Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema ziara yake ya kitaifa nchini Russia ni ya umuhimu mkubwa kwa Tanzania, akieleza inafungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano wa kihistoria uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumatano, Juni 3, 2026 baada ya kupokewa Ikulu ya Kremlin jijini Moscow na mwenyeji wake, Rais Vladimir Putin, hafla rasmi iliyohudhuriwa na viongozi waandamizi kutoka Tanzania na Russia.
Rais Samia amewasili Ikulu ya Kremlin saa tisa alasiri kwa saa za Afrika Mashariki, akiwa ameambatana na ujumbe wa viongozi mbalimbali wa Serikali ya Tanzania wanaoshiriki ziara hiyo ya kitaifa inayotarajiwa kuvutia fursa za kibiashara na uwekezaji nchini.
Rais wa Rusia, Vladimir Putin akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow.
Akizungumza baada ya mapokezi hayo, Rais Samia amemshukuru Rais Putin na Serikali ya Russia kwa mapokezi mazuri na ukarimu aliopatiwa yeye pamoja na ujumbe wake, huku akisisitiza Tanzania inathamini mchango wa Russian katika safari yake ya maendeleo tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa haya.
“Kwa niaba yangu na watu wa Tanzania natoa shukrani za dhati kwa mwaliko huu. Naishukuru Russian kwa mchango wake katika harakati za kupigania uhuru wa Afrika. Tumekuwa tukishirikiana na Russia kwa muda mrefu katika maeneo mengi, maendeleo tunayoyazungumzia nchini kwetu leo, Russia ina mchango mkubwa sana,” amesema Rais Samia.
Rais huyo pia amekumbusha uhusiano wa Tanzania na Russia una mizizi ya kihistoria iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere na kuendelea kuimarika katika vipindi mbalimbali vya uongozi wa nchi hizi mbili.
Akitaja uzito wa safari yake hiyo, Rais Samia amesema ziara hiyo ni ya kipekee kwa Tanzania kutokana na muda mrefu uliopita tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kitaifa ya Rais wa Tanzania nchini Russia.
“Ziara hii ni ya umuhimu mkubwa kwa Taifa letu. Ni zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya kitaifa ya Rais wa Tanzania nchini Russia, baada ya ziara iliyofanywa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1969,” amesema.
Katika mazungumzo hayo, Rais Samia pia amempongeza Rais Putin akimtaja kama kiongozi mzalendo kwa namna anavyoiongoza Russia na kuendeleza masilahi ya wananchi wake.
Alichokisema Putin
Rais Putin amesema uamuzi wa Rais Samia kuifanya Moscow kuwa kituo cha ziara yake ya kwanza ya kiserikali baada ya kuapishwa tena kuwa Rais Novemba mwaka jana, ni ishara thabiti ya dhamira ya Tanzania kuimarisha zaidi uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Rais wa Rusia, Vladimir Putin akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Ikulu ya Kremlin jijini Moscow.
Akimkaribisha Rais Samia katika Ikulu ya Kremlin, Rais Putin amesema ziara hiyo ina umuhimu wa kipekee wakati Tanzania na Russia zikijiandaa kuadhimisha miaka 65 ya uhusiano wa kidiplomasia mwaka huu.
“Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba baada ya kuapishwa kwako, umeichagua Russia kuwa nchi ya kwanza ya kigeni kwa ziara yako ya kiserikali. Tunaona hili kama ishara nzuri sana,” amesema Putin.
Amesema Rais Samia amekuwa akiunga mkono maendeleo ya uhusiano wa pande mbili tangu alipokuwa akihudumu katika nafasi mbalimbali serikalini, ikiwemo uwaziri na makamu wa rais.
Katika kipindi hicho, amesema Rais Samia amesaidia kudumisha ushirikiano wa karibu ambao umeendelea kukua kwa kasi na uthabiti.
Putin amesema biashara kati ya Tanzania na Russia imeongezeka kwa asilimia 20 hadi 25 katika mwaka uliopita na akaeleza bado kuna fursa kubwa zaidi za kukuza biashara hiyo.
Amesema Tanzania na Russia zina nafasi ya kupanua ushirikiano katika sekta za kimkakati kama nishati, utafiti wa jiolojia, usafiri, vifaa na usafirishaji, afya na elimu.
Kiongozi huyo wa Russia pia amesisitiza ushirikiano wa karibu katika masuala ya kimataifa, akisema nchi hizo mbili zimeendelea kuungana mkono na kudumisha mazungumzo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya dunia.
Atembelea makaburi
Mapema kabla ya kufika Kremlin, Rais Samia ametembelea eneo la makaburi ya mashujaa wa Russia waliopoteza maisha wakilitumikia taifa lao, hatua ambayo amesema imeongeza uelewa wake kuhusu historia na uzalendo wa wananchi wa nchi hiyo, akiitaja kama fursa ya heshima aliyopewa nchini humo.
Rais Samia pia ametambulisha kwa Rais Putin ujumbe wa viongozi wa Tanzania alioambatana nao katika ziara hiyo, ambao wanatoka katika sekta nyeti za masuala ya kidiplomasia, uwekekezaji, madini na ulinzi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan akiweka shada la maua katika kaburi la Askari Asiyejulikana (Tomb of the Unknown Soldier) pembezoni mwa Ukuta wa Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow nchini Urusi.
“Katika msafara huu, nipo na Waziri wa Mambo ya Nje, Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Waziri wa Madini, Balozi wa Tanzania nchini Russia na mwakilishi wa Majeshi ya Ulinzi,” amesema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu, Rais Samia akiwa nchini Russian katika ziara hiyo ya siku tano, atafanya mazungumzo rasmi na Rais Putin kuhusu kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.
Pia atashiriki Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF 2026), kukutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa kimataifa, pamoja na kushuhudia utiaji saini wa makubaliano mbalimbali ya ushirikiano yatakayolenga kukuza maendeleo na fursa za kiuchumi kwa mataifa haya mawili.
Mtazamo wa wanazuioni
Akizungumzia mazungumzo hayo, mwanadiplomasia na mwanazuoni Profesa Benson Bana, amesema mahusiano ya mataifa makubwa ni fursa muhimu kwa Tafa akilitaja Taifa hilo kuwa limekuwa na mchango mkubwa kwa Tanzania katika nyanja mbalimbali.
“Rusian ni nchi ambayo tangu mwanzo kabisa haikuwahi kuunga mkono mabeberu, ilikuwa upande wetu Afrika na imetusaidia mambo mengi. Ngoja tuone mpaka mwisho wa ziara hii viongozi wetu watakubaliana mambo gani,” amesema.
Ameongeza Russia ni taifa lenye fursa nyingi ambazo zinahitajika Afrika, akisisitiza kuwa ziara ya Rais Samia inafanyika muda muafaka kwani dunia inapitia mtikisiko wa kisiasa na kiuchumi, hivyo kuimarisha mahusiano na mataifa mengi ni hatua muhimu.
Profesa Mohamed Makame wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (Suza) amesema, umuhimu wa ziara hiyo kwa nchi unabebwa na falsafa ya uchumi ya Rais Samia ambaye anajenga uchumi wa nchi kwa kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na mataifa mengine.
“Uhusiano wa Tanzania na Russia umekuwa imara tangu mwanzo, haujawahi kuteteleka. Ziara hii kwa sasa bila shaka inabeba malengo ya Dira 2050, hivyo kuimarika kwa ushirikiano na Russia kwa kipindi hiki tunaweza kupata fursa za kutimiza malengo yaliyowekwa kwenye Dira kufikia 2050,” amesema.
Amesema Tanzania haiwezi kwenda peke yake ili iweze kufikia malengo ya Dira hiyo akifafanua kuwa kuimarisha mahusiano na Russia kama Taifa kubwa kiteknolojia na kiuchumi ni hatua muhimu itakayosaidia kufiyakia.