisho la demokrasia ya kidini na nguzo ya utungaji sheria katika Jamhuri ya Kiislamu,” akisema lina jukumu muhimu katika kutekeleza matakwa ya wananchi.
“Kiti cha mwakilishi kinatambuliwa kama safu ya mbele ya mapambano katika njia ya maendeleo ya nchi,” amesema Ayatullah Mojtaba Khamenei, akiwahimiza wabunge kujitolea kikamilifu na kuwa na uratibu kamili na utawala sambamba na kulinda uhuru wa kutunga sheria.
Ameorodhesha vipaumbele vya Bunge akisema kuwa ni pamoja na “kujenga upya nchi, kutatua matatizo ya watu – hasa masuala ya kiuchumi na kimaisha – kuongeza uzalishaji na ajira, kuendeleza sayansi na viwanda, kuinua utamaduni na maadili, kupambana na rushwa, kupunguza mfumuko wa bei na ughali wa maisha na kutokomeza kabisa umaskini.”
Kwingineko, Ayatullah Khamenei ametaja baadhi ya mambo anayopaswa kuwa nayo mbunge, ikiwa ni pamoja na kuzingatia uchamungu, kudumisha “ujasiri na kutangaza misimamo iliyo wazi na thabiti mbele ya sera za kupenda makuu za madola ya kibeberu,” pamoja na kuzingatia kwa makini na kimapinduzi nafasi mpya ya Iran katika eneo la Magharibi mwa Asia na duniani.”
Vilevile ametoa wito kwa kila mtu ambaye moyo wake unapiga kwa ajili ya Uislamu, Mapinduzi ya Kiislamu au kujitawala na hadhi ya Iran kuzidisha juhudi za kulinda umoja wa safu yenye mfungamano na iliyoungana ya taifa, kutogeuza hitilafu za kimizatamo kuwa migogoro na migawanyiko, na kuwa “dhihirisho la mshikamano na mfungamano wa taifa” kwa maneno na vitendo.
