
Harakati ya mapambano ya Ansarullah nchini Yemen imetangaza kuwa vikosi vya jeshi la Israel vilivyotumwa Lebanon vitaendelea kuwa katika hatari ya mashambulizi yatakayofanywa na harakati hiyo kuonyesha mshikamano na Lebanon na harakati yake ya mapambano ya Hizbullah hadi vitakapoondoka kabisa kwenye ardhi ya Lebanon.
Mohammed al-Farah, mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Ansarullah, ametoa ujumbe huo katika chapisho kwenye mtandao wa X.
“Adui Muisraeli anapaswa kutambua kwamba hujuma yoyote nchini Lebanon itakabiliwa na jibu, na kwamba wanajeshi wake kusini wa nchi hiyo wataendelea kuwa katika hatari ya mauaji ya kila siku hadi watakapoondoka kusini mwa Lebanon,” amesema al-Farah.
Mapema Jumatatu, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alitangaza kuwa utawala huo utafanya mashambulizi katika kitongoji cha Dahiyeh cha mji mkuu wa Lebanon, Beirut huku utawala huo ukiendelea kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.
Hata hivyo, baadaye, Rais wa Marekani, Donald Trump alisema utawala wa Israel umeghairi kufanya shambulio la kijeshi lililopangwa.
Tangazo la Trump lilitolewa baada ya Iran kuonya kuwa haitavumilia wimbi jipya la uchokozi wa Israel dhidi ya mji mkuu wa Lebanon.
Jamhuri ya Kiislamu imetaka kukomeshwa uchokozi katika nyanja zote katika eneo la Magharibi mwa Asia, ikiwemo Lebanon.
Tehran inatambua kukomeshwa mashambulizi kuwa mojawapo ya masharti ya makubaliano tarajiwa na Marekani, yenye lengo la kukomesha vita vilivyosababishwa na mashambulizi ya Washington yasiyo na sababu dhidi ya Iran kati ya Februari 28 na Aprili 7.