
Leo ni Jumamosi tarehe 13 Dhulhija 1447 Hijria sawa na 30 Mei mwaka 2026.
Miaka 282 iliyopita katika siku kama ya leo, Alexander Pope mshairi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiingereza aliaga dunia.
Alizaliwa mjini London Mei 21 mwaka 1688 katika familia ya kitajiri. Hata hivyo kutokana na kuwa na ulemavu wa viungo, baba na mama yake walimlea nje ya mji katika nyumba moja. Alipofikisha umri wa miaka 15 Alexander Pope alikuwa tayari anazifahamu vyema lugha za Kigiriki, Kifaransa na Kitaliano. Alichapisha diwani yake ya kwanza ya mashairi alipokuwa na umri wa miaka 23. ****
Siku kama ya leo miaka 248 iliyopita sawa na tarehe 30 Mei 1778, Francois – Marie Arouet maarufu kwa jina la Voltaire, mwanafalsafa na mwandishi wa Kifaransa alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 84.
Katika maisha yake, Voltaire aliwahi kuwekwa mahabusu mara mbili na kubaidishwa kwa muda wa miaka mitatu nchini Uingereza.
Kitendo hicho kilimkasirisha sana Voltaire na kumfanya kuwa dhidi ya utawala wa Ufaransa. ***
Tarehe 13 Dhilhija miaka 109 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran.
Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza.
Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni. ****
Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita, alifariki dunia Ali Akbar Khan Nafisi aliyejulikana kama Naadhimul Atibaa, daktari na mtaalamu wa lugha wa Kiirani, katika mji wa Tehran.
Baada ya kumaliza masomo yake ya msingi alianza kujifunza masomo ya kidini na udaktari katika chuo cha Darul Funun cha Tehran. Baadhi ya vitabu vilivyoandikwa na Naadhimul Atibaa katika uwanja wa tiba vimetarjumiwa katika lugha za kigeni.
Ali Akbar Khan Nafisi ambaye pia alikuwa mtaalamu wa lugha alifanya jitihada kubwa katika kukusanya maneno ya lugha ya Kifarsi na kuandika kamusi inayoitwa ‘Kamusi ya Nafisi.’ ***
Tarehe 30 Mei 1981, aliuawa Ziaur Rahman, Rais wa Bangladesh baada ya kupigwa risasi katika mji wa Chittagong ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo.
Rais Ziaur Rahman aliuawa baada ya kuchungulia dirishani kwenye nyumba ya wageni ya serikali katika mji huo. Watu wanane waliuawa kwenye shambulio hilo, wakiwemo wasaidizi na walinzi wa rais huyo. ***
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu, Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu.
Allamah Agha Bozorge Tehrani alikweya kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za nchi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la “Adhari’a ila Tasaanifish Shia”. Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni “Tabaqatu Aalami Shia” chenye juzuu 8.