Tanga. Kwa zaidi ya siku 10 tangu Mei 22, 2026, maisha ya wakazi wa Kitongoji cha Bago Kwakisokwe, Kijiji cha Masakangoto, Kata ya Kigombe, Muheza mkoania Tanga yamegeuka simulizi la majonzi, hofu na sintofahamu baada ya nyumba zao 67 kubomolewa na kuwaacha bila makazi.
Wengi wao wanaishi chini ya miti na maturubai, wakikabiliana na jua kali la mchana na mvua za usiku wakisubiri kujua hatima ya maisha yao.
Kila kunapokucha, familia hizo huamka chini ya vivuli vya miti walikogeuza makazi ya muda.
Wakazi wa Kitongoji cha Bago Kwakisokwe katika Kijiji cha Masakangoto, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga wakiwa kwenye maisha mapya baada ya nyumba zao kubomolewa.
Watoto hukaa pembeni ya wazazi wao huku baadhi yao wakikosa hata nafasi ya kucheza au kujifunza kutokana na mazingira magumu yanayowazunguka.
Usiku unapowadia, hofu ya baridi, nyoka na wadudu kutoka kwenye vichaka vinavyozunguka eneo hilo huwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Mbali na kupoteza makazi, wananchi hao wanasema wameathirika kwa kiasi kikubwa baada ya chakula, samani na mali nyingine kuharibiwa au kupotea wakati wa ubomoaji.
Baadhi yao wanadai walipoteza akiba ya chakula waliyohifadhi kwa matumizi ya familia, fedha na mali walizokuwa wamezitunza ndani ya nyumba zao.
Mmmoja wao, Herman Makwara amesema walipewa eneo hilo na serikali ya kijiji mwaka 2009 na kuanza kujenga makazi yao kwa matumaini ya kuanzisha maisha mapya.
Hata hivyo, mwaka mmoja baadaye walikumbwa na mgogoro wa ardhi uliowafikisha mahakamani baada ya kudaiwa kuvamia eneo linalomilikiwa na kampuni ya Amboni Plantation.
Makazi ya wakazi wa Kitongoji cha Bago Kwakisokwe katika Kijiji cha Masakangoto, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga yaliyobomolewa na kusababisha kukosa mahala pa kuishi. Picha na Mbonea Herman
Makwara anasema baada ya kijiji kushindwa kesi hiyo, wananchi waliendelea kuwasiliana na viongozi wa kijiji wakitaka kufidiwa gharama walizotumia kujenga nyumba zao.
Hata hivyo, kabla ya kupata suluhisho, walikumbwa na taarifa za kushtukiza kwamba nyumba zao zilikuwa zinabomolewa wakati wengi wao wakiwa mashambani.
“Tuliporudi tulikuta nyumba zimebomolewa na mali zetu zimeharibika. Tulikuwa na chakula, mahindi, unga na vitu vingine muhimu kwa ajili ya familia zetu. Leo hii hatuna pa kuishi wala hatujui tuanze upya vipi,” anasema Makwara.
Kwa upande wake, Jane Sigalo anasema alirejea kutoka shambani na kukuta nyumba yake tayari imebomolewa. Anasema tukio hilo lilimwacha katika hali ya mshtuko mkubwa kiasi cha kuzimia alipofika eneo la nyumba yake.
“Nilipoona nyumba yangu imeanguka nilihisi dunia imesimama. Hapo ndipo nilipokuwa ninaishi na watoto wangu. Hadi leo sijui nitawaweka wapi. Tulikuwa na vitu vyetu ndani, lakini hatukuruhusiwa kuingia kuviokoa,” anasema Sigalo akionyesha vifusi na kububujikwa na machozi.
Naye Maria Daudi anasema athari za ubomoaji huo zimewafikia zaidi watoto ambao sasa wanaishi katika mazingira yasiyofaa kwa ukuaji na elimu yao. Anaeleza baadhi ya watoto wanaojiandaa kufanya mitihani ya kitaifa hawana sehemu ya kusomea wala kufanya maandalizi ya masomo yao.
“Mtoto wangu wa kidato cha nne anarudi kutoka shule na kubadilishia nguo chini ya mti. Hana sehemu ya kujisomea wala mazingira ya kumsaidia kujiandaa na mitihani. Hali hii imewaathiri sana watoto wetu kisaikolojia,” anasema.
Makazi ya wakazi wa Kitongoji cha Bago Kwakisokwe katika Kijiji cha Masakangoto, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga yaliyobomolewa na kusababisha kukosa mahala pa kuishi. Picha na Mbonea Herman
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Bago, Dora Gambo, anasema wananchi wengi wanadai kupoteza fedha na mali zao wakati wa ubomoaji huo.
Anadai baadhi ya vitu vilitoweka wakati wa ubomoaji, huku wananchi wengi wakikosa nafasi ya kuokoa mali zao kutokana na kasi ambayo shughuli hiyo ilifanyika.
Kwa mujibu wa Gambo, wengi wa wakazi wa eneo hilo ni wafanyakazi wa muda mrefu wa mashamba ya mkonge ambao wameishi hapo kwa miaka mingi wakijenga familia zao na kuendesha shughuli za kujipatia kipato.
Kutokana na hali hiyo, kuondolewa kwao ghafla katika eneo hilo kumeathiri kwa kiasi kikubwa maisha yao ya kijamii na kiuchumi.
Alichokisema RC
Kutokana na malalamiko ya wananchi hao, Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian ameunda timu maalumu kuchunguza mchakato mzima wa kuwaondoa wakazi hao.
Amesema Serikali inaunga mkono utekelezaji wa uamuzi wa mahakama, lakini wasiwasi wake ni namna shughuli hiyo ilivyotekelezwa bila ushirikishwaji wa baadhi ya mamlaka muhimu za Serikali na vyombo vya usalama.
Wakazi wa Kitongoji cha Bago Kwakisokwe katika Kijiji cha Masakangoto, Kata ya Kigombe wilayani Muheza mkoani Tanga wakiwa kwenye maisha mapya baada ya nyumba zao kubomolewa
Dk Buriani anasema taarifa za wazee kukutwa ndani ya nyumba zilizokuwa zikibomolewa pamoja na kukosekana kwa maandalizi ya kutosha kwa ajili ya kuwahamisha wananchi hao, ni miongoni mwa mambo yatakayofanyiwa uchunguzi.
Pia ameagiza kuangaliwa kwa karibu ustawi wa watoto walioathirika ili kuhakikisha haki yao ya kupata elimu haiathiriki.
Kwa sasa, matumaini yao yameelekezwa kwa Serikali na timu ya uchunguzi iliyoundwa kubaini ukweli wa kilichotokea na kutafuta njia ya kurejesha hadhi, usalama na matumaini ya maisha yao ya baadaye.