Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Revocatus Chipando maarufu Baba Levo amesema anatamani kuona maridhiano yatakayoliunganisha Taifa na kujenga heshima kati ya watawala na wapinzani ili nchi ‘itembee’ katika njia inayofaa.

Anasema uwepo wa upinzani ni muhimu kwa sababu husaidia kuonesha maeneo yenye changamoto ndani ya Serikali akisisitiza kuwa: “Napenda kuwepo kwa upinzani kwa sababu wanapokosoa wanakuonyesha sehemu zenye matatizo.”

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, yaliyofanyika nyumbani kwake jijini Dar es Salaam hivi karibuni, mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa Bongo Flava, anasema anatamani kuona maridhiano ambayo watawala watatambua kuwa, kukosolewa ni njia ya kujenga na kusahihisha makosa ili kuchochea maendeleo ya Taifa.

Baba Levo alichaguliwa kuingia bungeni kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba 29, 2025 baada ya kuwashinda wagombea wenzake kutoka upinzani akiwemo mbunge wa zamani katika jimbo hilo, Zitto Kabwe wa ACT-Wazalendo.

Katika mahojiano hayo, anasema: “Natamani sana tuwe na maridhiano ambayo yatarudisha Taifa tuwe pamoja, yatakayofanya mtawala amheshimu mpinzani na mpinzani amheshimu mtawala; maridhiano ambayo yatafanya Watanzania wawe na imani na watu waliowapa dhamana ya kuwaongoza.

“Natamani yawe ni maridhiano yatakayowafanya watawala kutambua mtu anapokosoa, hakosoi kwa sababu ya masilahi yake binafsi, anakosoa ili kuhakikisha nchi yetu inapata njia bora ya kutembea. Yawe ni maridhiano ambayo yatatuvusha kwenye mustakabali mwingine kabisa,” anasema.

Baba Levo aliyewahi kuwa Diwani wa Mwanga, Mkoa wa Kigoma kupitia ACT- Wazalendo, anasema anatamani kuona Taifa likitoka kwenye mkwamo wa sasa wa kisiasa na kuingia katika hatua mpya ya maelewano, kuheshimiana na mshikamano wa kitaifa.

Hali ya kisiasa ya mvutano

Akizungumzia hali ya kisiasa nchini, Baba Levo anasema imekuwa na mvutano kiasi kwamba kutokana na uhuru uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha demokrasia, wananchi wamekuwa huru kueleza mawazo yao, jambo ambalo wakati mwingine limechangia mvutano wa kisiasa uliopo sasa.

“Hali ya kisiasa Tanzania imekuwa na mvutano kidogo kutokana na namna Rais Samia alivyoamua kuiongoza nchi kwa kutoa uhuru kwa upinzani kueleza maoni yao.

“Yote haya yanatokea ni kwa sababu Rais Samia ameamua kuwa mwanademokrasia kama alivyozoea katika maisha yake yote, kwa hiyo ameamua kuacha watu waongee,” anasema Baba Levo.  

Pia, anasema uwepo wa uhuru huenda sambamba na changamoto zake kwa kuwa, baadhi ya watu hutumia nafasi hiyo kwa kufuata utaratibu huku wengine wakitumia vibaya kwa lengo la kuvuruga au kutoa lugha zisizofaa.

“Ndiyo maana unaona kuna watu wanaosema mambo kwa nia ya kuvuruga au hata kutoa matusi na maneno yasiyofaa majukwaani, hiyo ni kwa sababu kuna uhuru wa kutoa mawazo,” anasema.

Baba Levo anasema hali hiyo inatokana na msimamo wa Rais Samia wa kuamini katika demokrasia na kuwapa watu nafasi ya kuzungumza kwa uhuru, jambo ambalo wananchi wamekuwa wakilitumia kwa kiwango kikubwa.

Umuhimu wa upinzani

Akizungumzia kuhusu upinzani, Baba Levo anasema binafsi anaona uwepo wa upinzani ni muhimu kwa sababu husaidia kuonesha maeneo yenye changamoto ndani ya Serikali.

“Napenda kuwepo kwa upinzani kwa sababu wanapokosoa wanakuonesha sehemu zenye matatizo. Wakati mwingine unaweza usione changamoto zote, lakini wanaokukosoa wanaweza kukuonesha wapi pa kurekebisha,” anasema.

Pia, anasema kama kiongozi ni msikivu, hali hiyo husaidia kuziba upungufu uliopo na kuimarisha utendaji wa Serikali, ingawa kwa mtazamo wake, hali ya kisiasa nchini inaendelea vizuri katika kujenga demokrasia.

Kuhusu matukio ya vurugu na ghasia ya Oktoba 29, 2025, Baba Levo anasema hatamani kuona tukio kama hilo likijirudia, akieleza Watanzania wengi walipoteza ndugu na marafiki katika mazingira ambayo yangeweza kutatuliwa bila madhara makubwa.

Pamoja na hali hiyo, anasema anamshukuru Rais Samia kwa kuamua kushughulikia suala hilo kwa njia ya kisheria kupitia kuundwa kwa tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.

Ripoti ya Jaji Chande ilionesha watu 518 walipoteza maisha, majeruhi na uharibifu wa mali.

“Namshukuru Rais Samia kwa kuunda tume iliyofanya uchunguzi na kutoa taarifa ambayo wananchi wengi tayari wanaifahamu, ikieleza chanzo cha vurugu hizo,” anasema.

Pia, anasema tume hiyo ilifanya kazi kwa uwazi na Serikali imeunda tume nyingine ya kijinai ili kubaini waliohusika kupanga na kusababisha vurugu hizo, pamoja na waliokosea katika kuzizuia.

“Kikubwa tusubiri matokeo ya uchunguzi huo wa kijinai ili ukweli ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe,” anasema.

Akiwasilisha taarifa ya matokeo ya ripoti hiyo Aprili 23, 2026, Jaji Chande alitaja vyanzo vitano na vichocheo vinne vya vurugu hizo, ikiwamo kauli za wanasiasa, matukio ya utekaji, pamoja na ushawishi wa baadhi ya wagombea waliokatwa kwenye vyama vyao.

Pia, ripoti hiyo ilibaini kuwa vurugu hizo zilipangwa kwa kutumia watu wasiokuwa na uelewa wa kutosha, waliokusanywa kutoka maeneo mbalimbali kama vyuoni, masokoni na sehemu nyingine kwa lengo la kushawishiwa kushiriki maandamano.

Ahimiza ushirikiano

Baba levo anawataka wananchi wa Kigoma Mjini kuendelea kumpa ushirikiano na kumueleza changamoto zao ili aweze kuwatumikia kwa ufanisi zaidi.

“Matatizo yaliyokuwa yanajitokeza Kigoma Mjini hapo awali hayatokei tena. Kwa mfano, Ziwa Tanganyika kiutaratibu lilitakiwa liwe limefungwa kwa miezi mitatu kupisha mazalia mapya lakini halijafungwa kwa sababu tunafahamu wananchi wengi wanategemea shughuli hizo kujipatia kipato na tayari tumezungumza na Serikali kuhusu hilo,” anasema.

Anasema alizungumza na Waziri wa Uvuvi na Mifugo akimueleza athari za kufunga ziwa kwa miezi mitatu alimuelewa na maisha yanaendelea kama ilivyo kawaida.

“Natoa wito kwa wananchi wa Kigoma wasimame na mimi, naamini tutavuka salama, Rais Samia amekuwa akipenda mji wa Kigoma upige hatua za kimaendeleo,” anasema.

Anasema Serikali inaendelea kuonesha dhamira ya kuendeleza Kigoma kupitia maboresho ya miundombinu ya reli na usafiri wa majini, jambo ambalo litachochea ukuaji wa uchumi wa mkoa huo.

“Kuna meli mpya inajengwa Ziwa Tanganyika, ina maana Reli ya Kisasa (SGR) ikitoka Dar es Salaam ikifika Kigoma inangia moja kwa moja kwenye kivuko na mabehewa yake na kwenda kusambazwa kwenye bandari kama ni Kalemii au Burundi au Zambia,” anasema.

“Namuomba Rais aendelee kunisikiliza kwa sababu amenitoa mbali. Nilikuwa naishi maisha magumu, na si rahisi kwa CCM kumuamini mtu hadi kumpa nafasi ya kugombea ubunge,” anasema.

Baba Levo anasema ushindani ndani ya CCM ni mkubwa kutokana na idadi kubwa ya wanaowania nafasi za uongozi, tofauti na alivyoshuhudia alipokuwa upande wa upinzani, wakati mwingine wagombea walikuwa wakitafutwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *