Katika kaya nyingi nchini, kuna janga linalotokota jikoni kila kukicha. Hii ni kutokana kwamba, kwa miongo kadhaa, maandalizi ya chakula yamekuwa yakihusishwa na harufu nzito ya moshi wa mkaa na adha ya kupuliza moto wa kuni, jambo ambalo limeonekana kama desturi ya kawaida ya maisha, lakini takwimu zinaonyesha hali ya kutisha.
Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), Tanzania inakabiliwa na changamoto ya afya ya jamii ambapo takriban watu 33,000 hufariki kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa upumuaji yan-ayosababishwa na kuvuta moshi wa nishati isiyo safi.
Licha ya changamoto hizi hizi, utegemezi wa kuni na mkaa bado ni mkubwa, huku zaidi ya asilimia 80 ya kaya zikitumia nishati hizi zisizo na tija. Mbali na athari za kiafya, mzigo wa kiuchumi na kijamii ni mzito, hasa kwa wanawake na watoto ambao ndiyo wahusika wakuu wa maandalizi ya chakula katika familia nyingi.
Muda ambao kundi hili unayatumia katika kutafuta kuni au kusimamia jiko la mkaa ni muda ambao ungetumika katika masuala ya elimu, kazi za uzalishaji mali na mapumziko. Hata hivyo, sasa kuna mabadiliko makubwa yanayochochewa na mifumo bunifu ya kifedha inayomfikia mwananchi wa kawaida.
Kikwazo cha matumizi ya nishati safi
Suluhisho la janga hili lipo katika nishati ya kisasa ya umeme, hususan matumizi ya majiko ya umeme (Electric Pressure Cookers, EPCs)), ambayo yana uwezo wa kupunguza muda wa kupika kwa asilimia 70, kuondoa moshi na kupunguza gharama za nishati.
Kikwazo kikuu imekuwa ni gharama za kununulia vifaa hivyo, ambapo jiko moja la EPC hugharimu kati ya Sh 150,000 hadi Sh 200,000, kiasi ambacho ni kikubwa kwa familia zenye kipato cha kawaida.
Hivyo basi bila kuwepo kwa njia mbadala za kuhakikisha vifaa hivi vinapatikana kwa urahisi, ndoto ya kuhakikisha asilimia 80 ya kaya zinatumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2030, itabaki kuwa kwenye makaratasi kwa Watanzania wengi.
Mapinduzi ya kifedha kupi-tia SACCOS
Ili kuondoa pengo hili, shirika la SNV Tanzania, kupitia programu ya Energising Development (EnDev), limeanzisha mfumo wa upatikanaji wa mikopo nafuu (RLF). Tofauti na mikopo ya benki ambayo huwatisha au kutowafikia wananchi wa vijijini, mfumo huu unatumia mitandao ya Vyama vya Akiba na Mikopo (SACCOS) ambayo tayari inaaminika.
Kupitia mfumo huu, SNV hutoa mtaji wa awali wa majiko 15 kwa kila SACCOS (kwa sasa zipo tisa) na wanachama wenye sifa hukopa majiko hayo. Masharti ya mkopo huu ni rafiki ambapo riba ya asilimia 7 tu na marejesho ya miezi mitatu hadi minne.
Kadiri mikopo inavyorejeshwa, fedha hizo hununua majiko mapya, na hivyo kutengeneza mzunguko endelevu ambapo SACCOS inakuwa mtoa huduma wa nishati safi. Mafanikio ya mpango huu yanaonekana kupitia maisha ya watu kama Godfrey Lema, mhasibu kutoka mkoani Morogoro anayeishi na mdogo wake ambaye ni mwanachuo.
Kabla ya kupata jiko kupitia Elimu SACCOS, walikuwa wakitumia kati ya Sh 1,200 na Sh 2,000 kwa ajili ya kununua mkaa kila wanapotaka kupika. “Mara ya kwanza nilipopika nyama kwa dakika 25, sikuamini,” anasema Lema, ambaye sasa anatumia muda aliookoa kutokana na matumizi ya jiko la EPC kwa ajili ya kazi na masomo. Kwa upande wake fundi cherehani na mama wa watoto saba, Happiness Sha-yo anasema ameshuhudia mabadiliko makubwa zaidi.
Mama huyo alikuwa akitumia Sh 45,000 kwa mwezi kwa ajili ya kununulia mkaa, jambo lililomchosha na kumzuia kufanya kazi yake ya ushonaji vyema. Baada ya kupata jiko la EPC kwa mkopo, gharama yake ya nishati imeshuka hadi Sh 20,000 kwa mwezi, huku akiokoa Sh 25,000 ambazo sasa zinasaidia biashara yake ya ushonaji.
Mfanyabiashara wa chakula kutoka Iringa, Saida Kisinda akipiga hesabu za biashara yake ambayo sasa imekuwa mara mbili. Kupitia mkopo wa jiko la umeme kutoka programu ya EnDev na SNV Tanzania, Saida ameweza kuongeza mapato na kuimarisha afya yake kwa kuacha kutumia mkaa.
Hata wafanyabiashara kama Catherine Msigwa, muuza maharage na makongoro, amefaidika baada ya mpenzi wake kumchukulia mkopo wa jiko hilo. Sasa anaweza kupika vyakula huku akihudumia wateja, jambo lililoongeza tija ya biashara yake mara mbili, huku matatizo ya kikohozi na macho kuwasha kutokana na moshi wa kuni yakitoweka kabisa.
Hadithi hizi, kutoka kwa vijana na wanawake wajasiriamali hadi wafanyabiasha-ra wadogo, zinaonyesha kuwa; kuondoa vikwazo vya kifedha kunafungua fursa nyingi. Hivi sasa kaya zinaokoa kati ya asilimia 50–70 ya gharama za nishati ya kupikia, kupata muda wa saa 2–4 za ziada kila siku, huepuka magonjwa yanayotokana na moshi wa kupikia na hutumia muda wanaookoa kujiongezea kipato.
Kwa pamoja, manufaa haya yameimarisha ustahimilivu wa kaya, kukuza usawa wa kijinsia na kuchangia ukuaji wa uchumi. Mfumo huu wa RLF umekuwa kutoka kuhudumia SACCOS tatu pekee katikati ya mwaka 2023 hadi kufikia SACCOS tisa kufikia Februari 2024, huku majiko 2,489 yakiwa yameshatolewa kwa mkopo.
Ili kuondoa hofu ya wana-nchi, mafunzo ya vitendo hufanyika kuonyesha kuwa kupika mlo mmoja kwa EPC hugharimu Sh 150 hadi Sh 250 tu, ikilinganishwa na Sh 1,200 hadi Sh 2,000 za mkaa. RLF imeonyesha kuwa uwepo wa huduma rahisi za kifedha kunaweza kuharakisha safari ya kufikia malengo ya ajenda ya matumizi ya nishati safi za kupikia kwa kiwango kikubwa.
Kwa kuunganisha mikopo ndani ya taasisi za kijamii, mfumo huu umewezesha viwango vya juu vya urejeshaji wa mikopo, uendelevu wa shughuli za mifuko na kuzalisha manufaa zaidi; kila mkopo unaorejeshwa unawezesha ufadhili wa kifaa kingine na kwa mtu mwengine. Hata hivyo, utekelezaji wake umekumbana na changamoto kadhaa.
Baadhi ya SACCOS zilikuwa na mifumo dhaifu ya usimamizi, jambo lililochelewesha mzunguko wa fedha za mfuko na kufanya maamuzi kuchukua muda mrefu.
Vilevile, baadhi ya wanachama walikuwa na wasiwasi wa kuchukua mikopo kwa ajili ya vifaa vya kupikia kwa umeme, hususan katika maeneo yenye changamoto ya umeme, kwa kuhofia ongezeko la gharama za umeme. Hali hii ilichangia kiwango cha chini cha matumizi ya mikopo hiyo.
Aidha, baadhi ya SACCOS ziliona usimamizi wa mikopo mingi ni mzigo wa kiutawala. Mradi huu unasisitiza kuwa safari ya kuelekea matumizi ya nishati safi za kupikia haihitaji tu msaada wa kiufundi au kifedha, bali pia mabadiliko ya kijamii na kitabia.
Kuridhika kwa watumiaji kupitia maonyesho ya moja kwa moja ya upishi pamoja na manufaa ya kiuchumi yaliyoonekana wazi vilichangia kwa kiasi kikubwa kudumisha mahitaji ya teknolojia hizi.
Hii inaashiria kwamba hatua za baadaye zinapaswa kuendelea kuunganisha huduma za kifedha, kuimarisha uwezo wa taasisi na mikakati ya kuhamasisha mabadiliko ya tabia ili kuhakikisha mafanikio endelevu. Programu ya EnDev, inayofadhiliwa na wadau mbalimbali imeweka msingi unaoweza kuungwa mkono na kuendelea kukuwa.
Hii ni fursa kwa wawekezaji na taasisi za kifedha kusaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan Usawa wa Kijinsia (SDG 5), Nishati Safi (SDG 7), na Kazi Zenye Staha (SDG 8). Upatikanaji wa fedha si msamiati wa kibenki tu bali ni kichocheo kinachookoa afya, muda na kukuza uchumi wa Watanzania.
Taifa linaposonga mbele, mabadiliko kutoka kwenye mkaa kwenda kwenye umeme ni ushahidi wa kile kinachowezekana wakati mifumo bunifu ya fedha inapokutana na imani ya jamii.
Programu ya EnDev inafadhiliwa kwa ushirikiano wa wafadhili mbalimbali wakiwemo; Shirika la Maendeleo la Ujerumani, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, Norad na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SDC), UKAid, Shirika la Misaada la Australia na Sweden