Moshi. Simanzi na hasira vimetawala katika Mtaa wa Matindigani, Kata ya Pasua wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro baada ya mtoto mwenye umri wa miaka sita, Idrisa Ramadhani, aliyekuwa akitafutwa tangu jioni ya jana Jumamosi, Mei 30, 2026 kukutwa amefariki dunia ndani ya bwawa la kufugia samaki la mtu binafsi.

Tukio hilo lilitokea leo Jumapili Mei 31, 2026, limezua simanzi na hasira kwa wananchi wa eneo hilo wamedai bwawa hilo si salama kutokana na kutokuwa na uzio imara unaoweza kuzuia watoto kufika karibu na maji.

Akizungumza katika eneo la tukio, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro, Philbert Beda amesema walipokea taarifa za mtoto huyo kudondoka kwenye bwawa hilo saa sita mchana na kufika eneo la tukio kwa ajili ya uokoaji.

“Kwa taarifa za awali, mtoto alipotea tangu jana mchana na leo ndipo amepatikana akiwa amefariki ndani ya bwawa hilo. Chanzo halisi cha tukio bado kinaendelea kuchunguzwa,” amesema Beda.

Baba wa mtoto huyo, Khatibu Ramadhani amesema mara ya mwisho kumuona mwanaye ilikuwa jana jioni alipokuwa akielekea kuswali.

“Usiku mzima tulikuwa tunamtafuta bila mafanikio. Leo saa tano ndipo majirani walikuja kuniita na kuniambia mtoto amepatikana kwenye bwawa hili,” amesema baba huyo.

Bwawa la kufugia samaki alikokutwa mtoto mwenye umri wa miaka sita, Idrisa Khatibu Ramadhani, akiwa amefariki dunia katika Mtaa wa Matindigani, Kata ya Pasua wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Yese Tunuka.

Amesema familia ilitoa taarifa za kupotea kwa mtoto huyo kwa viongozi wa mtaa, miskitini na maeneo mbalimbali ya jirani ili kusaidia juhudi za kumtafuta.

Akizungumza kuhusu tukio hilo, Imamu wa Msikiti wa Al Nurul Falah, Sheikh Kheri Jumaanne amesema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilimfikia saa 2:00 usiku baada ya sala ya Isha, ambapo aliombwa kutumia vipaza sauti vya msikiti kutangaza ili wananchi wasaidie jitihada za kumtafuta.

Sheikh Jumaanne amesema ni utaratibu wa kawaida kwa msikiti huo kutangaza taarifa mbalimbali za watu waliopotea kupitia vipaza sauti vya msikiti huo, lakini licha ya jitihada hizo mtoto hakupatikana siku hiyo.

Amesema asubuhi ya siku iliyofuata (leo) baba wa mtoto huyo amemweleza bado hajapatikana, hali iliyomlazimu kutangaza tena kabla ya kuendelea na shughuli nyingine za dua.

“Baadaye nilipigiwa simu na jirani pamoja na mmoja wa waumini wa karibu na msikiti wakisema kuna mtoto ametumbukia kwenye maji. Nikampigia mwenyekiti wa eneo hilo simu saa 5:00 asubuhi naye akaja kuangalia, ndipo harakati za kutoa taarifa sehemu mbalimbali zikaanza,” amesema Sheikh Jumaanne.

Balozi wa Mtaa wa Matindigani, Albina Lelo, amesema taarifa za kupotea kwa mtoto huyo zilianza kusambaa tangu usiku wa kuamkia leo na juhudi za kumtafuta zilifanyika katika maeneo mbalimbali ambayo watoto huzoea kucheza.

Amesema mtoto huyo alikuja kugunduliwa leo na watoto waliokuwa wakitoka madrasa baada ya kuona mwili ukiwa ndani ya bwawa hilo. “Watoto ndio waliokuwa wa kwanza kuona kuna mtu ndani ya maji, ndipo watu wazima wakaenda eneo hilo na baadaye tukathibitisha kuwa ni Idrisa aliyekuwa akitafutwa tangu jana,” amesema.

Kutokana na tukio hilo, wananchi wenye hasira walitaka kubomoa uzio wa bwawa hilo wakidai limekuwa hatari kwa wakazi wa eneo hilo, hasa watoto.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo, Emmanuel Msuya, akizungumza kwa uchungu amedai aliwahi kuonya kuhusu hatari ya bwawa hilo baada ya mtoto wake mwenyewe kunusurika kifo kufuatia kutumbukia katika shimo hilo hapo awali.

“Niliwaambia fukieni hili shimo litakuja kuua wakakataa, sasa limeshaua. Mtoto wangu alitumbukia hapa lakini hakuna mtu aliyekuja kunifuata hata kunisaidia hela ya paracetamol,” amesema Msuya huku akionyesha nyumba yake iliyo jirani na eneo hilo.

Msuya ameongeza  tukio hilo linamuumiza moyoni kwani lingeepukika kama ushauri wake wa kufukia shimo hilo ungechukuliwa kwa uzito mapema.

Akizungumza na wananchi hao, Diwani wa Bomambuzi, Juma Raibu, amesema ni kosa kuacha eneo hatarishi kama hilo bila ulinzi wa kutosha katika makazi yenye watu wengi.

“Hili ni eneo la makazi ya watu wengi, hivyo si jambo jema kuacha maeneo kama haya bila kuyafunika au kuyawekea ulinzi. Lazima hatua zichukuliwe ili lisijirudie tena,” amesema Raibu.

Amesema viongozi wa eneo hilo pamoja na vyombo vya dola watahakikisha suluhisho la kudumu linapatikana kuhusu bwawa hilo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kata ya Pasua, Amosi Chibago, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kuacha vyombo vya sheria kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

“Msibomoe eneo hili kwa sasa kwa sababu sheria inafuata mkondo wake. Uchunguzi utafanyika ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Chibago.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *