Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema uongozi thabiti na wenye maono unahitajika ili kuhakikisha wananchi wa mikoa ya kusini wananufaika moja kwa moja na rasilimali ya gesi asilia iliyopo katika ukanda huo.

Chama hicho kimesema mikoa ya kusini imebarikiwa kuwa na rasilimali nyingi za asili, hususan gesi asilia, ambazo zingeweza kuwaletea maendeleo makubwa wananchi iwapo kungekuwa na mfumo bora wa usimamizi wa rasilimali na Katiba inayolinda masilahi ya umma.

Makamu Mwenyekiti  Chadema Bara, HecheJohn, akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo, Juni 3  2026, Kilwa Kivinje, Mkoa wa Lindi.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara wa operesheni ya katiba mpya na kampeni ya Free Tundu Lissu uliofanyika Kilwa leo Jumatano Juni 3, 2026, Makamu Mwenyekiti wa Chadema Bara, John Heche amesema usimamizi mzuri wa rasilimali unaweza kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

“Kusini mmejaliwa kuwa na gesi yenye futi za ujazo trilioni 54.5. Kukiwa na uongozi bora unaoweza kusimamia mikataba yenye manufaa kwa Taifa, rasilimali hiyo inaweza kuwanufaisha wananchi kwa kiwango kikubwa,” amesema Heche.

Amesema gesi asilia hutumika kuzalisha mbolea kwa ajili ya kilimo, kuzalisha umeme na katika shughuli nyingine nyingi muhimu za maendeleo ya binadamu.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema Mkoa wa Lindi unatekeleza mradi mkubwa wa gesi wenye thamani ya takribani Sh57 trilioni.

Makamu Mwenyekiti  Chadema Bara, HecheJohn, akihutubia wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo, Juni 3  2026, Kilwa Kivinje, Mkoa wa Lindi.

Mnyika amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa zaidi nchini tangu Tanzania ipate uhuru.

“Hata hivyo, bila mikataba bora na usimamizi madhubuti, wananchi hawatanufaika ipasavyo. Inaweza kutokea kama ilivyokuwa Songosongo, ambapo manufaa makubwa yaliwanufaisha watu wengine kuliko wananchi wa maeneo husika,” amedai Mnyika.

Amedai hali hiyo inaweza kujirudia katika miradi mingine ya gesi ya Mtwara ikiwa hakutakuwa na mifumo madhubuti ya kuhakikisha wananchi wanapata sehemu ya manufaa yatokanayo na rasilimali hizo.

“Mageuzi ya kweli yanayolenga kunufaisha wananchi yanahitaji Katiba mpya pamoja na uongozi bora,” ameendelea kudai Mnyika.

Akizungumzia historia ya Kilwa, Mnyika amesema eneo hilo lilianza kustawi tangu karne ya 11 na lilikuwa kitovu muhimu cha biashara na utawala katika Pwani ya Afrika Mashariki.

Makamu Mwenyekiti  Chadema Bara, HecheJohn akiwapokea wanachama wapya waliohamia Chadema kutoka vyama mbalimbali vya siasa katika mkutano wa hadhara uliofanyika leo, Juni 3,  2026, Kilwa Kivinje, Mkoa wa Lindi.

 Amesema hata masultani waliwahi kuwa na makao yao Kilwa Kisiwani, huku Kilwa Masoko ikitumika kama kituo kikubwa cha biashara kilichounganisha maeneo mbalimbali ya ukanda huo.

“Kilwa ina historia ndefu ya ustaarabu na mapambano. Historia hiyo imeendelea kujidhihirisha hata katika maendeleo ya mfumo wa vyama vingi vya siasa nchini,” amesema.

Naye Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Mzee amesema wananchi wa kanda ya kusini wana mchango mkubwa katika historia ya Zanzibar na maendeleo ya kisiasa ya Tanzania.

Akizungumza na wananchi wa Kilwa, amesema kati ya viongozi 14 waliounda Baraza la Kwanza la Mapinduzi Zanzibar chini ya Rais wa kwanza wa Zanzibar, Abeid Amani Karume, mawaziri watano walitoka kanda ya kusini.

“Wananchi wa Kusini, hususan Kilwa mnayo historia kubwa katika kuchangia ukombozi wa Zanzibar kupitia Mapinduzi ya mwaka 1964. Nawaomba muendelee kujiunga na Chadema na kuendeleza ari ya maendeleo na uelewa ambayo imekuwepo katika eneo hili kwa muda mrefu,” amesema.

Said Mzee pia amesema wanawake walitoa mchango mkubwa katika harakati za Mapinduzi ya Zanzibar, hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kuwaunga mkono viongozi wanaopigania haki zao.

Katika maelezo yake, amemtaja aliyekuwa Mbunge wa Kilwa Kusini, Seleman Bungara, maarufu Bwege.

“Umaskini si sifa. Wananchi wa Kilwa mnalima korosho kwa wingi, lakini bado mnakabiliwa na changamoto za kiuchumi. Hali hiyo si ya kawaida, hivyo ni muhimu kuendelea kupigania haki na maendeleo,” amesema.

Amewataka wananchi kutokubali kuwa watumwa wa kisiasa wa chama tawala, akidai kuwa maslahi yao hayapewi kipaumbele cha kutosha.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Belchomas Ponera amesema Mkoa wa Lindi una historia ya kuwa na wananchi wapambanaji.

Amesema kati ya majimbo manane ya uchaguzi yaliyopo mkoani humo, matano yamewahi kushindwa na chama tawala na kuchukuliwa na vyama vya upinzani.

“Kama viongozi, jukumu letu ni kuwaunganisha wananchi ili wawe na sauti moja ya mabadiliko. Tunaamini mabadiliko hayo yanaweza kupatikana kupitia ushiriki mkubwa wa wananchi katika masuala ya kisiasa na maendeleo ya Taifa,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *