Ndoto ya Arsenal katikati ya usingizi wa PSGNdoto ya Arsenal katikati ya usingizi wa PSG

LONDON, ENGLAND. Kocha Mikel Arteta yuko karibu kuandika historia mpya, huku Arsenal wakijiandaa kwa usiku mkubwa zaidi wa maisha yake ya ukocha katika fainali ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Paris Saint-Germain keshokutwa Jumamosi.

Baada ya kumaliza ukame wa miaka 22 bila ubingwa wa Ligi Kuu England, sasa Arteta ana nafasi ya kuiongoza Arsenal kutwaa ubingwa wa Ulaya kwa mara ya kwanza katika historia yao.

The Gunners wamerejea kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 20 tangu walipopoteza dhidi ya FC Barcelona mjini Paris mwaka 2006 baada ya kuwatoa Atlético de Madrid katika nusu fainali iliyokuwa na ushindani mkubwa.

Bao la Bukayo Saka lilikuwa tofauti kubwa katika michezo hiyo miwili na kuipa Arsenal tiketi ya kucheza fainali hiyo.

Kati ya Arsenal na historia ya milele wanasimama mabingwa watetezi PSG, ambao waliitoa FC Bayern Munich kwa jumla ya mabao 6-5 na kufika fainali kwa msimu wa pili mfululizo na mara ya tatu tangu msimu wa 2019-20.

Hii pia ni marudio ya nusu fainali ya msimu uliopita, ambayo PSG walishinda kwa jumla ya mabao 3-1 kabla ya kuifunga Inter Milan mabao 5-0 mjini Munich na kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yao.

Kikosi cha Luis Enrique kilishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Emirates kabla ya kuhimili mashambulizi ya Arsenal mjini Paris na kushinda 2-1 katika mchezo wa marudiano.

Lakini imani ndani ya kambi ya Arsenal haijawahi kuwa kubwa kiasi hiki. Kikosi hicho kilisherehekea ubingwa wao wa Premier League katika sherehe ya siri jijini London mapema wiki hii, ambapo Arteta aliwaambia wachezaji kuwa wako karibu kuandika historia.

Ametangaza: “Nina uhakika tutashinda Ligi ya Mabingwa.”

Nahodha Martin Ødegaard alikiri kuwa hali ya furaha ndani ya klabu imekuwa ya kipekee tangu Arsenal walipotwaa ubingwa.

Akizungumza baada ya mechi ya Jumapili dhidi ya Crystal Palace FC amesema: “Tulikuwa na sherehe nzuri Jumanne. Hali ya furaha ni ya ajabu. Kila mtu ana furaha sana.

“Lakini bado tuna fainali nyingine kubwa ndani ya wiki moja, hivyo tutasubiri kusherehekea zaidi hadi baada ya hiyo.

“Kama tukifanikiwa kufanya hivyo, itakuwa jambo la ajabu sana. Tunaishi ndoto kushinda Ligi Kuu na kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa.”

Maandalizi ya Arsenal yamekuwa magumu kutokana na kuongezeka kwa majeraha ya wachezaji.

Noni Madueke sasa yuko kwenye mashaka baada ya kupata tatizo la misuli ya nyuma ya paja katika mchezo dhidi ya Crystal Palace kabla ya nafasi yake kuchukuliwa na Viktor Gyökeres.

Jurrien Timber pia anapambana kurejea akiwa fiti baada ya kukosa zaidi ya miezi miwili kutokana na jeraha la kifundo cha mguu alilopata dhidi ya Everton mwezi Machi.

Bado kuna matumaini kuwa anaweza kucheza mjini Budapest, ingawa kuanza kikosi cha kwanza kunaonekana kuwa vigumu.

Mchezaji mmoja ambaye amethibitishwa kuukosa mchezo huo ni Ben White, ambaye yuko nje kutokana na jeraha kubwa la goti.

White alikuwa ameonyesha kiwango kizuri wakati Timber akiwa majeruhi na alitarajiwa kuanza kama beki wa kulia kwenye fainali hiyo.

Hali hiyo inaweza kumlazimisha Arteta kumtumia Cristhian Mosquera, huku Piero Hincapié akiwa chaguo jingine licha ya kutokuwa na uzoefu mkubwa katika nafasi hiyo.

Kulikuwa pia na habari njema baada ya Mikel Merino kurejea kutoka nje ya uwanja kwa miezi minne kufuatia upasuaji wa mguu na kucheza kama mchezaji wa akiba dhidi ya Crystal Palace.

PSG pia wana wasiwasi wa majeraha kuelekea fainali hiyo.

Beki nyota Achraf Hakimi bado hajarejea mazoezini baada ya kupata jeraha la misuli ya nyuma ya paja katika mchezo wa kwanza dhidi ya Bayern Munich.

Mmorocco huyo anachukuliwa kuwa mmoja wa mabeki bora wa kulia duniani na kukosekana kwake kutakuwa pigo kubwa kwa Luis Enrique.

Kijana nyota Warren Zaïre-Emery alicheza kama beki wa kulia katika mchezo wa marudiano na kuonyesha kiwango kizuri, huku Fabián Ruiz akicheza kiungo pamoja na Vitinha na João Neves.

Ousmane Dembélé pia ni wasiwasi mwingine baada ya kupata tatizo la paja mapema mwezi huu, ingawa PSG bado wana matumaini kuwa atakuwa fiti.

Kipa wa akiba Lucas Chevalier pamoja na kinda Quentin Ndjantou wote wako nje kutokana na majeraha.

Fainali ya Jumamosi inaahidi kuwa pambano la kusisimua la mitindo tofauti ya soka.

Mashambulizi makali ya PSG na soka lao la ujasiri chini ya Luis Enrique vitajaribu uimara wa Arsenal ambao bado hawajapoteza mchezo wowote katika Champions League msimu huu.

Historia inaonyesha kuwa mchezo mwingine wa kusisimua unaweza kushuhudiwa.

Arsenal waliifunga PSG mabao 2-0 katika hatua ya ligi mapema msimu huu baada ya awali kutoka sare ya 1-1 na 2-2 katika hatua ya makundi msimu wa 2016-17.

Mwaka 1994, The Gunners pia waliitoa PSG katika robo fainali ya European Cup Winners’ Cup kabla ya kwenda kushinda taji hilo.

Sasa Arteta na wachezaji wake wako umbali wa mchezo mmoja tu kutoka usiku mkubwa zaidi katika historia ya Arsenal.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *