Dar es Salaam. Dodoma ya leo sio ya jana. Ndiyo maneno unayoweza kuyatumia kuonyesha kasi ya mabadiliko ya jiji hilo, kutoka kuwa makao ya watumishi wa umma na Serikali, hadi kuwa kitovu cha uwekezaji wa majengo ya biashara.

Sio ongezeko la uwekezaji tu, hata kodi za upangishaji wa majengo ya biashara zimepanda maradufu na kuifanya Dodoma kuwa mikoa inayoongoza kwa gharama ya pango la ofisi, kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

BoT kupitia ripoti yake ya Utulivu wa Mfumo wa Fedha ya Desemba 2025, inaonyesha wastani wa kodi ya ofisi jijini Dodoma, umefikia kati ya Sh30,000 hadi Sh35,000 kwa mita ya mraba, kiwango kinacholifanya kuwa soko ghali zaidi la ofisi nchini.

Kiwango hicho kimezidi kile kinachotozwa jijini Dar es Salaam, ambacho ni kati ya Sh25,000 na Sh30,000 kwa mita ya mraba, huku Arusha, Mwanza na Mbeya ikiwa na viwango vya chini zaidi vinavyokadiriwa kufikia Sh20,000 hadi Sh25,000 na Sh10,000 kwa mita ya mraba mtawalia.

Ripoti hiyo pia, inaonyesha kiwango cha matumizi ya majengo ya biashara kinaendelea kuongezeka katika miji mikuu ya Tanzania. Dodoma na Mbeya zimefikia asilimia 100 ya matumizi ya nafasi zilizopo.

Kwa upande wa Arusha, imefikia karibu asilimia 95, huku Dar es Salaam ikirekodi kati ya asilimia 80 na 100 kulingana na eneo husika.

“Miradi inayoendelea ya miundombinu ikiwamo barabara, bandari na viwanja vya ndege imeimarisha muunganiko wa maeneo ya biashara na kufanya mali za kibiashara kuwa na mvuto mkubwa zaidi kwa wawekezaji na wafanyabiashara,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kwa wawekezaji, mchanganyiko wa ongezeko la kodi za upangishaji na uhaba wa nafasi za biashara unaifanya Dodoma kuingia katika hatua mpya ya ukuaji wa sekta ya mali isiyohamishika na kwamba mahitaji yanayochochewa na shughuli za Serikali yanazidi kuimarika.

Mshirika Mkuu wa Kampuni ya Hello Africa Consults, Emmanuel Njavike, anasema uhamishaji wa shughuli za Serikali kwenda Dodoma umezalisha kundi jipya la wateja wanaohitaji huduma za kibiashara na ofisi.

Ingawa Dar es Salaam bado ndiyo kitovu kikuu cha biashara nchini, anasema muundo wa mahitaji katika miji mbalimbali unaendelea kubadilika kwa kasi.

“Dar es Salaam bado inaendelea kuwa nyumbani kwa mashirika makubwa ya kimataifa kama Umoja wa Mataifa na Benki ya Dunia pamoja na kampuni nyingi za kimataifa, lakini Dodoma sasa inachukua sehemu kubwa ya mahitaji yanayotokana na shughuli za kiutawala na huduma zinazohusiana na Serikali,” anasema.

Njavike, anaeleza uwekezaji mkubwa katika miundombinu ikiwamo Reli ya Kisasa (SGR), Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba na mtandao wa barabara umeongeza mvuto wa jiji hilo kwa wawekezaji.

Hata hivyo, anasema bado Dodoma haijafikia kiwango cha Dar es Salaam katika upatikanaji wa huduma za kisasa za kibiashara kama majengo ya kifahari ya ofisi, huduma za burudani na miundombinu ya biashara.

“Dodoma bado iko katika hatua ya ukuaji, lakini hali hiyo ndiyo inayoifanya kuwa na fursa kubwa katika uwekezaji wa maduka makubwa, hoteli za hadhi ya juu, nyumba za huduma maalumu kwa wageni na vituo vya mikutano,” anasema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Faammo Real Estate, Fadhil Mkwachu, anasema sekta ya mali isiyohamishika huongozwa na mahitaji ya soko.

Kuhusu ripoti hiyo ya BoT, anasema ongezeko la mahitaji hayo jijini Dodoma, limetokana na kuhamishiwa kwa shughuli za Serikali pamoja na huduma zinazozizunguka.

Anasema watu na biashara hufuata maeneo yenye fursa za kiuchumi.

“Watu huenda mahali penye fursa zaidi za maisha na biashara,” anasema, akisisitiza mkusanyiko wa wizara, watumishi wa umma, makandarasi na watoa huduma umeongeza mvuto wa kiuchumi wa Dodoma.

Anasema hali hiyo imeimarishwa zaidi na utekelezaji wa miradi mikubwa ya miundombinu kama SGR, Uwanja wa Ndege wa Dodoma, Mji wa Serikali Mtumba na upanuzi wa mtandao wa barabara za mzunguko.

Hata hivyo, Mkwachu anaeleza kuwa sekta hiyo inakabiliwa na changamoto ya kimuundo kwani ongezeko la mahitaji haliwezi kuendana haraka na kasi ya ujenzi wa majengo mapya.

“Mahitaji yanaweza kuongezeka kwa haraka, lakini ujenzi wa majengo mapya huchukua miaka kadhaa kukamilika,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, Dodoma inashuhudia uhaba wa nafasi za ofisi na biashara unaosababisha ushindani mkubwa wa upangishaji na kupandisha zaidi viwango vya kodi.

Msimamizi wa mali, Magreth Ngombale, anasema hali ya sasa ya soko la mali isiyohamishika jijini Dodoma inachochewa na kiwango kikubwa cha matumizi ya majengo yaliyopo na uhaba wa miradi mipya ya kibiashara.

Anasema maendeleo ya majengo huchukua muda mrefu ilhali mahitaji katika mji mkuu wa kiutawala yanaweza kuongezeka ghafla kutokana na uamuzi wa kisera au uhamishaji wa taasisi za Serikali.

Kutokana na tofauti ya majukumu ya miji hiyo miwili mikubwa nchini, Dar es Salaam imeendelea kuwa kitovu cha biashara na fedha, wakati Dodoma ikibeba jukumu la kuwa makao makuu ya utawala wa Serikali.

Ngombale, anasema hali hiyo imezalisha aina tofauti ya mahitaji ya wateja. Dodoma, watumiaji wengi wa huduma za majengo ya biashara ni watu na taasisi zinazoshiriki shughuli zinazohusiana na Serikali kama mikutano, semina, warsha na mafunzo.

Kutokana na mazingira hayo, kuna mahitaji makubwa ya ofisi zinazotolewa kwa muda mfupi, kumbi za mikutano na huduma za malazi zinazoweza kubadilika kulingana na mahitaji ya taasisi mbalimbali.

Anasema soko la mali isiyohamishika la Dodoma kwa sasa linaongozwa na uhaba wa nafasi za biashara, ongezeko la mapato ya upangishaji na mahitaji endelevu yanayotokana na shughuli za Serikali.

Tofauti na Dar es Salaam, ambayo ni soko lililokomaa na lenye ushindani mkubwa, anasema Dodoma bado ina maeneo mengi ambayo hayajaendelezwa kikamilifu na hivyo kutoa nafasi kwa wawekezaji wapya.

Anaeleza fursa kubwa zaidi kwa sasa zinapatikana katika uwekezaji wa nyumba za wageni zenye huduma maalumu, hoteli za mikutano, vituo vya biashara na ofisi zinazoweza kukidhi mahitaji ya taasisi na mashirika yanayofanya kazi katika makao makuu ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *