Dar es Salaam. Viongozi mbalimbali wa Serikali na sekta binafsi, wametembelea nyumbani kwa Mwenyekiti wa zamani wa Bodi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Leonard Mususa, aliyefariki dunia Mei 30, 2026.
Mususa aliyeiongoza bodi ya MCL kuanzia mwaka 2015, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 72. Tayari alishatumikia nafasi mbalimbali katika sekta binafsi na umma kwa zaidi ya miongo mitatu.
Kabla ya kujiunga na MCL, Mususa alihudumu wadhifa wa Mwakilishi Mwenza wa Kampuni ya Ukaguzi ya Price House Water Coopers Ltd kwa miaka 14 na alistaafu mwaka 2014.
Kwa upande wa Serikali, waliotembelea nyumbani hapo, Masaki jijini Dar es Salaam ulipo msiba ni Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Bakari Machumu, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa MCL.
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji mstaafu wa MCL, Bakari Machumu, akisaini kitabu cha maombolezo nyumbani kwa marehemu Leonard Mususa, aliyefariki Dunia Mei 30, 2026.
Machumu, alifika msibani usiku wa jana Jumapili, akiambatana na waombolezaji wengine.
Pia, alikuwepo Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.
Balozi Ulanga pia, alikuwa sehemu ya bodi ya MCL chini ya Mususa. Alikuwa mjumbe wa bodi hiyo, kabla ya baadaye kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kuwa balozi.
Sambamba na hao, wageni wengine waliofika nyumbani hapo kwa Mususa ni Mkurugenzi Mtendaji wa MCL, Rosalyn Mndolwa-Mworia, Mhariri Mtendaji Mkuu wa MCL, Mpoki Thomson na watumishi wengine wa Kampuni hiyo.
Ratiba ya msiba
Kwa mujibu wa ratiba iliyosambazwa na familia ya marehemu, mwili wa Mususa unatarajiwa kuzikwa kesho Jumanne, Juni 2, 2026 katika makaburi ya Kondo jijini Dar es Salaam.
Leo Jumatatu, Juni 1, 2026 mwili wake utapokewa nyumbani kwake Masaki, ratiba itakayotanguliwa na mlo wa mchana, kisha misa maalumu itakayofanyika nyumbani.
Kesho Juni 2, 2026 ratiba itaanza na chai kisha ibada katika Kanisa la St. Peter, itafuatiwa na heshima za mwisho na safari ya kwenda makaburi ya Kondo kwa ajili ya maziko itafuata.
Huyu ndiye Mususa
Mususa alifahamika zaidi ya taaluma yake ya uhasibu na anatajwa kuwa miongoni mwa waanzilishi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA).
Alizaliwa Septemba 25, mwaka 1953 katika visiwa vya Ukerewe mkoani Mwanza, eneo ambalo alipata elimu yake ya msingi na baadaye kujiunga na sekondari katika Shule ya Sekondari Kibaha.
Mkurugenzi wa Diplomasia ya Uchumi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi John Ulanga.
Mususa ambaye ni mtoto wa pili kati ya saba wa wazazi wake, alisoma Chuo Kikuu nchini Uingereza na alipomaliza alipata nafasi ya kuwa Mkufunzi katika Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) kwa takriban mwaka mmoja.
Baadaye, akahamia katika Kampuni ya Ukaguzi ya Price House Water Coopers Ltd, ilivyokuwa inawakilisha Afrika Kusini, Uingereza na Tanzania na alistaafu mwaka 2014 baada ya kuhudumu kwa takriban miaka 36.
Pia, Mususa ni mmoja wa waasisi wa CEO Roundtable alihudumu kwa nafasi ya Mwenyekiti wa bodi kwa miaka 10 na aliwahi kuwa mjumbe wa Tume ya Rais ya Kurekebisha Mifumo ya Kodi akiteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan.