
Shirika la Afya Duniani (WHO) limesema kuwa kiwango cha vifo katika mripuko wa sasa wa ugonjwa wa Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ni kati ya asilimia 30 na 50, huku mkuu wa shirika hilo akizuru nchi hiyo kusaidia juhudi za kuudhibiti ugonjwa huo hatari.
Anaïs Legand, kutoka timu ya WHO inayoshughulika na vimelea hatari, amesema makadirio hayo mapya ya kiwango cha vifo yanatokana na visa vilivyothibitishwa.
Pia amesema kuwa mgonjwa mmoja amepona Ebola na kuruhusiwa kutoka kituo cha afya nchini DRC mnamo Mei 27 baada ya vipimo viwili kuonyesha hana virusi, likiwa ndilo tukio la kwanza la kupona kuthibitishwa tangu kuanza kwa mripuko huu.
WHO imerekodi vifo 10 vilivyothibitishwa na vifo 223 vinavyoshukiwa kusababishwa na Ebola nchini DRC tangu mripuko huo utangazwe Mei 15, miongoni mwa zaidi ya visa 1,000 vilivyothibitishwa na vinavyoshukiwa.
Tedros Adhanom Ghebreyesus, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, aliwasili Kinshasa siku ya Alhamisi. Amezuru kitovu cha mripuko huo katika mkoa wa Ituri, ulioko kaskazini-mashariki mwa nchi hiyo, siku ya Ijumaa.
Dkt. Tedros amewaambia waandishi wa habari kuwa, ugonjwa huo unaweza kusitishwa na akiongeza kuwa WHO haiungi mkono zuio la kusafiri kwa sababu “haitasaidia sana.”
Katika ujumbe wake kwa raia wa Kongo, amesema: “Pamoja, tutauangamiza mripuko huu,” akiahidi kufanya kila kitu kilicho chini ya uwezo wake kusaidia.
Huu ni mripuko wa 17 wa Ebola kurekodiwa katika nchi hiyo pana ya Afrika ya Kati yenye idadi ya watu zaidi ya milioni 100. Ugonjwa huo uligunduliwa kwa mara ya kwanza nchini humo mwaka 1976.
Mripuko huo umejikita katika eneo lenye utajiri wa madini ambalo linakumbwa na uasi. Mkurugenzi Mkuu wa WHO amesema: “Migogoro na watu kulazimika kuyahama makazi yao hufanya kila kitu kuwa kigumu zaidi.” Ametoa wito wa moja kwa moja kwa pande zote zinazopigana katika eneo hilo kutangaza usitishaji vita wakati huu ili kurahisiha shughuli za kuokoa maisha ya wagonjwa.
Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la wakimbizi, zaidi ya watu 245,000 wamekimbia mashariki mwa DRC kuelekea nchi jirani tangu Januari 2025. Kuna makundi kadhaa ya waasi katika eneo hilo ambapo kundi linalotenda jinai zaidi ni lile la M23, linaloungwa mkono na Rwanda, na linadhibiti maeneo makubwa ya mikoa ya Kivu Kaskazini na Kusini, upande wa kusini mwa Ituri.
Dalili za mapema za Ebola ni pamoja na homa, uchovu, maumivu ya misuli, maumivu ya kichwa na koo kuwasha. Hizi zinaweza kuendelea na kuwa kutapika, kuharisha, maumivu ya tumbo, vipele na kudhoofika kwa utendaji kazi wa figo na ini.
Ugonjwa huo huenea kupitia mgusano wa moja kwa moja na damu au majimaji ya mwili ya mtu aliyeambukizwa au mtu aliyefariki kutokana na Ebola.