Manchester, England. Michael Carrick ameanza kutengeneza bomu jipya Manchester United! Hivyo ndivyo unaweza ukasema baada ya klabu hiyo kufikia makubaliano na Atalanta ya Italia ya kumsajili kiungo wa Brazil, Éderson, kwa ada ya awali ya Euro 40.5 milioni, huku nyota huyo akitajwa kuwa mrithi wa Casemiro.

Makubaliano hayo yanaweza kufikia hadi Euro 45 milioni kutokana na nyongeza mbalimbali zitakazotegemea mafanikio ya mchezaji na klabu.

Ederson (26) tayari amekubaliana masuala binafsi na Manchester United na anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano utakaomalizika Juni 2030, ukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mmoja zaidi.

Hata hivyo, usajili huo umebakisha hatua moja ya staa huyo kufanyiwa vipimo vya afya ili kukamilisha rasmi dili hilo.

Taarifa zinaeleza kuwa Carrick kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Soka wa United, Jason Wilcox, wamemchukua Éderson kama mbadala sahihi wa Casemiro ambaye ameondoka klabuni hapo baada ya mkataba wake kumalizika.

Kiungo huyo anasifika kwa uwezo wake wa kucheza mbele ya mabeki, kukaba, kusoma mchezo na kusaidia mashambulizi kutoka eneo la chini hadi mbele, sifa ambazo Carrick anaamini zitasaidia kuimarisha safu ya kiungo ya United.

Kuwasili kwa Ederson kunaongeza shinikizo kwa Manuel Ugarte ambaye alisajiliwa kutoka Paris Saint-Germain mwaka 2024 kwa Pauni 51 milioni lakini alishindwa kupata nafasi ya kudumu kikosini msimu uliopita. Inaelezwa kuwa United inaweza kumuuza au kumtoa kwa mkopo mchezaji huyo katika dirisha hili la usajili.

Ederson alikuwa mmoja wa viungo waliovutia zaidi katika Ligi ya Italia kwa misimu ya hivi karibuni ambapo alijiunga na Atalanta Januari 2022 akitokea Salernitana baada ya kupitia akademi na timu mbalimbali nchini Brazil zikiwemo Cruzeiro, Corinthians na Fortaleza.

Katika ngazi ya kimataifa, Ederson ameichezea Brazil mara tatu tangu alipoanza kuitumikia timu hiyo mwaka 2024. Mechi yake ya mwisho ilikuwa Machi 2025 katika kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Argentina.

Licha ya kutajwa katika kikosi cha awali cha wachezaji 55 wa Brazil kilichotajwa na kocha Carlo Ancelotti kuelekea Kombe la Dunia, Ederson hakufanikiwa kuingia kwenye kikosi cha mwisho cha mashindano hayo.

Wakati huo huo, Carrick anaendelea kutafuta kiungo mwingine wa kuongezea nguvu eneo ka katikati Man United. Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwamo kwenye orodha ya United ni Aurélien Tchouaméni wa Real Madrid, Carlos Baleba wa Brighton, Adam Wharton wa Crystal Palace, Elliot Anderson wa Nottingham Forest na Sandro Tonali wa Newcastle United.

Hata hivyo, gharama kubwa za wachezaji hao zinaonekana kuwa changamoto, huku Tchouaméni akitajwa kugharimu karibu Pauni 70 milioni, Baleba Pauni 50 milioni, Wharton zaidi ya Pauni 60 milioni na Anderson na Tonali ambao thamani yao inaweza kuzidi Pauni 100 milioni.

Usajili wa Éderson unaonekana kuwa hatua ya kwanza ya Carrick katika kujenga Manchester United mpya yenye ushindani mkubwa baada ya mabadiliko ya benchi la ufundi na kikosi kuelekea msimu wa 2026/27.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *