
Bei ya mafuta duniani yapanda huku majeshi ya Israel yakisonga ndani zaidi kusini mwa Lebanon
Shirika la habari la Reuters liliripoti Jumatatu kuwa bei ya mafuta ilipanda kwa zaidi ya asilimia 3, baada ya Iran na Marekani kushambuliana, na huku utawala wa Israel ukiwaagiza wanajeshi wake kuingia zaidi ndani ya Lebanon.
Hatima ya mafuta ghafi ya Marekani ilipanda kwa dola 2.88—sawa na asilimia 3.3—na kufikia dola 90.24 kwa pipa kufikia. Nayo mafuta ya Brent yaliongezeka kwa dola 2.78, au asilimia 3.05, na kufikia dola 93.9 kwa pipa.
Wataalamu wanasema endapo kutatokea kuongezeka zaidi kwa ghasia, au kukawa na hitilafu ya usambazaji wa mafuta na gesi katika Ghuba ya Uajemi, kuna uwezekano bei kupanda zaidi ya kiwango hiki.
Hapo awali, ripoti zilizodai kuwepo kwa “maendeleo yanayotia moyo” kuelekea mwafaka wa mwisho kati ya Marekani na Iran zilikuwa zimesababisha Brent na WTI kushuka na kufunga soko kwa upungufu wa asilimia 1.8 na 1.7 mtawalia.
Hata hivyo, kushadidi uvamizi wa jeshi la Israel nchini kumeondoa matarajio ya kuwa Marekani na Iran zingefikia makubaliano ya amani karibuni au kuongeza muda wa usitishaji mapigano uliopatanishwa na Pakistan.
Iran imesisitiza kuwa usitishaji mapigano nchini Lebanon hauwezi kutenganishwa na makubaliano yoyote ya mwisho ya kusitisha vita, huku utawala wa Israel ukituhumiwa kuendeleza mashambulizi dhidi ya Lebanon kinyume na makubaliano ya awali ya sitisho la mapigano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Esmaeil Baghaei, alisema Jumatatu kuwa usitishaji mapigano nchini Lebanon ni sehemu isiyotenganishwa na mpango wowote wa mwisho wa kumaliza vita.