
Dar es Salaam. Wataalamu wa sheria wamesema matumizi ya nembo za taifa kinyume na taratibu zilizowekwa kisheria ni kosa linaloweza kumuweka mtu hatarini kukabiliwa na adhabu ya faini au kifungo cha jela, au vyote kwa pamoja.
Wamesema nembo za taifa, ikiwemo bendera, wimbo wa taifa na alama nyingine rasmi za Serikali, zinalindwa kisheria na zinapaswa kutumiwa kwa heshima na kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa na mamlaka husika.
Kwa mujibu wa wataalamu hao, sheria inaweka bayana kuwa mtu yeyote atakayezitumia nembo hizo kwa njia inayopotosha, kudhalilisha au isiyoidhinishwa anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, wamesema lengo la sheria hizo ni kulinda hadhi ya taifa na kuhakikisha alama hizo zinabaki kuwa ishara ya umoja, mamlaka na heshima ya nchi.
Wamefafanua kuwa mara nyingi makosa hayo hutokea kupitia matumizi yasiyo sahihi ya bendera au alama za taifa katika biashara, matangazo au mitandao ya kijamii bila kibali.
Ufafanuzi huo wa wanasheria unakuja kufuatia taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida kutangaza kumtafuta Kassimu Ally Juma (34), mkazi wa Kata ya Unyambwa, kwa tuhuma za kupandisha bendera tano zinazofanana na bendera ya Taifa katika shamba lake pamoja na bango lenye ujumbe uliosema ‘Uzinduzi wa Mapenzi’.
Kulingana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Amon Kakwale, tukio hilo lilibainika Mei 26, 2026 majira ya saa tano usiku baada ya Jeshi la Polisi kupokea taarifa kutoka kwa wananchi.
Akifafanua tukio hilo kwa mujibu wa sheria, Wakili wa kujitegemea Edson Kilatu amesema nembo za taifa ni mali za Serikali.
Wakili Kilatu ameeleza kuwa, Sheria ya Nembo za Taifa (The National Emblems Act Cap. 10 ilivyofanyiwa mabadiliko 2023), kifungu cha 6 kinasema:
“Ni kosa la jinai kutumia Nembo za Taifa au mifano kama trade mark kutangazia bidhaa au kitu chochote kilichouzwa au kinachouzwa kwenye matangazo ya biashara na matumizi mengine ambayo Waziri wa Mambo ya Ndani hajatoa ruhusa ya kutumia,” amesema.
Wakili Kilatu ametaja nembo zenyewe ni bendera ya taifa, Coat of Arms (wengi wanaiita Bibi na Bwana) na Mihuri ya Taifa.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu yeyote akikiuka masharti au vigezo vilivyowekwa na Waziri, anatenda kosa la kisheria.
Amesema mtu huyo akipatikana na hatia anaweza kutozwa faini isiyozidi Sh20,000 au kufungwa jela kwa muda usiozidi miaka miwili, au kupewa adhabu zote mbili kwa wakati mmoja.
Wakili Kilatu akizungumzia tukio lililofanywa na kijana huyo, amesema inaweza kutafsiriwa kama dhihaka na endapo mahakama ikiridhika, kosa hilo linatambulika kama kosa la jinai.
Kwa upande wake, Wakili Ibrahim Bendera amesema kulingana na sheria ni lazima Waziri wa Mambo ya Ndani ndiye aruhusu matumizi mengine ya nembo za taifa.
Kwa mantiki hiyo amesema kushonea bendera kwenye nguo, kuvaa nguo zenye bendera au kuweka vifungo ni kosa kwa kuwa Waziri hakutoa maelekezo hayo.
Japo, Wakili Bendera amesema watu wanaokamatwa kwa tuhuma hizo hawatabainika kutenda kosa hadi pale Mkurugenzi wa Mashtaka Tanzania (DPP) mwenye mamlaka ya kuthibitisha kama mtuhumiwa ana kosa la kujibu.
Sheria hiyo ya Nembo za Taifa inaipa mamlaka Serikali, kupitia Rais, kuamua ni lini na kwa tukio gani bendera itashushwa nusu mlingoti.
Hili linafanyika kwa tangazo rasmi kupitia vyombo vya habari au waraka wa kiserikali.
