Iringa. Kwa miaka mingi, wakazi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa waliishi katika changamoto ya usafiri kutokana na ubovu wa barabara ya vumbi iliyounganisha maeneo mbalimbali wilayani humo mpaka kufika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, hali iliyosababisha safari kuwa ndefu, gharama za usafirishaji kupanda na wakati mwingine mazao ya wakulima kuharibika kabla ya kufika sokoni.

Wakulima ndio mamlaka ya moja kwa moja ya ushuhuda wa mabadiliko ya kiuchumi yaliyotokea baada ya ujenzi wa barabara ya Ipogolo–Kilolo, wakieleza kuwa mradi huo umebadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yao, uzalishaji na hata namna wanavyopanga kilimo chao.

Kwa miaka mingi, Kilolo ilikuwa miongoni mwa maeneo yaliyotegemea zaidi kilimo cha mazao ya chakula na biashara kama mahindi, viazi, mbogamboga na matunda, lakini changamoto ya barabara ilifanya sekta hiyo isitoe matokeo yanayolingana na uwezo wa eneo hilo na Wakulima walilazimika kuuza mazao yao kwa hasara kutokana na kuchelewa kufika sokoni na gharama kubwa za usafirishaji.

Wakizungumza na Mwananchi, wakulima hao wamesema wakati wa mvua, hali ilikuwa mbaya zaidi ambapo barabara ya vumbi iligeuka tope, magari yalikwama na baadhi ya safari zilighairishwa kabisa, jambo lililosababisha mazao kuoza mashambani au kushuka thamani sokoni.

Muonekano wa barabara ya kutoka Ipogolo -Kilolo mkoani Iringa iyojengwa kwa lami na Wakulima wanasafirisha mazao yao bila changamoto. Picha na Ofisi ya Wizara ya Ujenzi

“Zamani tulikuwa tunapata shida sana. Wakati wa mvua magari yalikwama, mazao yalichelewa kufika sokoni na mara nyingi tulipata hasara kubwa sana,” amesema mkulima Michael Singaeli na kuongeza.

“Kwa kweli tulikuwa tunafanya kazi kwa hasara bila kujua na unavuna mazao mengi lakini mwisho wa siku faida ni ndogo sana kwa sababu ya usafiri,” ameongeza.

Hata hivyo Wakulima hao wamesema hali hiyo sasa imekuwa historia baada ya Serikali kukamilisha ujenzi wa barabara ya Ipogolo–Kilolo yenye urefu wa kilomita 33.61 kwa kiwango cha lami kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kwa gharama ya takribani Sh 60.4 bilioni, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kuboresha miundombinu vijijini na kuimarisha uchumi wa wakulima.

“Sasa hali imebadilika kabisa. Tunafika sokoni haraka, mazao hayaharibiki na tunapata bei nzuri zaidi kuliko zamani,” alisema Ezekiel Kisoma.

Naye Asha Mboya Mkulima kutoka Wilayani Kilolo alisema

“Kilimo chetu sasa kina thamani. Hata wafanyabiashara wanakuja moja kwa moja mashambani kununua mazao,”

Wakulima hao pia wamesema mabadiliko hayo yameongeza mzunguko wa biashara kati ya Kilolo na Iringa Mjini, ambapo sasa bidhaa zinafika sokoni kwa haraka zaidi na kwa ubora unaotakiwa, hali inayoongeza ushindani na bei nzuri kwa mkulima.

Muonekano wa barabara ya kutoka Ipogolo -Kilolo mkoani Iringa iyojengwa kwa lami na Wakulima wanasafirisha mazao yao bila changamoto. Picha na Ofisi ya Wizara ya Ujenzi

“Gharama za usafirishaji zimepungua sana.  Zamani tulilipa pesa nyingi sana kusafirisha mzigo mmoja, sasa ni nafuu na wakati mfupi,” amesema Juma Mkwawa.

Aidha, wamesema huduma za kijamii kama afya, elimu na usafiri wa dharura zimeimarika kwa kiasi kikubwa, kwani sasa kufika hospitali au vituo vya huduma ni rahisi zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kwa sasa tunaweza kupanga kilimo chetu vizuri kwa sababu usafiri si tatizo tena na hii imetupa matumaini ya kuongeza uzalishaji,” alisema Rehema Lusekelo.

Nao Madereva wa malori ya mizigo wanaosafirisha mazao kutoka Wilaya ya Kilolo kwenda maeneo mbalimbali nchini wamesema ujenzi wa barabara hiyo umepunguza kwa kiasi kikubwa muda wa safari na gharama za uendeshaji, huku ukirahisisha usafirishaji wa mazao kufika sokoni kwa wakati na bila hasara.

“Ngoja tuseme ukweli, zamani tulikuwa tunapata changamoto kubwa sana hapa Kilolo, lakini sasa barabara ni nzuri, safari ni haraka na mizigo inafika salama bila kuchelewa wala kuharibika,” alisema Aidan Msolwa mmoja wa madereva wa lori la mizigo.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba alipotembelea na kukagua mradi huo, alieleza kuridhishwa na ubora wa ujenzi huo akisisitiza kuwa barabara ni kichocheo kikuu cha uchumi wa wananchi wa vijijini.

Muonekano wa barabara ya kutoka Ipogolo -Kilolo mkoani Iringa iyojengwa kwa lami na Wakulima wanasafirisha mazao yao bila changamoto. Picha na Ofisi ya Wizara ya Ujenzi

“Barabara ya Ipogolo-Kilolo ni nyenzo muhimu ya kukuza uchumi wa wakulima. Itapunguza gharama za usafirishaji na kuhakikisha mazao yanafika sokoni kwa wakati,” alisema Dk Nchemba.

Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya alisema kuwa ujenzi wa barabara ya Ipogolo–Kilolo unalenga moja kwa moja kukuza uchumi wa wananchi kwa kuboresha miundombinu ya usafirishaji, kupunguza gharama za uchukuzi wa mazao na kurahisisha upatikanaji wa masoko.

Kasekenya alisema kuwa Serikali imewekeza katika barabara hiyo kwa lengo la kuhakikisha wakulima wananufaika na kazi zao kwa kupata thamani halisi ya mazao yao, sambamba na kuchochea shughuli za kiuchumi katika Wilaya ya Kilolo na maeneo ya jirani.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Tanroads, Mkoa wa Iringa, Hosea Machaka, alisema mradi huo umejumuisha ujenzi wa madaraja, makalavati na mifumo ya maji ya mvua ili kuhakikisha uimara wa barabara hiyo mwaka mzima.

Muonekano wa barabara ya kutoka Ipogolo -Kilolo mkoani Iringa iyojengwa kwa lami na Wakulima wanasafirisha mazao yao bila changamoto. Picha na Ofisi ya Wizara ya Ujenzi

“Tumefanya ujenzi kwa viwango vya kisasa na barabara hii sasa iko tayari na ina uwezo wa kudumu kwa muda mrefu bila changamoto kubwa za uharibifu,” alisema Machaka.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema mradi huo umefungua mnyororo mzima wa maendeleo, kuanzia kilimo, biashara hadi huduma za kijamii.

“Kilolo sasa si Kilolo ya zamani na eneo linalokua kwa kasi kiuchumi kwa sababu ya miundombinu bora ya barabara,” alisema RC James.

Mbunge wa Kilolo, Ritta Kabati, alisema mradi huo ni ushahidi wa moja kwa moja wa jinsi uwekezaji wa serikali unavyogusa maisha ya wananchi.

“Hii barabara imeleta mabadiliko makubwa sana. Wakulima sasa wana uhakika wa kufikisha mazao yao sokoni bila kupoteza thamani,” alisema Mbunge Kabati.

Wachambuzi wa maendeleo ya vijijini wanasema mradi wa barabara ya Ipogolo–Kilolo ni mfano halisi wa jinsi miundombinu inavyoweza kubadilisha uchumi wa eneo, hasa kwa kuondoa vikwazo vya msingi vinavyokwamisha uzalishaji wa kilimo.

Kwa mujibu wa wataalamu hao, barabara hiyo imefungua fursa mpya za uwekezaji, kuongeza thamani ya ardhi, na kuchochea uanzishwaji wa shughuli za kibiashara pembezoni mwa barabara.

Kwa ujumla, mradi huo sasa unatajwa kuwa miongoni mwa miradi ya kimkakati iliyobadilisha moja kwa moja maisha ya wananchi wa Mkoa wa Iringa, ukibeba matumaini mapya ya uchumi imara unaotegemea kilimo chenye tija na miundombinu bora.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *