JKT Queens imeanza mipango ya kufanya maboresho makubwa ya kikosi kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu ya Wanawake Bara baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu hiyo msimu huu wa 2025/26.
Taarifa zinaeleza maboresho hayo yatahusisha kuwaacha baadhi ya wachezaji ambao hawapo kwenye mipango sambamba na kusajili nyota wapya watakaoongeza ushindani katika kikosi.
Mbali na usajili mpya, JKT Queens tayari imeanza kuimarisha kikosi chake kwa kuwapa mikataba mipya baadhi ya wachezaji waliomaliza mikataba yao, akiwemo nyota chipukizi Elizabeth John ambaye ameendelea kuonyesha ubora mkubwa katika kikosi hicho.
Chanzo cha karibu na klabu hiyo kililiambia Mwanaspoti viongozi wanaamini kuna haja ya kufanya mabadiliko kadhaa ili kurejesha makali ya timu hiyo katika mbio za ubingwa msimu ujao.
“Uongozi unaona kuna maeneo yanahitaji kuongezewa nguvu. Ndiyo maana kuna tathmini ya kikosi inafanyika ili kujua nani ataendelea na nani ataachwa. Lengo ni kuwa na timu yenye ushindani mkubwa zaidi,” kilisema chanzo hicho.
Katika hatua nyingine, JKT Queens pia imeanza mchakato wa kutafuta kocha mkuu mpya atakayekiongoza kikosi hicho msimu ujao. Inaelezwa tayari wameanza mazungumzo na baadhi ya makocha wanaofanya vizuri kwenye soka la wanawake nchini.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kuingia kwenye rada za JKT Queens ni kocha mkuu wa B19 FC, Twaha Beimbaya.
JKT Queens ni miongoni mwa timu zenye historia nzuri katika soka la wanawake nchini, hivyo maboresho yanayopangwa yanaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa kurejesha timu hiyo kwenye ushindani mkubwa wa kutwaa mataji katika msimu ujao.