Dar es Salaam. Zaidi ya nusu ya Watanzania wanashiriki michezo ya kubahatisha yaani kamari, idadi ambayo wataalamu wa afya ya akili, wanasema inaashiria hatari itakayozalisha bomu litakalokuwa mzigo kwa Taifa.

Idadi ya wanaoshiriki michezo hiyo nchini inatajwa kufikia takriban watu milioni 39, kati yao vijana wenye umri wa chini ya miaka 35 ni asilimia 75, kama ilivyowahi kuelezwa na Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais),  Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka.

Makadirio hayo ya idadi ya wacheza kamari nchini, ni sawa na asilimia 61.3 ya Watanzania wote milioni 63.6, kwa mujibu wa makadirio ya kitaifa yanayoakisi ukuaji wa idadi ya watu kufuatia matokeo rasmi ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

Takwimu za idadi ya wacheza kamari, zilitolewa na Nanauka Mei 16, 2026 alipozungumza katika Kongamano la Wanafunzi wa Vyuo na Vyuo Vikuu, jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, alisema: “Nilikuwa nasoma takwimu imenishangaza sana, karibu milioni 39 ya wananchi wa nchi hii wapo kwenye kamari. Asilimia kubwa ni vijana chini ya miaka 35 ikiwa ni sawa na asilimia 75.”

Hata hivyo, kamari inayochezwa zaidi ya vijana, pia wamo watu wazima, wafanyabiashara, watumishi wa umma, sekta binafsi, maskini, matajiri na hata wanafunzi wa ngazi mbalimbali za elimu.

Idadi hiyo ya wacheza kamari, wataalamu wa magonjwa ya akili na saikolojia wanasema inaweza kuzalisha hatari hasa itakapotokea wachezaji wakapata uraibu.

Kwa mujibu wa Kanuni za Michezo ya Kubahatisha Mtandaoni za mwaka 2022, watoa huduma wanatakiwa kuchukua hatua za kuwalinda wachezaji dhidi ya uraibu.

Kanuni ya 47(1) inazitaka kampuni kuweka notisi za onyo kuhusu hatari ya uraibu kwenye majukwaa yao. Aidha, Kanuni ya 47(2) inazitaka kampuni hizo kuwa na watumishi waliopata mafunzo ya kufuatilia na kutoa ushauri kuhusu matatizo ya kamari.

Kwanini wanaingia kwenye kamari?

Akizungumza na Mwananchi Ijumaa Mei 29, 2026, Mtaalamu wa magonjwa ya akili, Dk Raymond Mgeni amesema vijana wengi huanza kamari kwa kufuata wenzao waliopata ushindi, hali inayowafanya waamini ni njia rahisi ya kupata kipato.

“Wengine huingia kwa lengo la kupata kipato, wanahisi kupitia kubashiri wataweza kupata fedha haraka, huanza kwa majaribio na baadaye huingia kwenye uraibu,” amesema.

Amesema kuwa, uraibu mmoja unaweza kusababisha uraibu mwingine, huku mazungumzo na simulizi za watu waliowahi kushinda zikichochea zaidi tabia hiyo.

Dk Mgeni amesema pia, udadisi huwachochea vijana kuamini watafanikiwa kupitia kamari, jambo linalowasukuma kuanza kucheza.

Amesema matokeo ya uraibu huo ni pamoja na msongo wa mawazo, kupoteza ajira au kushuka kwa ufanisi kazini.

“Baadhi huingia kwenye changamoto za kifedha, madeni kutokana na kutumia fedha nyingi kwenye kamari, na hata mahusiano ya kifamilia huathirika,” amesema.

Ameonya katika hatua za juu za uraibu, baadhi ya watu huweza kupata msongo mkali wa mawazo na hata kujiua.

Ameshauri kuimarishwa kwa elimu kwa umma kuhusu madhara ya kamari na njia za kujikinga na uraibu huo.

Mtaalamu wa Saikolojia, Mariam Jimka amesema uwepo wa watu wengi wanaocheza kamari ni njia nyepesi ya kupata waraibu wengi.

“Ukiwa na kundi kubwa la watu wanaocheza kamari ni rahisi kuwa na waraibu wengi, kwa hiyo ni muhimu kuhakikisha tunatoa elimu ya kutosha kwa vijana kuhusu athari za michezo hii,” amesema.

Athari kisaikolojia

Mtaalamu wa saikolojia, Ramadhan Masenga amesema uraibu wa kamari husababishwa pia na tabia ya binadamu kupenda njia za haraka za kupata mafanikio.

Amesema baadhi ya vijana huacha kazi au shughuli rasmi kwa kuamini  wanaweza kupata utajiri wa haraka kupitia kamari.

“Binadamu kwa asili hupenda mambo rahisi na yenye matokeo ya haraka. Hii inawafanya waamini kuwa kwa Sh500 tu wanaweza kuwa matajiri kupitia kamari,” amesema.

Masenga amesema hali hiyo huathiri nguvu kazi ya Taifa kwa kuwa, watu hupoteza mwelekeo wa uzalishaji.

Masenga amesema fedha zinazopatikana kwa njia ya kamari mara nyingi hazidumu kwa sababu hupatikana bila mpango wa kiuchumi.

Amesema njia ya kumsaidia mtu aliye kwenye uraibu ni kumuwezesha kuona uhalisia wa maisha na kuondoa imani potofu kuhusu utajiri wa haraka.

“Hakuna mafanikio ya njia ya mkato. Kamari si njia ya utajiri bali ni chanzo cha faida kwa wamiliki wa kampuni hizo,” amesema.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani asilimia 1.2 ya watu wazima duniani wana matatizo yanayotokana na kamari.

WHO pia linaeleza, asilimia 5.5 ya wanawake na asilimia 11.9 ya wanaume duniani wanakabiliwa na changamoto zinazohusiana na kamari.

Athari kwa elimu na vijana

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba amesema kuna baadhi ya vijana wanaotumia fedha za mikopo ya elimu na matumizi ya msingi katika kamari.

Tutuba alitoa kauli hiyo Mei 18, 2026 jijini Dodoma wakati akizindua utekelezaji wa makubaliano kati ya BoT na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB).

Amesema utafiti wa BoT wa mwaka 2023 ulionesha changamoto ya upungufu wa elimu ya fedha kwa vijana, hali inayochangia matumizi mabaya ya fedha.

Ushuhuda muathirika

James Peter, kijana aliyeathirika na kamari, amesema alianza kucheza akiamini ni njia ya kujipatia kipato cha ziada.

Amesema kadri alivyokuwa akiendelea, alizidi kujihusisha zaidi hadi kufikia kucheza kila siku na kubadili aina ya michezo kutoka ya kawaida hadi kasino.

“Nilikuwa naamini nitapata zaidi kila nikicheza,kila nilipopata fedha nilizitumia kucheza tena na kupoteza kila mara,” amesema.

Amesema uraibu huo ulimfanya ashindwe kulipa kodi, kushindwa kuendesha familia na hatimaye mke wake kumuacha.

James amesema baadaye alirudi kwa wazazi wake na kupata msaada wa kifedha na kisaikolojia uliomwezesha kuanza kupona.

Sera na mwelekeo wa Taifa

Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 (toleo la 2024) inatambua uwezeshaji wa vijana kiuchumi kama kipaumbele cha Taifa.

Sera hiyo inalenga kuwawezesha vijana kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuondoa vikwazo kama ukosefu wa mitaji, ardhi na huduma za ushauri.

Vilevile, Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inasisitiza matumizi ya vipaji vya vijana katika kukuza uchumi wa Taifa.

Katika hotuba yake ya Mei 16, 2026 Nanauka amesema changamoto inayowakabili vijana si ukosefu wa fedha, akibainisha ndani ya mwaka mmoja Serikali imewakopesha Sh52 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi.

Amesema licha ya fedha hizo kutolewa, matokeo yake hayaonekani kwa kiwango kinachotarajiwa kwa sababu hazidumu kwa walengwa wengi.

Kutokana na hali hiyo, amesema Serikali imekuja na mkakati wa kuwapeleka vijana kwenye mafunzo kwanza kabla ya kuwapatia mikopo hiyo.

“Kila kijana atakayepatiwa fedha atalazimika kupitia mafunzo maalumu ili apate maarifa ya namna ya kutumia fedha hizo kwa tija na kukuza shughuli zake,” amesema.

Nanauka ametaja fursa mbalimbali ambazo Serikali imeziandaa kwa ajili ya kuwawezesha vijana kupitia kupitia sekta ya ajira, kazi na mahusiano ya kazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *