
Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) limesema limefanya shambulio la kulipiza kisasi dhidi ya kambi ya anga iliyotumiwa na Marekani kuanzisha mashambulizi ya kijeshi dhidi ya mnara wa mawasiliano katika kusini mwa Iran.
Katika taarifa iliyotolewa Jumatatu, IRGC imesema Kikosi chake cha Anga za Juu kilishambulia na kuharibu kambi hiyo ya anga, ambako kwa mujibu wa taarifa hiyo, jeshi vamizi la Marekani lilianzisha shambulio dhidi ya mnara wa mawasiliano katika Kisiwa cha Sirik, kilichoko katika Mkoa wa Hormozgan kusini mwa Iran.
Taarifa hiyo imesema kuwa: “Kufuatia hujuma iliyofanywa na jeshi vamizi la Marekani dhidi ya mnara wa mawasiliano katika Kisiwa cha Sirik, Mkoa wa Hormozgan, wapiganaji wa Kikosi cha Anga za Juu cha IRGC walilenga kambi ya anga ambako shambulio hilo lilianzia, na malengo yaliyokuwa yameainishwa mapema yakaharibiwa.”
Kikosi hicho pia kimetoa onyo kali dhidi ya hatua zozote zaidi za kijeshi, kikisisitiza kuwa mashambulizi yoyote yajayo yatakabiliwa na jibu kali zaidi.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo: “Kikosi cha Anga za Juu cha IRGC kimeonya kwamba iwapo hujuma hii itarudiwa, jibu litakuwa tofauti kabisa, na dhima ya madhara yake itabebwa na utawala vamizi wa Marekani, unaoua watoto.”
Maendeleo hayo yamekuja baada ya Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani katika eneo la Asia Magharibi (CENTCOM) kusema mwishoni mwa Jumapili kuwa ilitekeleza kile ilichodai kuwa eti ni mashambulizi ya kujihami dhidi ya vituo vya rada vya Iran pamoja na miundombinu ya uongozi na udhibiti wa ndege zisizo na rubani katika mji wa Goruk na katika Kisiwa cha Qeshm.
Hata hivyo, Idara ya Mahusiano ya Umma ya IRGC ilisema katika taarifa yake yake kuwa vikosi vya ulinzi wa anga vya jeshi hilo viligundua na kufanikiwa kuitungua ndege vamizi isiyo na rubani au droni aina ya MQ-1 Predator inayomilikiwa na jeshi vamizi la Marekani, muda mfupi baada ya kuingia ndani ya anga ya Iran juu ya Ghuba ya Uajemi.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa ndege hiyo isiyo na rubani, yenye uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali kwa muda mrefu angani, ilinaswa na kuharibiwa mara tu ilipoingia katika anga ya Iran katika saa za awali za Jumapili.