Lindi/Mtwara. Nyuma ya uzio unaozunguka Mradi wa Nyengedi, kuna simulizi za wananchi waliopoteza ardhi yao kwa matumaini ya maendeleo, lakini mpaka sasa wamebaki bila fidia wala majibu.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini mradi huo haukuishia tu kukwama, bali umeacha athari kwa wakazi waliotoa maeneo yao kupisha uwekezaji huo.

Ismail Mituka, mkazi wa Kata ya Nyandeni ni miongoni mwa walioathirika.

Anasema walikubali kupisha maeneo yao kwa hiari baada ya kuahidiwa maendeleo na ajira.

“Walituambia huu ni mradi mkubwa utakaobadilisha maisha yetu. Tukakubali kutoa ardhi yetu,” anasema.

Hata hivyo, baada ya tathmini kufanyika, baadhi ya wananchi walipewa viwango vya fidia ambavyo havikuendana na thamani ya mali zao.

Mituka anasema kwa ekari 1.4 yenye mazao ya kudumu, alitakiwa kulipwa Sh210,000 alizozikataa.

Anasema baadaye, Serikali ilirejea na mpango mpya, akisema tathmini ilionesha kuwa, wananchi walihitaji takribani Sh53 milioni.

Hata hivyo, anasema kiasi kilichopatikana kilikuwa Sh21 milioni pekee.

Anasema upungufu huo wa fedha ulisababisha utekelezaji wa mradi kuanza kwa kusuasua na hatimaye kusimama.

Anasema kuwa, baadhi ya wananchi hawajalipwa fidia, huku wakizuiwa kutumia ardhi zao kwa hofu ya hatua za kisheria.

“Unachukua ardhi yangu halafu hunilipi, na wakati huo huo huniruhusu kufanya shughuli zangu. Hapo maendeleo yapo wapi?” anauliza Mituka.

Uchunguzi zaidi unaonesha changamoto za mradi huo hazikuishia kwa wananchi pekee.

Hata mkandarasi aliyekuwa akitekeleza mradi huo alidaiwa kushindwa kulipwa fedha zake, hali iliyomlazimu kusitisha kazi na kuondoka.

Pamoja na hayo, wananchi wanahoji hatima ya fedha zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo.

Wanasema waliambiwa kuwa kulikuwa na bajeti ya hadi Sh500 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, ikiwamo fidia kwa wananchi.

Hata hivyo, wanadai kuwa sehemu ya fedha hizo haikutumika na ilirejeshwa serikalini baada ya mwaka wa fedha kuisha.

“Kama fedha zilikuwepo, kwa nini hatukulipwa? Hili ndilo swali ambalo halijapata majibu mpaka leo,” anasema mmoja wa wananchi aliyetoa eneo lake.

Kwa upande mwingine, wataalamu wa maendeleo wanasema mradi wa Nyengedi ungeweza kuwa chachu ya ukuaji wa uchumi katika mkoa wa Lindi, ambao una rasilimali nyingi za bahari lakini bado hazijatumika ipasavyo.

Kulingana na jiografia ya Tanzania, Lindi ni miongoni mwa maeneo yenye fursa kubwa katika sekta ya uchumi wa buluu, ikiwamo ufugaji wa samaki na uvuvi wa kisasa. Hata hivyo, kusuasua kwa miradi ya kimkakati kunakwamisha jitihada za kunufaika na rasilimali hizo.

Kama Mradi wa Nyengedi ungekamilika kwa wakati, ungeweza kutoa ajira kwa vijana wengi, kuongeza uzalishaji wa samaki na kuchangia katika usalama wa chakula nchini. Lakini kwa sasa, ndoto hiyo imebaki kuwa simulizi.

Waathirika wa mradi huo wanasema wamefanya jitihada mbalimbali kufuatilia haki yao, ikiwa ni pamoja na kufika katika ofisi za ardhi na mamlaka za wilaya, lakini hawajapata majibu ya kuridhisha.

“Tumekuwa tukiahidiwa kila mwaka kuwa tusubiri mwaka wa fedha ujao. Lakini miaka inaenda, hakuna kinachobadilika,” anasema Mituka.

Kwa baadhi yao, suala hili limepoteza hata mvuto wa kisiasa, wakidai kuwa ahadi za viongozi hazijawasaidia chochote.

“Sasa hivi hata tukisikia ahadi, hatuna tena imani. Tumebaki kusubiri tu, lakini matumaini yamepungua sana,” anasema.

Mwathirika mwingine wa mradi wa Nyengedi unaodaiwa kusuasua ni Ibrahim Alage (75), ambaye anasema anamiliki eneo lenye ukubwa wa nusu ekari, awali alikadiriwa kulipwa fidia ya Sh3.85 milioni.

Anadai baada ya zoezi la tathmini, hakupatiwa nakala ya nyaraka za makadirio kwa kuwa, zilichukuliwa na wahusika, huku malipo yakifanyika kwa watu wachache tu katika eneo hilo.

Akieleza mkanganyiko uliopo, anasema mwaka juzi kulifanyika ziara ya Waziri wa Uvuvi, wakulima waliagizwa kukusanyika ili kuwasilisha kero zao.

Hata hivyo, hali ilibadilika ghafla baada ya baadhi ya viongozi kuzungumza na waziri huyo, baadaye ikaelezwa hapakuwa na nafasi ya kuwasilisha malalamiko.

“Naona kabisa kulikuwa na mazingira ya sisi kunyimwa fursa ya kueleza matatizo yetu,” anasema.

Aidha, anabainisha kuwa pamoja na maelekezo ya kuitishwa mkutano wa kijiji, hadi sasa hakuna hatua madhubuti iliyochukuliwa, huku yeye akiwa bado hajapokea taarifa yoyote rasmi kuhusu hatma ya fidia yake.

Mzee huyo anaeleza kuwa eneo lake lina mazao ya kudumu ikiwamo miembe na michikichi, hali inayomfanya kushindwa kuendelea na shughuli zake za uzalishaji kutokana na sintofahamu iliyopo.

“Mpaka leo sijapewa hata barua rasmi, muda unaenda. Inaonekana labda tukifa ndipo watoto wetu watakuja kulipwa,” anasema kwa masikitiko.

Anaiomba Serikali kutoa tamko rasmi iwapo mradi huo umeshindikana, ili wananchi waweze kuamua mustakabali wa maeneo yao badala ya kuendelea kusubiri bila majibu.

Kwa mujibu wa maelezo yake, mradi huo ulipangwa kujumuisha mabwawa ya samaki kwa ukanda wa kusini, na hata baadhi ya viongozi kutoka Dodoma walitembelea eneo hilo na kulipongeza kuwa, linafaa kwa uwekezaji huo pamoja na ujenzi wa miundombinu mingine na ingekuwa fursa ya ajira kwa vijana.

Hata hivyo, anadai mkandarasi aliyekuwapo aliondoka ghafla baada ya kung’oa vifaa vyake, jambo linaloashiria kuwa mradi huo huenda umesitishwa bila taarifa rasmi.

Anasisitiza kutokana na mali zake, ikiwamo minazi kukatwa na ardhi kutumika kwa muda mrefu, ni haki yake kulipwa fidia stahiki au kupewa ruhusa rasmi ya kuendelea na shughuli zake.

Kisa cha Nyengedi kinaibua maswali kuhusu usimamizi wa miradi ya maendeleo, uwajibikaji wa taasisi za umma na haki za wananchi wanaotoa rasilimali zao kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Ni jambo la kujiuliza, je, maendeleo yanaweza kuitwa maendeleo kama yanawaacha wananchi katika umaskini na mateso?

Kwa wakazi wa Nyengedi, jibu la swali hilo linaonekana wazi katika maisha yao ya kila siku, ya kusubiri, kukosa na kuishi na matumaini yaliyoyeyuka.

Hali hii imeibua mjadala kuhusu ufanisi wa usimamizi wa miradi ya maendeleo, na kuacha pengo kati ya mipango ya sera na utekelezaji halisi, huku wananchi waliotarajia kunufaika na miradi hiyo wakiendelea kusubiri majibu.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, suala la kuondoa umaskini linaelekezwa kupitia Ibara ya 9(i), ambayo inaitaka Serikali kuhakikisha kuwa utajiri wa taifa unahifadhiwa, unasimamiwa na kusambazwa kwa manufaa ya wananchi wote huku ikizuia hali ya kujilimbikizia mali kwa watu wachache na kuwaacha wengine katika umaskini.

Ibara hii inaweka msingi wa kuhakikisha kuwepo kwa usawa wa kiuchumi na fursa kwa wananchi wote, sambamba na wajibu wa Serikali kuandaa sera na mipango inayolenga kupunguza pengo la kipato na kuinua hali ya maisha ya wananchi kwa jumla.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *