
Dodoma. Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ameagizwa kuwashughulikia waajiri waliosababisha watumishi kukosa haki zao kutokana na utendaji wao na kusababisha baadhi wasipandishwe vyeo.
Agizo hilo limetolewa leo Jumatano Juni 3,2026 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Qwaray wakati akifunga kikao kazi cha Maofisa Utawala na Rasilimali Watu kutoka wizara, taasisi za umma, mashirika ya umma, sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kilichofanyika jijini Dodoma.
Amesema Serikali imebaini wapo baadhi ya watumishi wamekosa maendeleo ya kiutumishi si kwa sababu ya kushindwa kutekeleza majukumu yao, bali wamesababishwa na uzembe wa wasimamizi wao.
Qwaray amemwagiza Katibu Mkuu wa Utumishi kushirikiana na waajiri wote nchini kuwabaini wasimamizi hao na kuwachukulia hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, ikiwemo kuwaondoa katika nafasi za uongozi pale itakapobainika walishindwa kutekeleza wajibu wao bila sababu za msingi.
“Baadhi ya watumishi walikosa fursa za kupandishwa vyeo kwa sababu ya uzembe wa wasimamizi wao na si kwa makosa yao wenyewe, hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe ili kurekebisha dosari hizo na kuhakikisha haki inatendeka na jambo linahitaji majibu ya haraka,” amesema Qwaray.
Amemwelekeza Katibu Mkuu kuwapatia unafuu wa masharti watumishi walioathirika ili wasiathirike katika maendeleo yao ya kiutumishi kutokana na uzembe wa wasimamizi wao.
Amesema Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu mifumo ya upimaji wa utendaji kazi ili kuhakikisha kila mtumishi anapimwa kwa haki na kwa mujibu wa malengo ya kazi aliyopewa.
Kwa upande mwingine amewataka waajiri kuhakikisha watumishi wanalipwa stahiki zao kwa wakati ikiwemo gharama za uhamisho, nauli za likizo na mafao mengine, akisema ucheleweshaji wa malipo hayo huathiri ari ya kazi na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi amesema utawala na usimamizi wa rasilimali watu katika utumishi wa umma umeendelea kuimarika huku changamoto zikijadiliwa na kutafutiwa ufumbuzi kupitia kikao hicho.
Kuhusu maagizo ya Naibu Waziri amesema watayafanyia kazi na mrejesho utapatikana kwa wakati huku akiwahakikishia watumishi hakuna haki itakayopotea.