Dar es Salaam. Ikiwa imepita miezi saba tangu kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025, mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), ClaytonRevocatus Chipando maarufu Baba Levo amesema sasa anaheshimika kutokana na kazi anayoifanya jimboni kwake.

Baba Levo anasema hayo kwenye mahojiano maalumu na Mwananchi, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam alipozungumzia masuala mbalimbali kuhusu ubunge wake na uzoefu alioupata ndani ya muda huo mfupi.

Hii ni mara ya kwanza kwa Baba Levo kuwa mbunge baada ya kuwashinda wagombea wa upinzani akiwamo aliyewahi mbunge wa jimbo hilo kupitia ACT -Wazalendo, Zitto Kabwe, akiwa ni msanii wa muziki na mhamasishaji.

Mbunge huyo ambaye hujitambulisha kama ‘chawa’  anasema aliamini anapendwa na wananchi wa Kigoma Mjini tangu alipokuwa diwani kupitia ACT- Wazalendo, lakini walikuwa wakimheshimu Zitto, sasa anabadili upepo, wananchi wameanza kumheshimu.

“Mimi niliamini ninapendwa, kwa hiyo ninachokitengeneza sasa hivi ni heshima ili watu wawe wanampenda mtu na kumheshimu. Watu wengi walikuwa wananipenda lakini kuniheshimu, hapana, wanaona huyu chawa tu, walikuwa hawanipi heshima kama waliyokuwa wanampa Zitto.

Mbunge wa Kiboma Mjini, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam. Picha na Michael Matemanga.

“This time (wakati huu) baada ya kazi zinazotokea, mambo yamegeuka, sasa heshima inaanza kuingia kwamba huyu ndiye mtoto ambaye tunapaswa tumpe nguvu zetu zote, huyu ndiyo anakwenda kutuvusha,” anasema Baba Levo.

Alivyobadili mtazamo wa watu

Kutokana na alivyoanza kuutumikia wadhifa huo, Baba Levo anasema wengi waliokuwa wakimbeza wakiamini hawezi kufanya chochote, mitazamo yao imebadilika na kuona ana uwezo wa kuwasemea wananchi wake.

“Ingawa ni wachache, bado wanasubiri wapi nitateleza au kuanguka ili wanicheke lakini asilimia kubwa wananifuata kwa njia ya mitandao ya kijamii (DM), Baba Levo kama nilikusema vibaya nisamehe,” anasema.

Pia, anasema watu hao wanampongeza kwa anayoyafanya wakidai anawafurahisha na kuonesha mfano kwa kuwatumikia wananchi wa jimbo lake.

“Ambao hawakunipia kura wanajutia kwa kuninyima kura na wapo wanaotamani uchaguzi urudiwe ili watimize takwa hilo ili nao wawe sehemu ya furaha,” anasema mbunge huyo.

Anasema nyakati zote huwa anafurahi kuona watu wakimsifia na kuna vitu huwa anavifanya kwa sifa tu, ingawa huwa wakati mwingine vinamtia hasara.

“Mimi Muha sifa ndiyo zangu waswahili wanasema Muha mpe sifa mnyime hela,” anasema.

Atumia Sh470 milioni

Baba Levo anasema tangu achaguliwe katika nafasi hiyo, ametumia Sh470 milioni kutoka mfukoni mwake kuwasaidia wananchi wake.

Anasema fedha hizo zimetokana na fedha zake, mikopo, msaada kutoka kwa wadau wake pamoja na kuuza vitu vyake ili kutatua shida za wananchi wake wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii.

“Tangu nimekuwa mbunge hadi sasa nimetoa kwenye mfuko wangu, kukopa na kuuza vitu vyangu, zaidi ya Sh470 milioni na ni kipindi cha miezi saba pekee, kwa sababu kila kitu anachokwambia mwananchi anaamini wewe unaweza kumkwamua,” anasema. 

Anasema utamaduni uliojengeka kwa wananchi wengi kuamini wakikupa ubunge wamekupa utajiri, wanaamini hata kama walikuchagua maskini lakini wakikupa wadhifa huo lazima utawavusha kwenye baadhi ya vitu vyao.

“Kuna wengine wanadiriki hadi kukukaripia, mfano leo nilipokea simu ya mtu mmoja akajitambulisha na kunisalimia kisha akaniomba nimsaidie ana miaka mingi hajaoa, kwa hiyo nisaidie mahari aweze kuoa…nilimjibu ndoa ni kitu ambacho wewe unakipanga ni tofauti na msiba, nikikuchangia mahari kweli ndoa yako utaiheshimu kweli,” anasema.

Anasema baada ya kumjibu hivyo, mtu huyo ambaye hakutaja jina, alianza kumkaripia akimtaka kama hana fedha ni muhimu aseme ukweli badala ya kuwa na maneno mengi huku akisisitiza mambo hayo amekuwa akikutana nayo mara kwa mara.

“Kazi ya ubunge mwanzoni nilivyokuwa naifikiria ni tofauti na nilivyoipata, mwanzo nilikuwa nawaza sehemu ya kupata utajiri, nikiwa mbunge naweza kupata fedha na kutengeneza fedha nyingi,” anasema.

Anasema alikuwa anawaza akishika wadhifa huo anaweza kutengeneza fedha nyingi lakini baada ya kupata, amebaini kama kweli anataka kuutumikia wadhifa huo kwa kuwatumikia wananchi hadi anamaliza muda wake lazima apate hasara.

“Kama kweli unataka kuwatumikia wananchi asilimia 100, basi hadi unamaliza ubunge wako lazima uwe umepata hasara kwa namna moja ama nyingine, kwa hiyo si sehemu ya kutengeneza fedha,” anasema.

Alivyotumia fedha hizo

Baba Levo anasema sehemu ya fedha hizo, anasomesha wanafunzi 76 wa vyuo vikuu kutoka katika vyuo tofauti na amewalipia ada lakini bado kuna baadhi ya wazazi wanampigia wakisema, watoto wao hawana fedha ya kula.

“Ni changamoto ambayo nakutana nayo, nimekuwa nikiangalia namna ya kuzitatua au kuziepuka,” anasema.

Anasema ametoa fedha zake zingine zaidi ya Sh20 milioni kwa ajili ya harambee ya kuchangisha madawati zaidi ya 8,000 na amekuwa akiwachangisha wadau wake wakiwamo wasanii Nandy, Bilinas, Diamond pamoja na taasisi zingine za kifedha.

“Mwezi ujao naenda kugawa madawati 800 kati ya 8,000 yanayohitajika Kigoma Mjini ili wanafunzi wakae sehemu nzuri, kazi zingine zitafanywa na Serikali zinazobakia nitazifanya kwa kushirikisha wadau,” anasema.

Anasema amegawa pikipiki kwa vijana kwa sababu wanafanya shughuli ya bodaboda lengo la kufanya hivyo ni kile alichodai vijana wengi wamekuwa wakiingia mikataba ya kupata vyombo hivyo, kwa siku kuwasilisha Sh10,000 kwa mwaka mmoja na miezi sita.

“Niliwaza kama nikisema nimgawie mmoja mmoja, wengi hawatapata na nitakosa mashabiki, hivyo nimetenga vijiwe 250 vya kuvipatia pikipiki moja moja, na kwa siku wanipatie Sh3,000 kwa siku ndani ya mwaka mmoja pekee,” anasema.

Anasema wakifanya marejesho hayo kwa mwaka mmoja baada ya hapo pikipiki inakuwa mali yao kwani yeye huwa ananunua kwa Sh3.2 milioni lakini wao humrudishia Sh1.9 milioni kinachobakia ni msaada kwao.

“Ingawa baadhi ya watu walitaka kuzinunua hizo pikipiki baada ya kupiga mahesabu, nilipobaini hilo nimeweka kinga hata kama watamaliza kulipa fedha leo, bado pikipiki itakuwa chini ya umiliki wangu hadi mwaka uishe,” anasema.

Anasema mfumo huo wa kinga alianzisha kwa lengo la kuwaepuka walanguzi ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya vijana kutumia udhaifu wao wa kukosa fedha ili wanunue pikipiki hizo na kiasi kinachobakia wagawane.

“Kati ya vijiwe 250 hadi sasa vijiwe 25 tayari vimepata pikipiki na naendelea na jitihada kufikisha idadi inayohitajika, hayo yote nafanya ikiwa ni jitihada zangu binafsi,” anasema Baba Levo.

Pia, anasema Kigoma Mjini ukitokea msiba, amepiga marufuku kumzika mtu kwa sanda ya kukopa kwa kuwa, amepata mdau ambaye anagawa sanda kila kata.

“Mtu akifariki dunia hakuna kununua sanda tena, kinachofanyika ukifiwa unaenda ofisi za kata kuandikisha jina lako, unapewa sanda kwenda kuhifadhi mwili wa marehemu…sihitaji kusikia mtu anadaiwa sanda ya mkopo,” anasema.

Sambamba na hilo, anasema amegawa madaftari zaidi ya 100,000 kwa ajili ya wanafunzi ambao hawana uwezo ili wahudhurie shule bila kikwazo chochote.

“Vyote hivi vinafanyika kama juhudi zangu binafsi, harambee ya madawati mpango wangu ni kufuta wanafunzi kukaa chini,” anasema.

Kuhusu hela za mfuko wa jimbo, anasema amepewa Sh68 milioni na zote amezielekeza kujenga soko la Kwanoti; na hazitoshi, ili likamilike zinahitajika Sh250 milioni lakini ameona ziende huko kwa kuwa alitoa ahadi wakati wa kampeni.

“Nataka soko hili la Kwanoti lijengwe ili liwasaidie kina mama wanaofanya biashara zao chini, wafanye shughuli zao kwenye meza nzuri na kivuli ili mvua ikinyesha isije ikawaharibia biashara zao,” anasema.

Ubunge wa kupewa

Alipoulizwa kuhusu maoni ya baadhi ya watu kwamba wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) hawakuchaguliwa bali walipewa ubunge, Baba Levo anakanusha na kusema hayo ni maoni ya wapinzani ambao hawakushiriki uchaguzi na wengine walishiriki wakashindwa.

“Kiuhalisi hata mimi ningekuwa wao ningesema hivyohivyo, binafsi siwezi kuwalaumu, ningekuwa upinzani na nimejitoa kwenye uchaguzi ningesema hayohayo au nimeshiriki nimepigwa ningesema hivyo hivyo,” anasema.

Anasisitiza kuwa, anaamini wanaolalamika wanataka walichokikosa na hali hiyo haiwezi kumuondoa kwenye mstari wa kuendelea kupigania masilahi ya wananchi wake wa Kigoma.

“Naamini nitathibitisha ubora na utendaji kazi wangu kulingana na kazi nitakazozifanya ndani ya muda wangu Kigoma Mjini, ndiyo yatanipa heshima kubwa na nikigombea tena niweze kutumia mifano kwa kile nilichowafanyia,” anasema.

Itaendelea kesho…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *