TABORA: SERIKALI kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya Idara ya Mambo ya Kale inatarajia kuanisha wazi vivutio vya mambo ya kale katika mkoa wa Tabora yakiwemo Makumbusho ya Dk David Livingstone, ziweze kufahamika duniani kuwa ni sehemu ya vivutio vya utalii kwa ajili ya kukuza sekta ya utalii kiuchumi.
Waziri wa Wizara hiyo, Dk Ashatu Kijaji amesema hayo mkoani Tabora kuwa kazi hiyo tayari imeanza kufanyika ili mambo ya kale yaliyopo katika mkoa huo yaweze kutambuliwa duniani na vivutio vya utalii kwa mkoa huo na kuwezesha wananchi kunufaika kiuchumi na historia njema ya mkoa wa Tabora.

“Naomba nikuahidi Idara yetu ya Mambo ya Kale wiki ijayo itakuwa Tabora, kazi ambayo wameanza kuifanya ili malikale hizi tuzipeleke duniani viwe vivutio vya utalii,” amesisitiza Dk Kijaji.
Mambo ya kale zinazoelezwa ni Mji Mkongwe wa Tabora, Makumbusho ya Dk David Livingstone, Kisima cha Livingstone (Livingstone’s Well), Boma la Wajerumani Nyumba za Waarabu wa Kale, Njia za Misafara ya Kale na Mji wa Kale wa Uyui (Kazeh) Kazeh Historic Site.
Katika hatua nyingine ,Mhifadhi Mkuu wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Aloyce Kilemwa amesema TFS wilaya ya Tabora imetenga Sh milioni 77 katika mwaka wa fedha wa 2026/2027 kuanzisha kivutio maalumu cha utalii ikolojia kwenye hifadhi ya msitu wa Igombe uliona bwawa ndani yake.

Kilemwa ambaye ni Mhifadhi wa Misitu wa wilaya ya Tabora amesema mwaka wa fedha 2025/2026 zilitengwa Sh milioni 20 na kuwezesha kufanya maandalzi ya awali.
“TFS wilaya ya Tabora inalenga katika kuanzia eneo maalum la utalii ikolojia kwa watu kutembelea , kupumzika ndani ya hifadhi ya msitu,”amesema Kilemwa.
Kilemwa amesema hifadhi hiyo ni eneo muhimu kwa ajili ya utalii ikolojia na kwamba litawekwa maeneo maalumu yakiwemo ya kupokelea wageni na huduma nyingine nyinginezo wenye kuzingatia uhifadhi ikolojia.
Amesema zitatengenezwa njia malaumu za watu kutembea na kuzunguka bwawa na kwenye miinuko uliyopo ndani ya hifadhi ya m situ wa Igombe.

Kilemwa amesema wananchi watapata fursa ya utalii wa kupanda boti ndani ya m aji kwa kupiga makasia, kuvua Samaki , kuiona Wanyama wadogo ngedere , digidigi, na ndege pia uwekaji mizinga ya nyuki na kuanzisha huduma za tiba ya nyuki kwa binadamu ili kuongeza kina za mwili.
Kwa upande wake Mtaalamu wa Utalii wa TFS, Elisa Evarister amesema Bwawa la Igombe lenye mzunguko wa takribani kilometa 12 na kina cha maji takribani mita tano liliiunduliwa mwaka 1958 na Gavana wa Kiingereza Sir Edward Twining likiwa maalumu kwa matumizi ya maji katika mji wa Tabora ambao sasa ni Manispaa.
