
Harakati ya Hamas imelaani vikwazo vya Umoja wa Ulaya, ikiikosoa kambi hiyo kwa “kufumbia macho” ukiukaji wa sheria za kimataifa unaofanywa na Israel huku ikiyalenga makundi na viongozi wa mapambano ya ukombozi wa Palestina.
“Tunalaani uamuzi wa Baraza la Umoja wa Ulaya wa kupanua vikwazo dhidi ya Hamas na harakati za Kiislamu za Jihad na kuwajumuisha baadhi ya viongozi wao wa kisiasa kwenye orodha yake,” imesema taarifa ya Hamas iiliyotolewa jana Jumamosi.
Hamas imeongeza kuwa vikwazo hivyo si vya haki na vina upendeleo kwa simulizi ya utawala vamizi, na vinaakisi sera ya unafiki na undumakuwili katika kushughulikia suala la Palestina.
“Uamuzi huu unakuja huku Israel ikiendelea kufanya uhalifu wa mauaji ya kimbari, kuwatesa raia kwa njaa, kulazimisha watu kuhama makazi yao na kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, huku Umoja wa Ulaya ukipuuza ukiukwaji huu wa sheria za kimataifa na kuchagua kuwaadhibu viongozi wa kisiasa wanaotetea haki halali za watu wao,” imesema taarifa hiyo.
Hamas imesema: “Jaribio la kuyadhihirisha makundi ya mapambano ya ukombozi wa Palestina kama watenda jinai halitabadilisha ukweli kwamba watu wetu wako chini ya uvamizi, mapambano yao ni haki halali inayotambuliwa na sheria zote na kanuni za kibinadamu.”
Hamas imeeleza kuwa kuwalenga viongozi wa kisiasa kunathibitisha kwamba vikwazo hivi vinakuja kuitikia wito wa utawala vamizi na havitegemei viwango vya haki.
Harakati hiyo imeitaka EU kupitia tena sera zake zenye upendeleo, kuacha kutoa kinga ya kisiasa kwa Israel, na kufanya kazi ya kuwawajibisha viongozi wake badala ya kuwakatia hukumu waathiriwa.
Siku ya Ijumaa, Umoja wa Ulaya (EU) ulisema kwamba umewaweka wanachama kumi wa chombo cha juu cha uongozi wa kisiasa cha Hamas katika oarodha ya watu waliopigwa marufuku ya kusafiri na kuzuiliwa mali zao, na hivyo kuzuia upatikanaji wa fedha au rasilimali za kiuchumi kwa wale waliotajwa, ama moja kwa moja au kwa njia isiyo ya moja kwa moja.
Itakumbukwa kuwa, tangu Oktoba 7, 2023, Israel imeua zaidi ya Wapalestina 72,000 na kuwajeruhi wengine wasiopungua 172,000, wengi wao wakiwa wanawake na watoto.