
Unguja. Ni dhahiri sasa Zanzibar imedhamiria kumaliza maambukizi ya ugonjwa wa malaria, baada ya kuanza mapambano hayo kwa njia za kisasa zaidi.
Hii ni baada ya kuzinduliwa mradi maalumu wa kutumia ndege nyuki, kutambua na kuangamiza mazalia ya mbu katika kuhakikisha Zanzibar inafikia malaria sifuri.
Wizara ya Afya inasema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kumaliza malaria Zanzibar.
Katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2026/27 iliyowasilishwa na Kaimu Waziri wa wizara hiyo, Dk Saada Mkuya katika mkutano wa bajeti wa Baraza la Wawakilishi Mei 19, 2026 alisema mwaka wa fedha 2025/26, washukiwa wa malaria walikuwa 492,513 kati ya hao Unguja ni 394,014 na Pemba ni 98,499.
Kati ya hao waliochunguzwa, wananchi 7,654, Unguja 7,190 na Pemba 484 sawa na asilimia 1.6 waligundulika kuwa na vimelea vya malaria.
Alisema katika juhudi za kudhibiti mbu waenezao malaria, kazi ya upigaji dawa majumbani imefanyika katika wilaya nane (Unguja tano na Pemba tatu).
Nyumba 3,564 (Unguja 2,436 na Pemba 1,128) zimepigwa dawa ya kuuwa mbu waenezao malaria.
“Aidha, vyandarua 16,841 vyenye dawa ya muda mrefu vimetolewa katika wilaya zote kupitia kliniki ya mama na mtoto katika vituo vya afya,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk Saada, afua hizo zimesaidia kupunguza wagonjwa wa malari kutoka 22,102 mwaka 2024/25 hadi kufikia 17,118 mwaka 2025/26.
Mradi wazinduliwa
Mradi huo wa Teknolojia Mahiri ya Drones kwa Zanzibar isiyo na Malaria (Smart Drone Technology for a Malaria-Free Future in Zanzibar), ni mradi shirikishi kati ya Wizara ya Afya Zanzibar kupitia Mpango wa Zanzibar wa Kutokomeza Malaria (ZAMEP), Shirika la Afya Duniani (WHO), SORA Technology ya Japan, na Taasisi ya Afya ya Ifakara (IHI), ukifadhiliwa na Serikali ya Japan kwa gharama ya Sh1 bilioni.
Akizungumza wakati wa kuzindua mradi huo Mei 13, 2026, Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dk Miraji Mngereza Mzee alisema ni kwa mara ya kwanza Zanzibar kuwa na mradi unaohusisha mambo mawili; teknolojia na ushirikishaji wa jamii katika kuteketeza jambo hilo.
“Kwa miaka mingi kumekuwepo na changamoto ya malaria lakini kwa Zanzibar ipo chini ya asilimia moja na kwasasa baada ya kutumia teknolojia hii na kuihusisha jamii, tunaamini tunakwenda kuandika historia ya kutokuwa na malaria Zanzibar…Inatakiwa kuwa huru kutokuwa na malaria na iweze kutambuliwa duniani kama nchi ambayo haina maambukizi ya malaria,” anasema Dk Mngereza.
Kwa mujibu wa Katibu mkuu huyo, kupitia matumizi ya teknolojia hiyo, watakuwa na uwezo wa kuyafikia maeneo ambayo hayafikiki kwa njia za kawaida wakati huohuo kutumia ndege nyuki hizo kuangamiza vimelea vyote vya mbu kwa muda mfupi, badala ya kutumia siku tatu kwa utaratibu wa kawaida lakini teknolojia ikibaini inaangamiza mara moja.
Naye Mkurugenzi Kinga na Elimu Wizara ya Afya, Dk Salim Slim anasema mradi huo unakwenda kuleta mabadiliko makubwa kuhakikisha Zanzibar malaria inakwisha kabisa.
Anasema kwa sasa kiwango cha maambukizi ya malaria kipo asilimia 0.04 na inakaribia kumaliza kabisa, hivyo katika jitihada hizo muda mfupi watafanikisha azma hiyo kuangamiza mazalia ya mbu.
“Kuna maeneo ambayo binadamu hawezi kufika, kwahiyo kwa kutumia ndege nyuki tutafika mbali, kwanza zitakuwa na uwezo wa kutiwa dawa na kunyunyuzia maeno tofauti, kwhiyo itapunguza gharama kubwa za kutumia njia za kawaida,” anasema Dk Slim
Hata hivyo, anasema bado malaria ipo na inaua na kwamba takwimu zinaonesha kwamba malaria inaathiri vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 40, kwa sababu mara nyingi wanakuwa nje na kujikusanya kwenye vibanda na ndio wanaoonekana wapo hatarini ikilinganishwa na rika nyingine hivyo akawataka kuendelea kuchukua tahadhari.
Anasema kwa upande wa Pemba, wanatarajia ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2027 hakutakuwa na malaria tena lakini lazima wapunguze mazalia yao na kuharibu vizazi vya mbu.
Naye mwakilishi kutoka Ubalozi wa Japan, Jin Hashmoto anasema serikali ya Japan inaendelea kuhakikisha inasaidia changamoto zinazoikabili jamii kwa kutumia teknolojia, ubunifu na utaalamu mbalimbali.
Anasema wanaamini katika kutumia teknolojia hiyo, itasaidia kupunguza kuzaliana kwa mbu na kuondoa mazalia yao.
“Tunaamini mradi pia utasadia kupata takwimu sahihi za zenye ushahidi kuhusu malaria kwa nchi., Afya inabaki sekta ya kipaumbele kwa Japan,” anaeleza.
Tamko la WHO
Mkuu wa Ofisi ya Uhusiano ya WHO Zanzibar, Dk Ndoungou Salla BA, anasema Wizara ya Afya kupitia ZAMEP, itatoa uongozi wa kimkakati, uratibu wa kisheria, na usimamizi wa utekelezaji ili kuhakikisha ujumuishaji wa usimamizi wa vyanzo vya viwavi kwa kutumia ndege nyuki katika mifumo ya kitaifa ya udhibiti wa malaria.
“WHO itatoa uongozi na uratibu wa jumla ili kuhakikisha upatanifu wa kimkakati, ubora wa kiufundi, na ushirikiano mzuri baina ya washirika,” anasema Dk Salla na kuongeza kuwa SORA Technology itasambaza mifumo ya ndege nyuki, huku ikisaidia ujenzi wa uwezo wa ndani na utekelezaji unaoongozwa na data.
“Tunapongeza Serikali ya Zanzibar kupitia ZAMEP kwa uongozi imara na dhamira endelevu ya kutokomeza malaria. Mafanikio ya Zanzibar ya kudumisha kiwango cha maambukizi ya malaria chini ya asilimia moja, yanaonyesha kinachowezekana kupitia uwekezaji, ushirikiano na ubunifu endelevu,” anasema Dk Salla.
Mradi huu unaleta uvumbuzi wa hali ya juu wa ndege nyuki na Akili Unde, ili kuboresha utambuzi na usimamizi wa maeneo mbu wanapotaga mayai.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, ubunifu huu unajumuisha, upigaji ramani kwa anga wa makazi ya viwavi yenye hatari kubwa, ufuatiliaji wa kiwadudu ili kubaini aina za mbu wanaosambaza malaria, upigaji ramani wa utabiri ili kulenga kwa usahihi maeneo ya kuzaliana kwa ajili ya unyunyiziaji wa dawa ya kuua viwavi.
