Dar es Salaam. Ujio wa Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira mkoani Kilimanjaro utatatua mgogoro unaofukuta Moshi mjini? ndilo swali linalogonga vichwa vya viongozi na wanachama kwa sasa.

Hii ni baada ya vikao mbalimbali vya kamati ya siasa ya wilaya na mkoa Kilimanjaro kufanyika kwa nyakati tofauti vikihusisha kamati za usalama na maadili bila kupata mwafaka huku kada na viongozi wawili wa CCM wakitajwa kuwa kiini cha mgogoro.

Machi 1, 2026 kulifanyika kikao cha maridhiano chini ya mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Rabia Hamid, kilichokuwa faragha hadi usiku bila kupata ufumbuzi wa mgogoro huo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Shaaban Mlewa, Mkuu wa Mkoa Kilimanjaro, Nurdin Babu, Mkuu wa    Wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava, Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Zuberi Kidumo.

Wengine waliohudhuria kikao ni mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC), Seleman Mfinanga, Katibu mwenezi wa CCM Manispaa ya Moshi, Athman Ally na Diwani wa Kata ya Bomambuzi, Juma Raibu na mwenyekiti CCM Wilaya, Faraji Swai.

Kutokana na msuguano huo, kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM kilichoketi Machi 7, 2026 katika ukumbi wa CCM mkoa almanusura kisifanyike, kama sio busara za Mwenyekiti wa CCM Mkoa Kilimanjaro, Patrick Boisafi.

Kikao hicho kilichokuwa na ajenda ya kupokea taarifa ya utekelezaji ilani ya CCM, kilihudhuriwa pia na mkuu wa wilaya ya Moshi, Godfrey Mzava na Mbunge wa Moshi mjini, Ibrahim Shayo, ambaye hata hivyo aliondoka muda mfupi baadaye.

Lakini, katika mfululizo wa matukio ya msuguano huo, viongozi 70 waliandika na kusaini barua ya kutokuwa na imani na kigogo wa CCM ngazi ya wilaya wakimtuhumu kutengeneza majungu, hila na kufitinisha viongozi wenzake.

Ujumbe wa kiongozi huyo aliouweka kimakosa katika ukurasa wake (status) wa WhatsApp Jumapili ya Februari 22,2026 akitamba “kumshughulikia” Meya Zuberi Kidumo na Mkurugenzi wa Manispaa, Mwajuma Nasombe ulikoleza moto huo.

Kutokana na yale yanayoendelea, baadhi ya viongozi na wanachama wa CCM Manispaa ya Moshi na mkoa wanaona ujio wa Wasira mkoani Kilimanjaro unaweza kuwa usemi wa wahenga “mgeni njoo mwenyeji apone.”

Kiini cha mgogoro ni baadhi ya viongozi wa CCM Manispaa ya Moshi na kada mmoja, kushiriki kutengeneza makundi na kuwagawa viongozi na wanachama.

Mbali na tuhuma hizo, lakini kundi hilo la watu watatu linadaiwa kuanza kutengeneza safu ya viongozi kwa ajili ya uchaguzi wa ndani wa CCM 2027 na kuchonganisha baadhi ya viongozi wa CCM na wanachama wake.

Ukiacha hilo, mmoja wa makada hao anatajwa kutengeneza fitina na majungu dhidi ya baadhi ya viongozi wa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na kutaka wahamishwe kwa sababu tu wanamkwamisha katika kukiuka taratibu.

Ujio wa Wasira Kilimanjaro

Akizungumzia ujio wa Wasira, Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Abraham Urio amesema Wasira atawasili mkoani humo kesho  Juni 4,2026 ambapo ataanza ziara rasmi Juni 5, mwaka huu ikitawaliwa na vikao vya ndani vya chama hicho.

“Kutakuwa na ziara ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Steven Wasira aambapo atawasili Juni 4, mwaka huu. Itakuwa ni ziara ya kawaida ya chama katika kukumbushana, kuambiana lakini kwa kuangalia uhai wa chama chetu,” amesema Urio

Aidha, amesema Juni 5, atakuwa CCM Mkoa ambapo atakutana na kamati ya siasa ya mkoa na kujadili masuala mbalimbali kuhusiana na chama na kupokea taarifa za chama za mkoa.

Amesema Juni 7, Wasira atakuwa Wilaya ya Rombo ambapo atakutana na mabalozi pamoja na mabaraza ya jumuiya zote na wazee wa chama hicho ngazi ya Wilaya.

Urio amesema Juni 8 atakuwa Wilaya ya Same na atafanya mkutano wa hadhara katika ofisi za CCM Same mjini.

“Nitoe rai kwa wanachama wote wa Same Magharibi na Mashariki waje wamsikilize kiongozi wetu akiwa anatufunza na kutuambia mengi na utekelezaji wa ilani ya chama mwaka 2025/2030,”amesema Urio.

Ingawa ratiba hiyo haifafanui kama moja ya majukumu yake atakapokuwa Kilimanjaro itakuwa ni kutatua mgogoro huo unaofukuta Moshi mjini na kukigawa chama hicho, lakini taarifa za ndani zinadai ni moja ya mambo yaliyomleta.

“Ni ziara ya kichama lakini kubwa lililomleta ni huu mgogoro kwa sababu kuna advance team (timu ya awali) kutoka kwake ipo hapa Moshi karibu wiki sasa na ile siku ya Eid al-Adha walifanya kikao cha faragha kizito sana,” amedai mmoja wa makada wa chama hicho ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.

Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa Kili Home Garden mjini Moshi, kilihusisha wajumbe wa Kamati ya Maadili na Usalama na wakaguzi wa miradi kutoka makao makuu ya CCM na wajumbe wa kamati ya siasa wilaya na mkoa.

“Ulihusisha pia wajumbe wa sekretarieti za chama mkoa na wilaya na kilikuwa na kurushiana sana maneno humo ndani. Sisi tunaamini hao waliotoka makao makuu wameshajua mzizi wa tatizo ni nani hivyo Wasira atakuja kumaliza mzizi wa fitina.”

Taarifa kutoka ndani ya CCM zikiwanukuu baadhi ya makada, zinadai timu hiyo ya wakaguzi kutoka makao makuu zimekagua baadhi ya miradi ya maendeleo katika kata na kubaini uombaji wa fedha na matumizi yake haukufuata taratibu za CCM.

Alipotafutwa kuzungumzia ujio wa kiongozi huyo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Patrick Boisafi, amesema ni vigumu kujua iwapo Wasira ameletwa kwa ajili ya mgogoro huo au vinginevyo.

“Labda akishakuja ndio tutajua kuwa suala la mgogoro ni miongoni mwa mambo atakayoyashughulikia, kwa sasa hatufahamu na ni vigumu kufahamu,” amesema.

Boisafi, amesisitiza Wasira atafanya kikao katika mkoa huo keshokutwa Juni 5, 2026 lakini bado haijajulikana kama kitahusu masuala ya mgogoro au vinginevyo.

Alipoulizwa hatua ambazo mgogoro huo umefikia, amesema si mgogoro mkubwa ni mambo ya kawaida katika maisha na siasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *