
Dar es Salaam. Tanzania imepiga hatua ya kuchukua teknolojia zilizokwisha muda wa umiliki katika nchi nyingine ili kuja kusaidia jamii katika maeneo ya uzalishaji ili kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kiujumla.
Hatua hiyo inafuatia ushirikiano na Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO), ambapo utekelezaji umeanza kupitia mradi wa kwanza wa teknolojia ya kilimo na ufugaji mkoani Njombe.
Akizungumza kwenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika Dar es Salaam leo Jumatatu, Juni 1, 2026, Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk Amos Nungu amesema wanaangalia kwenye kanzi data ya WIPO, teknolojia sahihi kwa ajili ya mazingira ya Tanzania.
“Tunaangalia teknolojia zilizomaliza muda wa umiliki tayari kuja kutumika hapa nchini. Kupitia hatua hii tunataka kuwasaidia vijana wetu kuwa na bunifu na sampuli kifani,” amesema.
Dk Nungu amesema tayari wameshachagua teknolojia kwenye kilimo na ufugaji itakayotumia mabaki ya chakula kwa ajili ya kuzalisha ili kupunguza mzigo wa kuagiza vyakula vya wanyama.
“Tunachukua teknolojia tunapeleka, Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST), wanachukua taarifa wanatengeneza sampuli kifani kisha linaandikwa andiko halafu wawekezaji na wadau wanakuja kufanya uzalishaji mkubwa,” amesema.
Akizungumzia mradi huo wa Njombe, Mkuu wa Kitengo cha Uratibu wa Nchi Zinazoendelea Kidogo, Nchi Zisizozungukwa na Bahari na Nchi Ndogo za Visiwani katika shirika la WIPO, Purevdorj Vaanchig amesema uzinduzi wake una lengo la kujenga uwezo, hasa wa kiteknolojia wa vyuo vikuu vya ndani na taasisi za utafiti.
“Mradi unalenga namna ya kutumia mfumo wa kimataifa ili kupata uelewa wa kina katika nyanja za kiteknolojia. Pia jinsi gani ya kutafuta na kutambua suluhu zinazofaa za kiteknolojia, na kwa safari hii, sekta ya kipaumbele iliyoainishwa na nchi mnufaika ambayo ni Tanzania yenyewe ni teknolojia ya usindikaji wa chakula cha mifugo,” amesema.
Amesema lengo kuu la hili ni kuja kusaidia jamii za ndani na kuboresha maisha ya wananchi. Sehemu ya pili ya mradi ni kujenga ujuzi ndani ya vyuo vikuu na kuchangia katika mfumo wa ikolojia wa ubunifu wa ndani.
Awali, Mkurugenzi wa Miliki Ubunifu kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) Loy Mhando, amesema WIPO walikubali kuipa Tanzania teknolojia sahihi kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya jamii.
“Tukakubaliana tuangalie bunifu zilizopo kwenye kanzi data ndio maana tumekuja na mradi huu wa miezi 12 kuwanufaisha wakulima na wafugaji. Zitatafutwa teknolojia za kutumia mabaki ya chakula ili kupunguza kuagiza vyakula vya mifugo kutoka nje ya nchi,” amesema.
Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu kutoka Taasisi ya Nelson Mandela,Profesa Thomas Kivevele, amesema wakiwa kama wadau wa mradi huo watakuwa wanachakata taarifa zinazotoka kwenye chanzo ili kuja na ubunifu utakaotatua changamoto ya chakula cha mifugo.
“Tunatumia taarifa hizo tunakuja na sampuli kifani ili kwenda kwenye uzalishaji mkubwa. Lengo ni kuja na teknolojia nyingi zitakazosaidia kukuza uchumi,” amesema.