Mshauri mwandamizi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ameonya kuwa Rais wa Marekani Donald Trump anaisaliti diplomasia na kuupa nafasi mwelekeo wa vita kwa mara ya tatu, kutokana na kile alichokitaja kuwa ni hatua zake za kichokozi.

Katika chapisho kwenye akaunti yake ya X siku ya Jumamosi, Mohsen Rezaei aliandika: “Kama ilivyotabiriwa, Rais wa Marekani anaendelea kuisaliti diplomasia kwa mara ya tatu.”

Ameongeza: “Kwa kuendeleza mzingiro wa baharini na kuweka matakwa yaliyopita kiasi katika mazungumzo, amethibitisha zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwamba yeye si mtu wa mazungumzo, bali anafuata malengo mengine.”

Rezaei, ambaye pia aliwahi kuwa kamanda mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), hapo awali aliambia mtandao wa China wa CGTN kwamba Iran “itauvunja mzingiro ama kwa mazungumzo au, ikishindikana, kwa hatua ya moja kwa moja.”

Pia aliwahi kusema kuwa Wamarekani hawana budi ila kufanya mazungumzo, na kwamba kuendelea kwa vita hivi kutawaingiza kwenye “handaki lenye kiza”.

Kwingineko Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, ametangaza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iko tayari kufikia “mfumo wenye heshima” wa kumaliza vita na mvutano katika eneo hilo.

Ofisi ya rais, imetoa taarifa mpya Jumamosi kuhusu mazungumzo ya simu yaliyofanyika Jumanne kati ya Masoud Pezeshkian na Amir wa Qatar, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani, ikisema kuwa Pezeshkian alisisitiza kwamba Iran imekuwa ikithibitisha mara kwa mara uaminifu wake na dhamira yake ya kushikamana na mkondo wa mazungumzo.

Kwa upande wake, Sheikh Tamim bin Hamad Al Thani alisisitiza msimamo thabiti wa Doha na kusema kuwa serikali ya Qatar haitasita kufanya kila iwezalo katika kuimarisha amani, usalama na uthabiti wa kikanda, na itaendelea kutekeleza wajibu wake wa kujenga na wa upatanishi.

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *