
Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele amesema Mradi Shirikishi wa Wasindikaji na Wazalishaji wa Maziwa (TI3P) una mchango mkubwa katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa nchini kwa kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji wa maziwa.
Dk Madele amesema hayo leo Mei 30, 2026 alipotembelea banda la Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) katika Maonesho ya 29 ya Wiki ya Maziwa yanayoendelea katika Viwanja vya Mwembetogwa mkoani Iringa.
Amesema mradi huo umeendelea kuwa chachu ya maendeleo ya sekta ndogo ya maziwa kwa kuwawezesha wafugaji kuongeza uzalishaji na tija.
“Mradi huu una mchango mkubwa katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa maziwa kwa kuwaunganisha wazalishaji na wasindikaji. Ni muhimu kuongeza nguvu katika kuwaunganisha wafugaji na wadau wengine wa sekta hii pamoja na kuimarisha vyama vya ushirika ili kuwawezesha wafugaji wadogo kuongeza uzalishaji, tija na ushindani,” amesema Dk Madele.
Katika ziara hiyo, alipokea taarifa ya utekelezaji wa mradi kutoka kwa Mratibu wa TI3P, Joseph Mabula.
Akitoa taarifa hiyo, Mabula amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo Machi 2022, jumla ya wafugaji wadogo 92,831 pamoja na wadau wa mnyororo wa thamani wa maziwa kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wamenufaika, ambapo asilimia 30 ya wanufaika ni wanawake.
Amesema mradi huo wa miaka minne unafadhiliwa na TADB kwa kushirikiana na Bill & Melinda Gates Foundation na kutekelezwa kwa ushirikiano wa Heifer International, Land O’Lakes Venture37 pamoja na Tanager.
“Mradi unalenga kutatua changamoto mbalimbali zilizopo katika mnyororo wa thamani wa sekta ndogo ya maziwa ili kuongeza uzalishaji na kuboresha kipato cha wafugaji wadogo nchini,” amesema Mabula.
Kwa mujibu wa Mabula, tangu kuanza kwa mradi huo zaidi ya Sh42 bilioni zimetolewa kama mikopo kwa wasindikaji wa maziwa, wafugaji, wasambazaji wa pembejeo na wadau wengine wa sekta hiyo.
Amesema fedha hizo zimechangia kuanzishwa kwa viwanda vipya vya kuchakata maziwa pamoja na upanuzi wa viwanda vilivyopo, ambapo jumla ya viwanda 17 vya usindikaji vimefikiwa kwa uwekezaji wa Sh22.8 bilioni.
“Mradi umewezesha ununuzi wa mitamba 3,330 yenye thamani ya zaidi ya Sh11.09 bilioni, hatua iliyochangia kuongeza uzalishaji na tija katika sekta ya maziwa nchini,” amesema.
Mabula amesema wafugaji wameendelea kupata huduma za ugani, pembejeo bora, masoko na huduma za kifedha kwa ajili ya uwekezaji katika sekta hiyo, huku wasindikaji 19 wa maziwa wakinufaika na programu za kujengewa uwezo na kuongeza ufanisi wa uzalishaji.
Akizungumzia ushirikishwaji wa kijinsia, amesema TADB imetoa ruzuku linganifu yenye thamani ya Sh1.4 bilioni kwa wafugaji wadogo 1,216, wakiwemo wanawake 397.
“Ruzuku hii imelenga kupunguza changamoto za upatikanaji wa mitamba bora, kuongeza uzalishaji na uchakataji wa maziwa pamoja na kuhamasisha uwekezaji katika mnyororo wa thamani wa maziwa nchini,” amesema Mabula.