Dar es Salaam. Kuna pisi nyingi ndani ya ‘gemu’ la Bongo Fleva’. Naongelea zile manzi zilizoibuka baada ya Jide, Ray C, Stara Thomas, Enika na wengine. Achana na wachanaji Zay B, Rah P, Sister P, Witnes na Dataz. Nipo na waimbaji pekee.
Na waimbaji ni wengi. Mwasiti, Recho, Linnah, Nandy, Tammy, Sarah, Zuchu, Maua na wengine. Hawa ni rahisi kuwataja haraka hata kama umeamshwa katikati ya usingizi. Ingawa wapo wengi ambao sijawataja na walifanya vizuri kisanii.
Katika majina haya, asilimia 90 ni mkono wa Ruge. Aliwakuza ama kuwapa mazingira bora ya ukuaji kimuziki. Wapo kina Shishi, Lulu Diva lakini hao miye siwachukulii ‘siriazi’ na kisanaa. Kwa sababu kwao sanaa ni daraja la kwenda sehemu kimaisha.
Ukiwaacha kina Jide na ‘era’ yao, ongezea na marehemu Maunda. Kizazi cha pili yake kina majina matatu, ambayo hayajatendewa haki. Au hayajatutendea haki sisi mashabiki, kwa maana ya uwepo wao umekuwa na maluweluwe mengi.
Unamfahamu Grace Binti Matata? Dunia haina usawa kabisa kama utamfanya yeye kama mfano wa usawa. Umewahi kumsikia ama kumsikiliza Vumilia? Ni rahisi na kazi nyepesi kudondosha chozi ukitazama safari yake kimuziki. Ni balaa hawa viumbe jombaa.
Hawa ni ‘pyua talenti’. Vipaji na vipawa haswa vya muziki. Hawa ni alama sahihi ya wanamuziki wa kike. Ajabu njia zao zimekuwa na makandokando balaa. Ukiujua muziki na ukawasikiliza utaumia. Ni wao wanadaiwa au wanaudai muziki? Hapa nakosa jibu sahihi.
Sina uhakika kosa ni la nani kati yao na muziki wao. Wadau weka pembeni. Ajabu wakati mashavu yetu yakiwa bado yamelowana machozi. Namuona na Ruby naye akifuata njia za Grace Matata na Vumilia. Ruby anaudai muziki au muziki unamdai Ruby? Naye pia nakosa jibu.
Vipaji na maisha ya hovyo Bongo hii ni kulwa na doto. Haviachani.