Dar es Salaam. Tofauti na wanamuziki wengi, Aslay alianza kuvuma akiwa bado mdogo kabisa, lakini nyimbo zake kwa asilimia kubwa zilibeba hata maudhui yanayowagusa hadi watu wazima.
Akiwa tayari ameachia albamu mbili, Aslay ameendelea kuonyesha ukubwa wa kipaji chake katika uimbaji na utunzi wa mashairi ambayo wamewagusa wengi. Fahamu zaidi.
1. Aslay ni miongoni mwa wasanii wanne kutoka kwenye Bongo Fleva ambao wanafanya kazi na RockStar Africa pamoja na Sony Music Africa. Wengine ni Ommy Dimpoz, Young Lunya na Abigail Chams.
2. Albamu mpya na ya pili kutoka kwa Aslay, My Way (2026), imesimamiwa na kampuni hizo mbili ikiwa na nyimbo 14 huku akiwashirikisha wasanii wawili ambao ni Chino Kidd na Kontawa.
3. Kabla ya Aslay kuanza kufanya muziki peke yake (solo), aliunda kundi la Yamoto Band na wenzake watatu ambao ni Beka Flavour, Enock Bella na Mbosso. Yamoto Band walifanya kazi pamoja kati ya mwaka 2012 hadi 2017 walipotengana na kila mmoja kuanza kufanya muziki peke yake.
4. Kundi la Yamoto Band lilipata umaarufu kwa mara ya kwa baada ya kuachia wimbo wao, Ya Moto (2013) uliotengenezwa Vibe Records na Shirko. Huo ulikuwa wimbo wa kwanza kurekodiwa na vifaa vipya vya muziki vya Mkubwa na Wanawe na baada ya hapo walivuma kupitia nyimbo zao nyingine kama Niseme (2014), Nitakupwelepweta (2015), Cheza kwa Madoiko (2015), Mama (2016) na kadhalika.
5. Yamoto Band walishida Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2015 kama Kundi Bora la Mwaka Bongo Fleva wakiwabwaga Weusi, B.O.B, Navy Kenzo na Makomando. Na Yamoto ndio wasanii wa mwisho kushinda kipengele hicho maana hakipo tena ndani ya tuzo za TMA.
6. Ndani ya kipindi kifupi nyimbo za Yamoto Band zilikuwa maarufu na kujizolea mashabiki wengi huku akifanya shoo za kimataifa katika nchi kama Marekani, Sweden, Finland, Italia, Norway, Ujerumani, Uswisi, Uingereza na kadhalika.
7. Tangu ameachana na Yamoto Band, Aslay hajashinda tuzo tena ya TMA licha ya kufanya vizuri na hadi sasa kati ya wasanii wanne waliounda kundi hilo ni Mbosso pekee aliyefanikiwa kushinda tuzo hizo baada ya kila mmoja kushika njia yake.
8. Aslay alianza muziki akiwa na umri wa miaka 14, hivyo ametoa burudani ya aina yake kwa mashabiki kwa kipindi cha miaka zaidi ya 15 hadi sasa na ana umri wa miaka 31.
9. Wimbo wa kwanza wa Aslay kurekodi unaitwa ‘Niwe Nawe’ (2011) ambao alikuja kuurudia na kumshirikisha Mheshimiwa Temba, lakini ngoma iliyomtoa ni ‘Nakusemea’ (2012) ambayo ilibeba jina la albamu yake ya kwanza.
10. Baada ya kutoa albamu yake hiyo ya kwanza, ndipo likaanzishwa kundi la Yamoto Band chini ya menejimenti ya Mkubwa na Wanawe ambayo imewatoa wasanii wengi akiwemo Kayumba, mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2015.