Vinywaji vya sukari vinavyowasababishia wanaume uparaVinywaji vya sukari vinavyowasababishia wanaume upara

Mwanza. Watafiti wanaonya kuwa huenda kuna uhusiano kati ya unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi na upotevu wa nywele kwa wanaume, hali inayoweza kuongeza hatari ya kupata upara kwa wanaume wanaopendelea matumizi ya vinywaji hivyo kwa wingi.

Upara kwa wanaume unaojulikana kitabibu kama ‘Androgenetic alopecia’ ni hali ya kawaida inayowapata mamilioni ya wanaume duniani.

Kwa muda mrefu, wataalamu wamekuwa wakihusisha hali hii na vinasaba na homoni, lakini utafiti wa hivi karibuni unaonesha lishe hasa sukari inaweza kuchangia hali hiyo.

Utafiti uliofanywa na watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Tsinghua nchini China kupitia kitivo chake cha afya ya umma kinachojulikana kama Vanke School of Public Health, umeonyesha uwezekano wa uhusiano kati ya unywaji wa vinywaji vyenye sukari nyingi na upotevu wa nywele kwa wanaume.

Utafiti huo ulioongozwa na mtaalamu wa epidemiolojia ya lishe,  Ai Zhao ulichapishwa mwaka 2023 katika jarida la Nutrients ukishirikisha wanaume 1,028 wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45.

Washiriki waliulizwa kuhusu matumizi ya vinywaji kama soda, vinywaji vya kuongeza nguvu,  juisi zenye sukari iliyoongezwa, chai au kahawa yenye sukari, pamoja na maziwa matamu.

Matokeo yalionyesha kuwa wanaume waliokunywa vinywaji hivyo zaidi ya mara saba kwa wiki,  walikuwa na uwezekano wa mara 3.36 zaidi wa kupata dalili za upotevu wa nywele ukilinganisha na wale waliotumia kidogo au kutotumia kabisa.

Hata hivyo, watafiti wamesisitiza kuwa matokeo haya hayawezi kuthibitisha moja kwa moja kwamba sukari ndiyo chanzo cha upara, bali yanaonyesha uhusiano unaohitaji utafiti zaidi.

Ai Zhao amesema utafiti huo ulikuwa wa uchunguzi, hivyo haukuwa majaribio ya moja kwa moja ya kitabibu.

Upara wa wanaume ni nini?

Utafiti unaonyesha kuwa upara wa wanaume ni hali ya kawaida duniani na huathiri sehemu kubwa ya wanaume kadri wanavyozeeka.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi asilimia 15 ya wanaume wenye umri wa miaka 18 hadi 29 huanza kuona dalili za upotevu wa nywele, na kiwango hiki huongezeka hadi asilimia 50 kwa wanaume wa miaka 40 hadi 49.

Watafiti wamependekeza mchakato wa kibaiolojia unaoitwa ‘polyol pathway, ambapo sukari ya kawaida mwilini  hubadilishwa kuwa sukari inayopatikana kwenye matunda na vyakula vitamu, kisha baadaye kuwa mafuta yanayotumika na kuhifadhiwa mwilini kama chanzo cha nishati.

Mchakato huu unaweza kuathiri seli za mizizi ya nywele  ambazo ni muhimu katika ukuaji wa nywele. Hata hivyo, watafiti wanasema hii bado ni nadharia inayotokana zaidi na tafiti za wanyama na maabara.

Tafiti za wanyama na ushahidi wa awali

Tafiti za maabara, hasa zilizomhusisha panya zinaonyesha kuwa ulaji wa sukari kupita kiasi,  unaweza kuathiri metabolism ya seli za mizizi ya nywele. Hii inaongeza uwezekano wa uhusiano kati ya lishe na afya ya nywele, lakini bado haijathibitishwa kwa binadamu.

Tafiti nyingine zinaonyesha kuwa lishe yenye sukari nyingi, mafuta mabaya na vyakula vilivyosindikwa inaweza kuongeza uchochezi mwilini. Uchochezi huu unaweza kuathiri ngozi ya kichwa na mzunguko wa damu kwenye mizizi ya nywele.

Pia upungufu wa virutubisho kama chuma zinc, vitamin D na protein umehusishwa na kudhoofika kwa nywele, ingawa si chanzo kikuu cha upara wa kurithi.

Sababu kuu ya upara kwa wanaume

Wataalamu wanasema sababu kuu ya upara kwa wanaume bado ni urithi wa vinasaba na homoni ya DHT (dihydrotestosterone), ambayo husababisha mizizi ya nywele kupungua hatua kwa hatua na hatimaye kusimama kuzalisha nywele.

Matumaini kurejesha nywele

Wakati upara kwa wanaume ukiendelea kuwa changamoto kubwa ya kiafya na kisaikolojia, tafiti za kisayansi zinaanza kuonyesha dalili za matumaini kuhusu uwezekano wa kurejesha nywele.

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sheffield nchini Uingereza na Chuo Kikuu cha COMSATS kilichopo Islamabad, Pakistan wanaendelea na tafiti za awali kuhusu matumizi ya mafuta maalum kwa ajili ya kuchochea ukuaji wa nywele.

Kwa mujibu wa tafiti hizo za awali zilizofanyika kati ya mwaka 2022 na 2023, watafiti waligundua kuwa baadhi ya mafuta yana uwezo wa kuamsha mizizi ya nywele iliyokuwa imelala. Mizizi hii inapochochewa inaweza kuanza tena kuzalisha nywele.

Katika majaribio ya maabara na kwa wanyama, ilionekana kuwa matumizi ya mafuta hayo yaliongeza shughuli za seli muhimu zinazohusika na ukuaji wa nywele, hasa zile zinazojulikana kama ‘keratinocytes’.

Mbali na hilo, tafiti nyingine zimeangalia matumizi ya dawa kama Minoxidil na Finasteride ambazo tayari zinatumika kusaidia kupunguza kasi ya upotevu wa nywele na kwa baadhi ya watu kusaidia ukuaji mpya wa nywele.

Hata hivyo, wataalamu wanasema matokeo ya tafiti za mafuta bado yako katika hatua za awali, hivyo hayajathibitishwa kikamilifu kwa binadamu kupitia majaribio makubwa ya kitabibu.

Aidha, watafiti wanaendelea kuchunguza teknolojia nyingine kama matumizi ya seli shina (stem cells) na tiba za kijenetiki ambazo zinaweza kuwa suluhisho la kudumu kwa upara siku zijazo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *