Wananchi Mtwara wamkataa mwekezaji, wahofia kuhatarisha shughuli za uvuviWananchi Mtwara wamkataa mwekezaji, wahofia kuhatarisha shughuli za uvuvi

Mtwara. Hali ya tahadhari, hofu na maswali yasiyo na majibu ndiyo inayotawala katika vijiji vya Mnazi, Milamba na Nalingu vilivyopo Kata ya Nalingu, Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, kufuatia kuibuka kwa mwekezaji wa kigeni mwenye asili ya China anayetarajia kuanzisha shughuli za kilimo cha mwani katika eneo hilo.

Kwa sasa, wananchi wa vijiji hivyo wameungana kupinga uwekezaji huo wakidai hawajapatiwa taarifa rasmi kuhusu shughuli halisi zinazotarajiwa kufanyika, namna zitakavyotekelezwa pamoja na athari zake kwa maisha yao na shughuli za kiuchumi wanazozitegemea, hususan uvuvi.

Sintofahamu hiyo imeibuka baada ya kuonekana kwa mwekezaji huyo, ambaye awali alifahamika kwa shughuli za ununuzi wa malighafi za baharini, akifanya shughuli mbalimbali ambazo wananchi wengi wanadai kushindwa kuzielewa.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wameamua kupaza sauti zao kupitia mkutano maalumu wa kijiji uliowahusisha viongozi wa Serikali, akiwamo Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdallah Mwaipaya, uliofanyika leo Alhamisi Mei 28, 2026.

Abdallah Mwaipaya Mkuu wa wilaya ya Mtwara (wa kwanza kushoto) akiwa anasikiliza na kuandika hoja za wananchi  waliojitokeza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Nalingu, wilayani humo.

Kwa pamoja, wananchi hao wanamtaka mwekezaji huyo kusitisha mipango yake hadi watakapopewa maelezo ya kina na kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa uwekezaji huo.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Shaibu Siye, mkazi wa Nalingu, amesema mwanzoni waliamini mwekezaji huyo ni mfanyabiashara wa kawaida baada ya kununua eneo dogo kwa ajili ya makazi na kuanza kujihusisha na biashara ya baadhi ya malighafi za baharini.

“Alianza kununua maganda ya kumbwa na vitu vingine vya baharini. Wakati mwingine alikuwa ananunua, baadaye anaghairi. Hali hiyo ilituchanganya wananchi na kuanza kujiuliza ana mpango gani hasa,” amesema.

Naye Ally Mussa amesema wasiwasi wao umeongezeka kutokana na namna mwekezaji huyo alivyoanza shughuli zake bila kutoa maelezo ya wazi kwa jamii inayozunguka eneo la mradi.

Amedai wananchi wengi wanahofia aina ya mwani unaotarajiwa kupandwa unaweza kuathiri shughuli zao za uvuvi kutokana na eneo lililochaguliwa kwa ajili ya mradi huo.

“Tunampinga kwa sababu hatukueleweshwa vizuri kuhusu mradi wake. Tulipojaribu kufanya vikao naye, baadhi yetu tukagundua kuwa aina ya mwani anaotaka kupanda inaweza kuathiri maeneo yetu ya uvuvi,” amesema Ally.

Kwa upande wake, Shaibu Mtavanga, mkazi wa Mnazi, amesema changamoto kubwa ni kukosekana kwa uwazi na ushirikishwaji wa wananchi tangu hatua za awali za uwekezaji huo, hali ambayo imeongeza taharuki katika vijiji hivyo.

Amesema endapo Serikali na mwekezaji wangeanza kwa kutoa elimu na maelezo ya kina kuhusu mradi huo, huenda usingekumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wananchi.

“Mwekezaji akishapokelewa TIC anatakiwa ashuke hadi mkoani, wilayani, halmashauri na kwenye vijiji husika kabla ya kuanza shughuli zake. Hapo ndipo wananchi wanapaswa kupewa maelezo na kushirikishwa,” amesema.

Wananchi hao pia wameeleza kuwa hofu kubwa waliyonayo ni usalama wa maeneo ya uvuvi ambayo yamekuwa tegemeo la maisha yao kwa miongo mingi.

Mbali na kupinga uwekezaji huo, baadhi yao wamedai walijaribu kumshauri mwekezaji huyo kuanza kujenga mahusiano mazuri na jamii kwa kusaidia miradi ya maendeleo kabla ya kuanza shughuli zake.

Wananchi hao walimtaka kusaidia kukamilisha ujenzi wa ofisi ya kijiji, kuanzisha shule shikizi pamoja na kuchangia ujenzi wa barabara ili kujenga imani kwa jamii.

“Tulimshauri amalizie ujenzi wa ofisi ya kijiji, aanzishe shule shikizi na kusaidia barabara, lakini alisema hawezi kufanya chochote kwa jamii hadi aanze kupata faida kutokana na shughuli zake. Kauli hiyo ilituongezea wasiwasi,” amesema Hamisi Kalyasi, mkazi wa Milamba.

Baada ya kusikiliza malalamiko na hoja zilizotolewa na wananchi, Mwaipaya, alitoa maelekezo ya kusitishwa mara moja kwa shughuli zote zinazohusiana na uwekezaji huo hadi pale utaratibu rasmi wa ushirikishwaji wa wananchi utakapokamilika.

Baadhi ya wananchi  wa vijiji vinavyounda kata ya Nalingu wakiwa kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Nalingu, wilayani humo.

Mwaipaya aliwaagiza viongozi wa Serikali katika ngazi za wilaya, halmashauri na vijiji kuanza upya mchakato wa uwekezaji huo kwa kuhakikisha wananchi wanapatiwa taarifa sahihi na kushirikishwa kupitia mikutano ya hadhara itakayotoa nafasi kwa jamii kuelewa mradi huo na kutoa maoni yao.

Amesema Serikali haitamruhusu mwekezaji yeyote kuanza shughuli katika eneo lolote bila kwanza kupata ridhaa na ushirikiano wa wananchi wanaomiliki rasilimali za eneo husika.

“Hakuna mwekezaji anayekuja sehemu akaanza tu kuwekeza bila kupita kwenye ngazi za wananchi ambao ndio wamiliki wa rasilimali,” amesema Mwaipaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *