Dar/Masasi. Mahakama Kuu iliyoketi kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam na Masasi mkoani Mtwara, imewahukumu adhabu ya kifo, wanaume wawili baada ya kuthibitika bila shaka kuwa ndio waliofanya mauaji kutokana na wivu wa mapenzi.

Jijini Dar es Salaam, Mussa Mchoro alimuua mpenzi wake kwa kumnyonga baada ya kufanya naye mapenzi ambapo asubuhi majirani walipoona haamki, walifungua mlango na kukuta mtoto wao mdogo anajaribu kumuamsha mama yake.

Kwa upande wa tukio la Mtwara, Juma Athuman,  maarufu Fundi J, alimuua Frank Shoo au ‘Mangi’ kwa kumkata na panga kichwani, shingoni na usoni, akimshuku kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mmoja wa wake zake.

Katika hukumu walizozitoa Mei 29, 2026 na kuwekwa katika tovuti ya mahakama jana Jumatatu, Juni 1, 2026, Jaji Hamidu Mwanga wa Masjala ndogo ya Dar es Salaam na Edwin Kakolaki wa Masjala ndogo ya Mtwara, wamewahukumu adhabu ya kifo.

Majaji hao walisema kwa sheria za Tanzania, Kanuni ya Adhabu (Penal Code) kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2023, adhabu pekee kwa mtu anayepatikana na hatia ya kuua kwa kukusudia, ni moja tu nayo ni kunyongwa hadi kufa.

Mauaji Tabata Mawenzi

Kulingana na hukumu ya Jaji Mwanga, Mussa Mchoro alishtakiwa kwa kufanya mauaji ya mpenzi wake, Zainab Mazige yaliyotokea Machi 3,2025 huko Tabata Mawenzi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, kwa kumnyonga shingo.

Ni kesi ya upande wa mashtaka kwamba mshtakiwa na marehemu walikuwa wakiishi pamoja kama washirika chini ya kile kilichoelezwa kama ndoa ya mkeka, na walibarikiwa mtoto mmoja, ambaye jina lake tunalihifadhi kwa sasa.

Hata hivyo, uhusiano wao baadaye ukawa na shida kutokana na kutokuelewana mara kwa mara, haswa tuhuma za ukafiri, kutoelewana kuhusu ajira, na migogoro inayohusu majukumu ya wazazi juu ya mtoto wao huyo mdogo.

Mvutano ulipozidi kuongezeka, marehemu aliacha makazi yao ya kawaida Kunduchi na alirudi katika nyumba ya wazazi wake iliyoko Tabata Mawenzi, ingawa mtuhumiwa aliendelea kuwatembelea mtoto na marehemu mara kwa mara.

Machi 2, 2025, saa 9:00 alasiri, mshtakiwa alimtembelea marehemu nyumbani kwao ambapo mama yake hakuwepo alikwenda mkoani Tanga kwenye mipango ya mazishi ya jamaa yao.

Waliokuwepo siku hiyo ni marehemu, mdogo wake, Fatuma Shafii Mazige, kaka yake Olvin Salim Mazige, na mtoto mdogo wa wanandoa hao na usiku walishiriki chakula cha jioni, baada ya hapo mshtakiwa alibaki ndani ya nyumba.

Baadaye usiku, marehemu na mshtakiwa waliiingia katika chumba cha marehemu, ambapo, kulingana na mwendesha mashtaka walilala pamoja.

Asubuhi ya Machi 3, 2025, wasiwasi ulianza kuibuka baada ya marehemu kushindwa kuamka, jambo ambalo halikuwa la kawaida.

Wanafamilia waligundua kuwa mlango wa kuingilia ulikuwa umeachwa wazi na walipoingia chumbani kwake, walimkuta marehemu amelala akiwa mtupu na bila kuitikia huku mtoto wake mdogo akibaki karibu akijaribu kumwamsha.

Kwa kuwa mshtakiwa ndiye mtu wa mwisho kuwa na marehemu hadi usiku wa manane, ndugu na majirani walijaribu kumpigia simu ikawa haipatikani lakini ilipopatikana aliombwa afike mara moja kwani mzazi mwenzake hali yake sio nzuri.

Alirudi na ndipo alipokamatwa na Polisi ambao tayari walikuwa wameshafika na wakati huohuo mzazi mwenzake akapelekwa Hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam na kuthibitika alikuwa amefariki hivyo suala likageuka kuwa mauaji.

Wakati wa uchunguzi, polisi walimuhoji mshtakiwa na kuandika maelezo yake ya onyo ambapo alikiri kumtembelea mzazi mwenzake na walikaa usiku ingawa walitofautiana na akaamua kutoka kwenye nyumba na kumuacha marehemu.

Lakini alipofikishwa kortini na kusomewa shtaka la mauaji, alilikanusha.

Hukumu ya Jaji Mwanga

Katika hukumu yake, Jaji Mwanga alisema hakuna shahidi hata mmoja wa Jamhuri aliyesema alishuhudia mshtakiwa akimnyonga marehemu bali ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka uliegemea katika ushahidi wa mazingira.

Jaji alisema shahidi namba 5,  Olvin Salim Mazige, alieleza kinagaubaga kuwa Machi 2,2025  saa 3:00 usiku aliporudi nyumbani, alimkuta mshtakiwa pamoja na marehemu, aliwatazama wakila na baadaye waliingia chumbani na kulala.

Kulingana na yeye, karibu 7:00 usiku alipoamka kwa ajili ya kwenda kujisaidia haja ndogo, aliona viatu vya mshtakiwa hivyo kuthibitisha kuendelea kuwepo kwa mshtakiwa lakini alipoamka asubuhi hakuvikuta na mlango ulikuwa wazi.

Ushahidi wake uliungwa mkono na mashahidi wengine waliokuwepo siku hiyo lakini pia maelezo ya onyo ya mshtakiwa nayo ni ushahidi wa kesi hiyo.

Jaji alisema katika maelezo hayo, mshtakiwa alikiri kwamba usiku wa siku ya tukio alilala na marehemu chumbani kwake na alishiriki naye ngono usiku huo.

“Alisema kuwa baada ya kitendo hicho, marehemu alionekana kupoteza fahamu, kisha yeye akatoka nje ya nyumba karibu saa 02:00 usiku akimuacha katika hali hiyo bila kumtaarifu ndugu yeyote au kutafuta msaada,”alisema Jaji Mwanga.

“Kwa maoni yangu, kukiri huko kunamtia hatiani sana. Ingawa mshtakiwa hakukiri wazi kuwa alimnyonga marehemu, taarifa hiyo inamweka sawa katikati ya matukio kabla ya kifo cha marehemu,”alieleza Jaji Mwanga katika hukumu hiyo.

Kutokana na ushahidi uliotolewa dhidi yake, Jaji Mwanga alisema upande wa mashtaka ulithibitisha shtaka hilo pasipo kuacha mashaka kuwa mshtakiwa ndiye aliyefanya mauaji na hivyo anastahili adhabu ya kifo.

Tukio la mauaji Masasi

Tukio la mauaji ya Shoo au Mangi lilitokea Oktoba 11,2024 huko kijiji cha Maparawe Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara ambapo mshtakiwa Juma au Fundi J, alipomshambulia marehemu kwa panga sehemu mbalimbali za mwili wake.

Siku hiyo asubuhi, marehemu alikuwa amepanga kwenda kwenye shamba lake na njiani alikutana na Baraka Manyoni ambaye naye ana shamba linalotazamana na la kwake, hivyo wakaongoza pamoja kuelekea yalipo mashamba yao.

Ghafla wakiwa njiani, alitokea mshtakiwa akiwa na kuanza kumkata kata kwa panga Shoo kwa madai kuwa ana uhusiano wa kimapenzi na mkewe.

Kutokana na mshtuko aliupata, Baraka Manyoni alifanikiwa kutoroka eneo hilo na kumwacha rafiki yake na wakati huohuo mshtakiwa naye alitoroka eneo hilo.

Shoo alipata msaada wa Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) na kupelekwa hospitali alikolazwa wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 11 lakini alifariki hospitali hapo Oktoba 22,2024.

Hata hivyo, siku ya tukio saa 3:00 usiku, mshtakiwa huyo alitiwa mbaroni na polisi na kuandika maelezo ya ungamo, ingawa aliyakana mahakamani kuwa alilazimishwa kuyaandika na alikuwa hafahamu maudhui ya nyaraka hiyo.

Hukumu ya Jaji Kakolaki

Jaji Kakolaki katika hukumu yake, alichambua kwa ujumla wake ushahidi wa upande wa mashtaka na kunukuu maelezo ya ungamo ya mshitakiwa.

Katika maelezo hayo anasema “Tarehe 11.10.2024 majira ya saa 12:00 asubuhi nilitoka nyumbani  na kubeba panga moja lenye mshikio wa mbao na kuelekea mashambani huko Maparawe kuandaa shamba langu kwa ajili ya kilimo”

“Nilifanya shughuli za shambani na ilipofika saa 01:00 asubuhi nikiwa njiani naelekea nyumbani ndipo nilipokutana na mtu ambaye ninamtambua kwa jina la Frank au Mangi akiwa na mwenzake ambaye simfahamu kwa jina.”

“Ila kwa kuwa nilikuwa muda mrefu namhisi huyo Mangi ana mahusiano ya kimapenzi na mke wangu japo sina ushahidi wa jambo hilo na ndipo nilipochukua uamuzi wa kumkata kata na panga huyo Mangi maeneo ya kichwani kwake na maeneo ya shavuni na alianguka chini akiwa anatokwa na damu nyingi na kwa wakati huo yule mwenzake alikimbia na ndipo na mimi nilikimbia,” alisema.

Jaji alisema ushahidi huo na ushahidi mwingine kwa ujumla wake, umeithibitishia Mahakama kuwa mshtakiwa alitekeleza mauaji hayo hivyo anamtia hatiani kwa kosa la kuua kwa kukusudia kinyume cha sheria na kumhukumu adhabu ya kifo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *