
Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) inatumia Sh1.6 bilioni kila mwaka kununua chanjo za magonjwa mbalimbali, huku ikifanikiwa kufikia asilimia 92 ya utoaji wa huduma hizo kwa walengwa.
Chanjo hizo ni pamoja na saratani ya shingo ya kizazi (HPV), chanjo ya kifaduro na pepopunda (Td), chanjo ya ini, mafua makali na tetenasi (Penta), chanjo ya Bacillus Calmette-Guérin (BCG) na chanjo ya kuhara (Rota).
Hayo yamebainishwa leo Mei 28, 2026 na Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya kutoka Wizara ya Afya, Dk Salim Slim, katika mafunzo kuhusu chanjo ambapo amesema Serikali inaweka nguvu kubwa katika kuimarisha huduma hizo ili kuboresha makuzi ya watoto na kuzuia magonjwa yanayoweza kukingwa.
“Serikali inatoa Sh1.6 bilioni kila mwaka kununua chanjo tu na imefanikiwa kuwafikia asilimia 92 ya walengwa,” amesema Dk Slim bila kutaja idadi kamili ya waliochanjwa.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, chanjo nne kati ya hizo hutolewa kwa jinsia zote, isipokuwa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) ambayo hutolewa kwa wasichana pekee wenye umri wa miaka 9 hadi 14.
Amesema baadhi ya watoto wanatakiwa kupata chanjo zaidi ya mara moja, lakini baadhi ya wazazi wamekuwa wakipuuzia ratiba hiyo, jambo linalohatarisha afya za watoto.
Amesema iwapo watoto wote watapata chanjo kwa wakati, kutakuwa na uwezekano wa kupunguza au kuondoa kabisa wagonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi katika visiwa hivyo.
Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha ndani ya miaka 15 ijayo tatizo la saratani ya shingo ya kizazi linapungua kwa kiasi kikubwa au kutokomea kabisa Zanzibar.
Hata hivyo, amesema bado kuna mitazamo hasi na fikra potofu kuhusu chanjo, lakini jitihada za elimu zinaendelea ili kufikia asilimia 100 ya uchanjaji.
“Waliobaki hawajachanjwa ni kuendelea kuwapa elimu ili wote wachanjwe na kuifanya Zanzibar iwe salama,” amesema.
Amesema pia wamebaini changamoto katika masuala ya uzazi wa mpango, ambapo baadhi ya akina mama wenye watoto wanaofuatana kwa karibu hushindwa kuwahudumia ipasavyo, ikiwemo kuwapeleka kupata chanjo kwa wakati.
Naye, Mratibu wa Magonjwa Yanayokingwa kwa Chanjo katika Mpango wa Taifa wa Chanjo, Ibrahim Juma, amesema watoto wanaopata chanjo wanakingwa na magonjwa kwa zaidi ya asilimia 80.
Amesema kuna haja ya wazazi kutambua umuhimu wa chanjo kwa watoto, kwani ni salama na zinasaidia kulinda afya zao kwa muda mrefu.
