Dar es Salaam. Katika tasnia ya muziki wapo watu wanaofanya kazi nyuma ya pazia. Wakipanga na kupambana kuhakikisha jina la msanii linapenya kwenye masoko makubwa ya muziki.
Kwa upande wa msanii kutoka Afrika Kusini Tyla, safari yake ya mafanikio kimataifa inaonekana kuwa nyepesi. Hii ni kutokana na kuwepo kwa watu wenye akili ya kipekee ambao wameweza kusoma upepo wa burudani duniani.
Tangu Tyla alipoachia wimbo wake Water, ambao ulifanya vizuri kimataifa na kumfanya atambulike zaidi dunia, amekuwa akionekana katika matukio makubwa ikiwemo Met Gala, Grammy Awards na MTV Awards, majukwaa ambayo mara nyingi huwakutanisha mastaa wakongwe na wapya wanaotikisa kwenye gemu ya muziki.
Kinachowashangaza wengi ni kuwa kila hatua ya Tyla inapangwa kwa wakati sahihi. Ambapo kwa takribani miaka mitano kila event kubwa inakayofanyika nchini Marekani msanii huyo lazima awepo na jina lake lazima litajwe kuanzia kwenye red carpet kubwa, matamasha ya mitindo hadi kumwaga wino katika mikataba ya muziki inayomuweka karibu zaidi na wasanii wakubwa wa Marekani.
Sasa macho yameelekezwa katika Kombe la Dunia 2026. Ambapo Marekani ndio mwenyeji huku kukiwa na tetesi kuwa anaandaliwa kwa ajili ya kutumbuiza kwenye ufunguzi wa michua hiyo tukio ambalo litaendelea kuliweka jina lake katika nafasi nzuri.
Zaidi ya hapo, ameachia wimbo rasmi wa ‘Game Time’ wa Kombe la Dunia aliyomshirikisha rapa kutoka Marekani Future unaoendelea kutikisa katika mitandao ya kijamii.
Aidha baadhi ya wadau mbalimbali wamekua wakitoa maoni yako wakieleza kuwa mafanikio hayo ya Tyla si ya bahati mbaya. Bali ni kutokana na kuwepo kwa timu nzuri iliyokamilika na yenye malengo ya kumfikisha msanii huyo sehemu kubwa.
Huku wakitoa ushauri kwa mastaa wengine kuchagua timu bora na yenye jicho la maono katika game ya muziki duniani.
Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali nyuma ya Tyla upo mtandao mkubwa unaomuwezesha kupata mafanikio zaidi ikiwemo Lebo ya Fax Records (Afrika Kusini), Epic Records chini ya Sony Music Entertainment kampuni ambayo inasimamia usambazaji wa muziki wake kimataifa, mikataba na kuhakikisha anafika kwenye masoko makubwa ya muziki Marekani. Lakini pia timu yake ya management na PR.
Tangu atambulike kupitia ‘Water’ amechia ngoma nyingine mbalimbali ikiwemo Jump, Truth or Dare, ART, Girl Next Door aliyomshirikisha Ayra Starr, Been Thinking, Safer na nyinginezo. Huku akiachia albamu moja aliyoipa jina lake Tyla iliyobeba nyimbo 12.
Ameshinda tuzo kubwa ikiwemo Grammy 2024 na 2026 kupitia wimbo wa Water na Push 2 Start MTV Video Music Awards (VMAs) 2024 alishinda katika kipengele cha Best Afrobeats wimbo wa Water, BET Awards, MTV Europe Music Awards (EMAs) na nyinginezo.