Dar es Salaam. Wakati Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ikisema haikionei Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uongozi wa chama hicho umedai kuwa ofisi hiyo imeshindwa kuzingatia misingi ya weledi na utawala bora katika utekelezaji wa majukumu yake, hususan kwa kuvujisha kwa umma barua zinazoandikiwa.
Pia, Chadema imeituhumu Ofisi ya Msajili kwa kupotosha umma kupitia kauli zinazotolewa kwa vyombo vya habari kwamba inakwenda kukutana na viongozi chama hicho kwa lengo la kutoa maelekezo kuhusu masuala ya kisheria, ilhali ilikuwa na dhamira nyingine tofauti na hiyo.
Hata hivyo, Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema Ofisi ya Msajili haiionei Chadema, bali inasimamia utekelezaji wa Sheria ya Vyama vya Siasa kwa vyama vyote bila upendeleo.
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa,Sisty Nyahoza (wapili kulia) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Chadema, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Kwa muda mrefu, Chadema na ofisi hiyo wamekuwa katika mvutano kupitia mawasiliano ya barua na matamko kwa vyombo vya habari, huku kila upande ukiutuhumu mwenzake kwa masuala mbalimbali.
Ofisi ya Msajili imekuwa ikiituhumu Chadema kukiuka masharti ya Sheria ya Vyama vya Siasa ya mwaka 2019 zikiwamo kauli za viongozi zinazotafsiriwa kuwa za matusi au zinazokiuka misingi ya sheria na Katiba ya nchi.
Chadema nayo imekuwa ikijibu tuhuma hizo kwa kuikosoa ofisi hiyo kwa madai ya matumizi mabaya ya mamlaka na kuendesha mikakati inayolenga kuidhoofisha.
Mwezi mmoja uliopita, Chadema ilipokea barua mbili za kutakiwa kujieleza kwa nini isichukuliwe hatua za kisheria, ikiwamo kufutiwa usajili au kutozwa faini, kutokana na kauli zinazodaiwa kutolewa na baadhi ya viongozi wake katika mikutano ya hadhara iliyofanyika nchini.
Jana Jumatatu, Juni mosi, 2026, pande hizo mbili zilikutana katika makao makuu ya Chadema, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kujadili baadhi ya sintofahamu ambazo hazikusemwa hadharani.
Kikao hicho pia kilihusisha ukaguzi wa muundo wa dawati la jinsia ndani ya chama.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa amesema, “haiwezekani barua inaandikwa kwa Chadema, lakini vyombo vya habari vinakuwa tayari vinafahamu maudhui yake kabla hatujaipokea au kuisoma. Hilo ni jambo linalozua maswali mengi.”
Golugwa akiwa mbele ya Nyahoza, ameitaka ofisi hiyo kuhakikisha vyama vyote vya siasa vinatendewa kwa usawa na kwa kuzingatia misingi ya utawala bora.
“Tumezungumza mambo mengi kuhusu namna ya kushughulikia barua hizi za kujieleza, lakini baadhi ya masuala hayo yanabaki kuwa ya ndani,” amesema.
Hata hivyo, Nyahoza amesema hata wingi wa barua zinazoandikwa kwa Chadema kuhitajika maelezo kuhusu kauli za viongozi wake, hauwezi kutumika kama kigezo cha kuonesha kuwa chama hicho kinaonewa.
“Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ni mlezi wa vyama vyote vya siasa. Vyama vyote ni watoto wetu na hatumpendelei mtu yeyote. Ndio maana tumekuja hapa Chadema na tumepokewa vizuri.
Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa,Sisty Nyahoza (wapili kulia) akiwa kwenye kikao na viongozi wa Chadema, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Michael Matemanga
Kama tungekuwa na uhusiano mbaya nao, tusingepokewa namna hii. Kazi yetu ni kuvilea vyama vyote na kuvielekeza pale panapojitokeza changamoto,” amesema Nyahoza.
Amesema njia bora kwa vyama vya siasa kuepuka kuandikiana barua mara kwa mara na Ofisi ya Msajili; ni kuzingatia kikamilifu Sheria ya Vyama vya Siasa pamoja na masharti ya usajili.
“Kama walezi wa vyama vya siasa, tunavihimiza vyama vyote kuzingatia Sheria ya Vyama vya Siasa na masharti ya usajili katika shughuli zao zote za kisiasa na kichama, ikiwamo mikutano ya hadhara inayofanyika kote nchini,” amesema.
Nyahoza amesema ofisi yake inatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria bila upendeleo wala ubaguzi.
Amefafanua kuwa, vifungu vya nne na vya tano vya sheria husika, vinaipa mamlaka ya kutekeleza wajibu wake kwa uhuru.
Akijibu kuhusu Chadema kuandikiwa barua nyingi za kujieleza, Nyahoza amesema idadi ya barua si kipimo sahihi cha kutathmini uhusiano kati ya chama na ofisi hiyo.
“Huwezi kupima jambo kwa kuangalia wingi wa barua zinazoandikwa. Muhimu ni kuangalia sababu iliyosababisha barua hiyo kuandikwa. Hatuionei Chadema,” amesema.
Awali, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema ziara hiyo haikulenga kuelimishana kuhusu sheria, bali ilihusu masuala mawili muhimu.
“Amekuja kuona muundo wa dawati la jinsia ndani ya chama na namna linavyofanya kazi. Pili, amekuja kufahamu mchakato wa utekelezaji wa sera ya jinsia na ushirikishwaji wa jamii.
Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza akizungumza na viongozi wa alipotembelea Makao Makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam..
“Umma uelewe kuwa ujio wa Ofisi ya Msajili katika makao makuu ya chama hauna uhusiano wowote na barua ambazo wamekuwa wakituandikia wakitaka tujieleze kuhusu kauli mbalimbali za viongozi wetu,” amesema Mnyika.
“Kimsingi, Chadema ndiyo iliyoialika Ofisi ya Msajili kutekeleza wajibu wake kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa, kifungu cha 10(c), kinachohusu uundwaji wa madawati ya jinsia na utekelezaji wa sera husika.
“Tumeona ni vyema kuwapa nafasi hiyo, ingawa tunaendelea kuwa na mtazamo kwamba ofisi hiyo imekuwa ikitoa taarifa zinazopotosha,” amesema.
Mnyika amesema ziara hiyo ilitokana na barua iliyotumwa na Ofisi ya Msajili Aprili 28, 2026 kwa makatibu wa vyama vya siasa, ikieleza dhamira ya kutembelea vyama hivyo kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa masuala ya jinsia kwa mujibu wa sheria.
“Baada ya kupokea barua hiyo, tuliwajibu kwamba muda waliopendekeza haukuwa mwafaka kwetu. Tulipendekeza Juni 1, 2026 kuwa siku ya kukutana. Hivyo, ujio wao hauna uhusiano wowote na barua nyingine ambazo wamekuwa wakitutaka kujieleza kuhusu kauli za viongozi wetu,” amesema.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho, Nyahoza amekiri kuwa ujio wa timu yake katika makao makuu ya Chadema ulilenga kukagua muundo wa dawati la jinsia na kujionea mkakati wa utekelezaji wa shughuli zake ndani ya chama.