
Dar es Salaam. Wanahisa wa kampuni ya Swissport Tanzania Plc wanatarajia kupanda thamani ya uwekezaji wao baada ya kampuni hiyo kutangaza ongezeko la faida na kupendekeza kuwalipa gawio kubwa kwa mwaka ulioishia 2025.
Kampuni hiyo imeripoti faida halisi ya Sh6.5 bilioni mwaka 2025, ikipanda kutoka Sh5.5 bilioni mwaka 2024, ikiwa ni matokeo ya ongezeko la mapato ya huduma za mizigo (cargo), huduma za abiria pamoja na kuimarika kwa mikataba na mashirika ya ndege.
Katika kuimarisha thamani kwa wanahisa, bodi ya wakurugenzi imependekeza gawio la Sh3.27 bilioni, sawa na Sh91 kwa kila hisa iliyotolewa na kulipwa kikamilifu. Hii ni ongezeko ikilinganishwa na mwaka 2024 ambapo kampuni ilipendekeza gawio la Sh2.54 bilioni, sawa na Sh70.72 kwa kila hisa.
Akilizungumzia hilo hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa muda wa Swissport Tanzania, Joshua Jonas amesema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano mzuri na mashirika ya ndege pamoja na kuimarika kwa shughuli za usafiri wa anga nchini.
“Utendaji mzuri wa kifedha uliendeshwa na uendelevu wa wateja, mapitio ya kimkakati ya bei, uthabiti wa kiutendaji miongoni mwa washirika wa mashirika ya ndege, upanuzi wa shughuli za Air Tanzania, ongezeko la idadi ya abiria, ukuaji wa uagizaji wa mizigo, pamoja na kuimarika kwa matumizi ya Twiga Lounge ya Aspire,” alisema.
Alisema mazingira mazuri ya biashara kwa ujumla, pamoja na ukuaji endelevu katika sekta za utalii na usafiri wa anga yalichangia kwa kiasi kikubwa katika utendaji chanya wa Kampuni.
Alifafanua huduma za mizigo zimeendelea kuwa nguzo kuu ya mapato ya Swissport, zikiongezeka kwa asilimia 15 kutoka Sh26.56 bilioni mwaka 2024 hadi Sh30.44 bilioni mwaka 2025. Hii ilitokea licha ya ongezeko dogo la kiasi cha mizigo kilichoshughulikiwa, ambacho kilipanda kwa asilimia 1 tu kutoka tani 34,280 hadi 34,537.
Hali hiyo inaonyesha kuwa ukuaji wa mapato umetokana zaidi na uboreshaji wa bei, ufanisi wa kiutendaji na ongezeko la mizigo ya kuagiza kutoka nje ya nchi.
Huduma za abiria pia zilichangia kuimarika kwa mapato, hususan kupitia Twiga Lounge by Aspire katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro.
Lounge hiyo ilihudumia abiria 42,285 mwaka 2025, ikiwa ni ongezeko la asilimia 14 kutoka 37,214 mwaka 2024. Mapato ya huduma hiyo yalipanda kwa asilimia 20 hadi kufikia Sh2.39 bilioni kutoka Sh1.99 bilioni mwaka uliotangulia.
Alieleza kuwa katika kipindi hicho, Swissport pia iliimarisha wigo wake wa biashara kupitia mikataba mipya na upyaishaji wa mikataba muhimu. Kampuni ilifanikiwa kurejesha huduma za Ethiopian Airlines za ground na cargo katika Uwanja wa Kilimanjaro, pamoja na kupata huduma za usalama wa anga za Air Tanzania katika viwanja vya Dar es Salaam na Kilimanjaro.
Aidha, ilipanua huduma zake kwa kupata huduma za mauzo ya tiketi za Kenya Airways, hatua inayoongeza uwezo wake katika huduma za msaada kwa mashirika ya ndege.
Mikataba mingine muhimu iliyofanywa upya ni pamoja na Emirates Airlines (Dar es Salaam), Edelweiss na Eurowings (Kilimanjaro), pamoja na Qatar Cargo katika JRO, hatua inayoimarisha uthabiti wa mapato na imani ya wateja wa kimataifa.
Mwenyekiti wa bodi ya kampuni hiyo, Dirk Goovaerts, alisema kampuni inaendelea kuwa na matumaini makubwa kuhusu mustakabali wa sekta ya anga na utendaji wake.
“Tutaendelea kuimarisha uthabiti wa kiutendaji, kuboresha huduma kwa wateja, kupanua uwezo wa huduma, kuwekeza katika vifaa vya kisasa na maendeleo ya rasilimali watu, pamoja na kudumisha viwango vya juu vya usalama na utendaji,” alisema.
Uongozi wa kampuni hiyo umesisitiza kuwa utaendelea kuzingatia udhibiti wa gharama, ufanisi wa kiutendaji na utekelezaji wa nidhamu ya biashara ili kuhakikisha faida endelevu na ongezeko la thamani kwa wanahisa.