Lindi/Mtwara. Licha ya Serikali kujinasibu kuendeleza vituo vya ukuzaji viumbe maji katika matamko yanayojirudia miaka kadhaa, uhalisia wa utekelezaji wake, hususan katika Mradi wa Nyengedi ulioko wilayani Mtama Mkoa wa Lindi, hauakisi hayo.
Akiwasilisha bungeni mpango wa mapato na makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa mwaka 2021/2022, aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Mashimba Ndaki, alieleza Serikali ilikuwa imeanza ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vituo vya ukuzaji viumbe maji kikiwamo cha Nyengedi.
“Wizara imeendelea kufanya ukarabati, upanuzi na ujenzi wa vituo vya kuendeleza ukuzaji viumbe maji ili kupanua wigo wa utoaji huduma za ugani na uzalishaji wa vifaranga vya samaki ambapo vituo vya Kingolwira, Mwamapuli, Nyengedi na Ruhila vimeanza kufanyiwa ukarabati na upanuzi kwa gharama ya Sh802.3 milioni,” alinukuliwa Ndaki.
Mwaka wa Fedha 2024/2025, aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, aliendelea kusisitiza dhamira ya Serikali kuimarisha vituo hivyo.
“Katika mwaka 2024/2025, wizara itaendelea kuimarisha utoaji wa huduma za ugani na uzalishaji wa vifaranga kwa kusimamia na kuendesha vituo vitano vya ukuzaji viumbe maji ambavyo ni Ruhila Ruvuma, Kingolwira- Morogoro, Mwamapuli -Tabora, Machui- Tanga na Nyengedi- Lindi ili viweze kuzalisha vifaranga milioni 3,” alisema Ulega.
Mradi wa Nyengedi ulioko wilayani Mtama Mkoa wa Lindi.
Hata hivyo, zaidi ya miaka mitano baadaye tangu Waziri Ndaki alipotoa ahadi hiyo, picha halisi ya Nyengedi inaonesha tofauti kubwa kati ya mipango na utekelezaji.
Mwananchi ilitembelea eneo ulipo mradi na kushuhudia sehemu kubwa iliyotelekezwa yenye mabwawa mawili chakavu yaliyozungukwa na magugu na majani marefu. Eneo hilo siyo kwamba linatisha bali ni hatari.
Ukifika katika eneo la uwekezaji la Nyengedi, linalokadiriwa kuwa na ukubwa wa zaidi ya ekari 10, jambo la kwanza linalokukaribisha si dalili za maendeleo, bali ni ukimya mzito unaokatizwa na upepo unayumbisha vichaka virefu na majani yaliyotanda kila kona huku ukitaadharishwa na wenyeji juu ya kujihadhari na uwepo wa nyoka wakali wanaopatikana eneo hilo.
Mazingira hayo yanajenga picha ya kusahaulika ni vigumu kuamini kuwa hapa ndipo palipokusudiwa kuwa kitovu cha uwekezaji wa viumbe maji na utotoleshaji wa kisasa uliotajwa mara kadhaa kwenye mipango ya Serikali.
Katikati ya msitu wa vichaka, kwa mbali linaonekana jengo dogo lililochakaa, paa lake likiwa limeharibika na baadhi ya bati, milango na hata madirisha vikiwa tayari ng’olewa na kutokuwapo kwa ulinzi huku kuta zake zikianza kuchoka na kupoteza uhalisia wake wa rangi nyeupe kutokana na kuchorwachora maandishi yasiyofaa na watu wasiojulikana.
Wenyeji wanatahadharisha kuwa eneo hilo siyo salama ikifika nyakati za jioni au kwenda peke yako kwani limegeuka kuwa kichaka cha vitendo vya kihalifu kutokana na uwepo wa vijana walioweka maadili kando na kuamua kujitafutia kipato kwa njia haramu.
Nyumba hiyo, kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo, ilijengwa mahsusi kwa ajili ya kuratibu shughuli za mradi huo. Leo, imesimama kama alama ya ahadi zilizokwama hakuna harakati, hakuna ulinzi, hakuna uhai.
Karibu na jengo hilo, mabwawa mawili yaliyowahi kuchimbwa yamegeuka kuwa sehemu za maji yaliyotuama, yakizungukwa na magugu na mimea pori. Hakuna dalili ya uzalishaji, hakuna ishara ya uwekezaji ni kama muda ulisimama ghafla na kila kitu kikaachwa njiani.
Mradi wa Nyengedi ulioko wilayani Mtama Mkoa wa Lindi.
Wenyeji wanasema hata mlinzi aliyewahi kuwekwa kulinda eneo hilo aliondoka baada ya kukosa malipo kwa muda mrefu, hali iliyofanana na mkandarasi aliyekabidhiwa mradi huo ambaye naye aliondoka bila kuaga.
Leo, Nyengedi si tena eneo la matumaini ya kiuchumi bali ni ushahidi wa wazi wa miradi inayokwama, ikiacha nyuma ndoto zilizoyeyuka na maswali yasiyo na majibu.
Kwa kuangalia hali halisi ya eneo hili, ni vigumu kuamini kulikuwa na mpango madhubuti wa Serikali wa kuwekeza hapa kinachoonekana sasa ni kivuli cha kile kilichowahi kuahidiwa wananchi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini hakuna maendeleo yanayoendana na ahadi wala fedha zilizotajwa, wakati ambao wananchi waliotoa ardhi yao wakiendelea kusubiri fidia bila mafanikio.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na Mwananchi mkoani Lindi, tathmini juu ya wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya kupisha mradi huo walihitaji takribani Sh53 milioni. Hata hivyo, kiasi kilichopatikana kilikuwa Sh21 milioni pekee, hali iliyosababisha utekelezaji wa mradi kuanza kwa kusuasua huku wengine wakiwa wanadai mpaka hii leo.
Kulingana na bajeti iliyosomwa bungeni na Waziri Ndaki ya Sh802 milioni kwa miradi minne ni kiasi hicho kinatafsiriwa kuwa wastani wa zaidi ya Sh200 milioni kwa mradi, fedha ambazo kwa kiwango chake zingetosha kulipa fidia ya Sh53 milioni waliokuwa wakihitaji wananchi hao na fedha nyingine ikatumika kuenedeleza uwekezai huo katika kituo hicho cha Nyengedi.
Kwa mujibu wa Serikali, kwa sasa sekta ya uvuvi nchini inachangia asilimia nane kwenye Pato la Taifa (GDP) huku lengo ikiwa ni kufikia asilimia 10 ifikapo 2030.
Katika jitihada za kuongeza mchango huo, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati ya kuendeleza ukuzaji wa viumbe maji (aquaculture), ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya kimkakati kama vile Nyengedi mkoani Lindi na Ruvula mkoani Mtwara.
Katika jitihada za kuongeza mchango huo, Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi imeweka mikakati ya kuendeleza ukuzaji wa viumbe maji (aquaculture), ikiwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa vituo vya kimkakati kama vile Nyengedi mkoani Lindi na Ruvula Mkoa wa Mtwara.
Vituo hivi vinatajwa kuwa nguzo muhimu katika kufanikisha azma ya Uchumi wa Buluu, unaolenga matumizi endelevu ya rasilimali za maji ili kuchochea ajira, uzalishaji na ustawi wa wananchi.
Mradi wa Nyengedi-Lindi
Kituo cha Nyengedi kilichoko umbali wa kilometa 65 kutoka Lindi mjini kusini mwa Tanzania, ambacho awali kilitarajiwa kuwa nguzo ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki na huduma za ugani katika ukanda wa kusini ikiwamo kuchochea ajira, kimeendelea kukabiliwa na changamoto za utekelezaji zinazotia shaka hatma ya mradi huo.
Katika Kijiji cha Nyengedi, kilichopo Kata ya Nyengedi wilayani Mtama Mkoa wa Lindi kusini mwa Tanzania, simulizi ya uwekezaji uliowahi kuibua matumaini makubwa sasa imegeuka kuwa hadithi ya maumivu, sintofahamu na kusubiri kusiko na mwisho.
Awali, simulizi na taswira nzuri kuhusu mradi wa ujenzi wa kitotoleshi cha samaki pamoja na ukarabati na upanuzi wa Kituo cha Ukuzaji Viumbe Maji cha Nyengedi iliwahi kuonekana kama mkombozi wa kiuchumi kwa wakazi wa eneo hilo.
Kwa sababu ulipangwa kusaidia uzalishaji wa vifaranga vya samaki, kukuza ufugaji wa samaki wa maji baridi na kutoa ajira kwa vijana wa Kusini mwa Tanzania. Hata hivyo, miaka zaidi ya 10 baadaye, mradi huo umesimama bila maelezo ya kuridhisha, huku wananchi waliotoa ardhi yao wakibaki bila fidia stahiki.
Kwa wakazi wa Nyengedi, ni kama ndoto ya maendeleo sasa imegeuka kuwa mzigo wa maisha.
Mzee Ismail Mituka, mkazi wa Kata ya Nyandeni, ni miongoni mwa walioguswa moja kwa moja na mradi huo.
Anasimulia kwa masikitiko jinsi alivyojitolea kupisha mradi kwa matumaini ya kunufaika na maendeleo, lakini badala yake akajikuta akiingia kwenye mzunguko wa ahadi zisizotekelezwa.
Ilivyokuwa
Anasema safari ya mradi huo ilianza miaka ya 2000 pale mwekezaji mmoja wa kigeni alipowasili eneo hilo, akiwa na mshirika wa ndani, akiwashawishi wananchi kupisha maeneo yao ili kuanzisha mradi wa ufugaji wa samaki.
“Walituambia huu ni mradi mkubwa, utaleta maendeleo, ajira na kuinua maisha ya wananchi. Sisi tukakubali kupisha maeneo yetu kwa hiari kabisa,” anasema Mituka.
Mituka anasema awali mwekezaji huyo alionesha nia ya kulipa fidia moja kwa moja kwa wananchi, lakini baadaye mchakato huo ulisimamishwa na mamlaka za Serikali na kuelekezwa kufanyika kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mtama.
Hatua hiyo, kwa mujibu wa wananchi, ndiyo iliyoanza kuibua dosari katika utekelezaji wa mradi huo.
Mituka anasema baada ya tathmini kufanyika, alipewa fidia ambayo haikuendana na thamani halisi ya mali zake.
“Nilikuwa na ekari 1.4 zenye minazi, michikichi na mazao mengine, lakini nikaambiwa nilipwe Sh210,000. Hiyo haikuwa haki kabisa,” anasema Mituka.
Anasema alikataa kupokea fedha hizo, huku baadhi ya wananchi wakilazimika kukubali kutokana na hofu ya kupoteza kila kitu. Hata hivyo, wale waliokataa walirudishiwa maeneo yao na kuendelea na shughuli za kilimo kwa muda.
Lakini matumaini hayo hayakudumu kwa muda mrefu. Miaka kadhaa baadaye, Serikali ilirejea tena na mpango mpya wa kuanzisha kituo cha kanda cha ukuzaji viumbe maji kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Wananchi waliitwa tena na kuombwa kupisha maeneo yao, safari hii wakiahidiwa fidia kamili na ya haki.
“Walituambia huu ni mradi wa Serikali, fedha zipo tayari, sisi tusubiri tu taratibu zikamilike,” anasema Mituka.
Mituka anasema tathmini mpya ilionesha kuwa fidia kwa wananchi ilihitaji takribani Sh53 milioni. Hata hivyo, kiasi kilichopatikana kilikuwa Sh21 milioni pekee, hali iliyosababisha utekelezaji wa mradi kuanza kwa kusuasua.
Pamoja na upungufu huo wa fedha, ujenzi ulianza kwa kuchimba mabwawa mawili na kujenga baadhi ya miundombinu. Lakini baada ya muda mfupi, shughuli zilisitishwa na makandarasi kuondoka eneo hilo.
Eneo la mradi huo limebaki na mabaki ya majengo yasiyokamilika, mabwawa yaliyotelekezwa na ukimya unaoashiria kushindwa kwa mpango uliokuwa na matarajio makubwa.
Kwa wananchi, athari za kusimama kwa mradi huo ni kubwa, kwanza, wengi wao walipoteza ardhi yao bila kulipwa fidia. Pili, walishindwa kuendelea na shughuli zao za uzalishaji kama kilimo, hali iliyosababisha kushuka kwa kipato chao. Tatu, ajira zilizokuwa zimetarajiwa hazikutokea.
“Unachukua eneo langu halafu hunilipi, na wakati huo huo huniruhusu nifanye shughuli zangu. Hapo maendeleo yapo wapi?” anauliza Mituka.
Anasema katika kipindi walichokuwa wakisubiri fidia, mazao yao mengi yaliharibika na kupotea, hali iliyowaacha katika mazingira magumu zaidi ya kiuchumi.
Mituka anasema baadhi ya wananchi walijaribu kurejea kwenye maeneo yao ili kuendelea na shughuli za kilimo baada ya kuona mradi umesimama, lakini walikumbana na vitisho vya kisheria.
“Tuliambiwa tukirudi pale tutashtakiwa kwa kuharibu miundombinu ya mradi. Tukaogopa. Mpaka leo hatujui hatima yetu,” anasema.
Hali hiyo imewaweka wananchi katika hali ya sintofahamu, hawawezi kutumia ardhi yao wala hawajalipwa fidia.
Itaendelea kesho