Tanzania kuwasilisha miradi ya uwekezaji ya zaidi ya Sh7 trilioni kuvutia wawekezaji wa kimataifaTanzania kuwasilisha miradi ya uwekezaji ya zaidi ya Sh7 trilioni kuvutia wawekezaji wa kimataifa

Arusha. Serikali imeweka mezani miradi ya maendeleo yenye fursa za uwekezaji yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.85, sawa na zaidi ya Sh7 trilioni, katika mkakati wa kuvutia mitaji ya kimataifa na kuimarisha kasi ya ukuaji wa uchumi wa taifa.

Mkakati huo ni sehemu ya kupunguza utegemezi wa misaada ya fedha za kigeni na kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani katika kugharamia miradi ya miundombinu na mageuzi ya kiuchumi nchini.

Aidha, miradi hiyo itawasilishwa katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji wa Tanzania 2026 utakaofanyika Juni 1 hadi 2 jijini Arusha, ukitarajiwa kuwakutanisha wawekezaji kutoka zaidi ya nchi 30 duniani.

Mkutano huo umeandaliwa na Taasisi ya Utafiti wa Sera na Maendeleo Tanzania (ESRF), kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), pamoja na Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (Zipa).

Jumla ya miradi 60 chini ya mfumo wa kitaifa wa kuwezesha uwekezaji nchini Tanzania (TIGF) itawasilishwa, ikijumuisha sekta mbalimbali zinazolenga kukuza uchumi wa nchi na kuongeza fursa za ajira na maendeleo.

Miongoni mwa sekta zitakazowasilishwa ni miundombinu ya utalii, nishati jadidifu, usafirishaji na usafirishaji wa mizigo, uchumi wa buluu, kilimo na uchakataji wa mazao, miundombinu ya maji pamoja na miradi ya maendeleo ya Serikali za mitaa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 28, 2026 jijini Arusha, Mkurugenzi Mtendaji wa ESRF, Profesa Fortunata Makene amesema Tanzania imejipanga kuhakikisha miradi hiyo inabadilishwa kuwa uwekezaji halisi wenye tija kwa uchumi wa taifa.

Amesema awamu ya kwanza itahusisha miradi 8 hadi 10 ya kipaumbele yenye thamani ya takribani dola milioni 100, ambayo inatarajiwa kuanza kufunguliwa mikataba ya awali ya uwekezaji.

“Tayari tumeandaa miradi iliyofanyiwa uchambuzi wa kina na kuthibitishwa kwa ushirikiano wa Serikali kupitia taasisi zake zinazohusika na uwekezaji pamoja na wadau wa maendeleo. Lengo ni kuhakikisha mchakato wa majadiliano ya uwekezaji unakuwa wa haraka, wazi na wenye ufanisi,” amesema Profesa Makene.

Ameongeza kuwa mkutano huo ni jukwaa muhimu la kuunganisha wawekezaji wa kimataifa na miradi ya sekta ya umma iliyo tayari kwa utekelezaji.

Profesa Makene amesema pia ni sehemu ya juhudi za Tanzania kufikia dira yake ya maendeleo ya 2050 inayolenga kuwa na uchumi wa dola trilioni moja.

Kwa upande wake, Naibu Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania, John Rutere, amesema taasisi hiyo inaunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi imara na unaojitegemea, hasa katika mazingira ya kupungua kwa misaada ya kimataifa ya maendeleo.

Amesema Tanzania, kama zilivyo nchi nyingine za Afrika, inapaswa kuimarisha vyanzo vya ndani vya ufadhili wa maendeleo badala ya kutegemea sana misaada ya nje ambayo sasa haina uhakika wa kudumu.

UNDP imeeleza kuwa itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha uwekezaji unaovutia unawanufaisha wananchi wote, hususan makundi ya kipato cha chini kupitia miradi ya maendeleo jumuishi na yenye matokeo chanya katika ngazi ya jamii.

Aidha, taasisi hiyo imesisitiza kuwa majadiliano endelevu kati ya Serikali na wawekezaji yataongeza kasi ya utekelezaji wa miradi mipya kila mwaka, hatua ambayo itaifanya Tanzania kuwa kitovu muhimu cha uwekezaji barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *