
Liverpool imefikia makubaliano ya awali na Meneja wa Bournemouth, Andoni Iraola, kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo baada ya kuachana na Arne Slot mwishoni mwa wiki iliyopita.
Taarifa zinaeleza kuwa Liverpool na Iraola wamekubaliana kocha huyo wa Hispania kuhamia Anfield, huku tangazo rasmi la uteuzi wake likitarajiwa kutolewa ndani ya siku chache zijazo.
Endapo uteuzi huo utakamilika rasmi, Iraola anatarajiwa kuwasili Liverpool akiwa na baadhi ya wasaidizi wake wa karibu akiwemo Pablo de la Torre, Tommy Elphick, Shaun Cooper na Tom Webber ambao anataka wawe sehemu ya benchi lake la ufundi.
Mchakato wa kumpata meneja huyo uliongozwa na Mkurugenzi wa Michezo wa Liverpool, Richard Hughes, ambaye ndiye aliyemshawishi Iraola kujiunga na Bournemouth mwaka 2023 kabla ya yeye kuhamia Liverpool mwaka uliofuata.
Baada ya Liverpool kumfuta kazi Slot Jumamosi iliyopita, Iraola alitajwa mara moja kuwa mgombea mkuu wa kurithi nafasi hiyo kutokana na mafanikio aliyoyapata akiwa Bournemouth pamoja na falsafa yake ya soka inayofanana na utambulisho wa Liverpool.
Inaelezwa kuwa lengo kuu la viongozi wa Liverpool katika mchakato huo lilikuwa kupata kocha mwenye uwezo wa kutekeleza mfumo wa mchezo unaoendana na historia na utamaduni wa klabu hiyo wa kucheza soka la kushambulia kwa kasi na presha kubwa uwanjani.
Hata hivyo, Liverpool bado haijafanya mawasiliano rasmi na makocha au wataalamu wengine kwa ajili ya kujiunga na benchi la ufundi. Uamuzi huo unatarajiwa kufanyika baada ya mazungumzo na Iraola kufikia hatua za mwisho.
Iraola (44) ameendelea kujijengea sifa kubwa katika Ligi Kuu England tangu alipochukua mikoba ya Bournemouth. Chini ya uongozi wake, timu hiyo ilifanya vizuri katika nusu ya pili ya msimu wa 2025/26 kwa kucheza mechi 18 mfululizo bila kupoteza.
Kocha huyo aliisaidia Bournemouth kumaliza nafasi ya sita kwenye msimamo wa EPL na kufuzu kushiriki michuano ya Europa msimu ujao.
Pia, Bournemouth ilimaliza msimu ikiwa nyuma ya Liverpool kwa tofauti ya pointi tatu pekee, jambo lililoonyesha kiwango kikubwa cha maendeleo ya timu hiyo chini ya kocha huyo.
Mafanikio hayo ndiyo yaliyozidi kuwashawishi viongozi wa Liverpool kuwa Iraola ndiye mtu sahihi wa kuiongoza timu hiyo katika kipindi kipya baada ya kuondoka kwa Slot, huku mashabiki wa klabu hiyo wakisubiri kwa hamu kuthibitishwa rasmi kwa uteuzi wake.