Walinda amani wengine wawili pia walijeruhiwa katika tukio hilo na wanaendelea kupatiwa matibabu katika kituo cha afya cha UNIFIL.

Kikosi hicho kimesema uchunguzi umeanza “ili kubaini mazingira halisi yaliyosababisha tukio hili la kusikitisha. Ghasia lazima zikome.”

Bado haijafahamika makombora hayo yalitokea upande gani, lakini tukio hilo limejiri wakati mashambulizi ya kurushiana risasi kati ya jeshi la Israel kusini mwa Lebanon na wapiganaji wa Hezbollah, ambao si sehemu ya jeshi la Lebanon, yakiendelea kuongezeka.

“Mashambulizi ya makusudi dhidi ya walinda amani ni ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na Azimio namba 1701 la Baraza la Usalama, na yanaweza kuchukuliwa kuwa uhalifu wa kivita,” imesisitiza  UNIFIL.

Shambulio hilo limetokea saa chache kabla ya kutangazwa kwa makubaliano mapya ya kusitisha mapigano kati ya Lebanon na Israel yaliyotangazwa na Marekani jana Jumatano.

Serbia yathibitisha kifo cha raia wake

Mamlaka za Serbia zimethibitisha kuwa mlinzi huyo wa amani alikuwa raia wa Serbia ambaye alipatiwa huduma za dharura za matibabu baada ya kambi yake kushambuliwa.

Baadaye alisafirishwa kwa helikopta hadi hospitali mjini Beirut ambako alifariki dunia kutokana na majeraha yake.

“Tunatoa rambirambi zetu za dhati kwa familia, marafiki na wafanyakazi wenzake wa mlinzi wa amani aliyepoteza maisha akiwa katika huduma ya kuleta amani,” umesema mpango wa UNIFIL katika taarifa yake.

“Fikra zetu pia ziko pamoja na walinda amani waliojeruhiwa tunapowaombea wapone haraka na kikamilifu.”

© UNICEF Gari lililoharibiwa limepinduliwa kwenye barabara iliyoharibiwa vibaya na mapigano ya hivi karibuni karibu na Hospitali ya Serikali ya Tebnine huko Tebnine, Kusini mwa Lebanon.

Wasiwasi waongezeka kusini mwa Lebanon

Katika taarifa yake, UNIFIL imeeleza wasiwasi kuhusu “ongezeko kubwa la makombora yanayorushwa na milipuko” katika maeneo mbalimbali ya kusini mwa Lebanon.

Mapigano yalianza tarehe 2 Machi baada ya wapiganaji wa Hezbollah kurusha mashambulizi kuelekea kaskazini mwa Israel, muda mfupi baada ya kuanza kwa mashambulizi ya anga ya Israel na Marekani dhidi ya Iran mwishoni mwa Februari.

Makubaliano ya hivi karibuni ya usitishaji mapigano, ambayo hayajumuishi Hezbollah, yanaripotiwa kuhusisha kuanzishwa kwa “maeneo ya majaribio yatakayowekwa chini ya udhibiti wa jeshi la Lebanon”.

OCHA: Tangazo la usitishaji mapigano lafifishwa na mashambulizi

Mauaji ya mlinda amani huyo yametokea saa chache baada ya Lebanon na Israel kutangaza kuwa zimekubaliana kutekeleza usitishaji wa mapigano kufuatia mazungumzo yaliyofanyika mjini Washington, hatua iliyokuwa imeibua matumaini ya kupungua kwa mapigano katika eneo la mpaka.

Hata hivyo, mashirika ya kibinadamu yameonya kuwa ghasia bado zinaendelea licha ya tangazo hilo.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu na masuala ya Dharura , OCHA, imesema watu wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa nchini Lebanon huku amri mpya za kuhama zikilazimisha familia nyingi kuondoka makwao.

“Watu wanaendelea kuuawa na kujeruhiwa nchini Lebanon licha ya tangazo la usitishaji mapigano,” imesema OCHA, ikiongeza kuwa wahudumu wa misaada wanaendelea kutoa msaada wa kuokoa maisha licha ya changamoto za usalama na vikwazo vya kufikia maeneo yaliyoathirika.

Madhara ya kibinadamu yaendelea kuongezeka

Hali ya kibinadamu nchini Lebanon inaendelea kuzorota huku zaidi ya watu 130,000 waliokimbia makazi yao wakihifadhiwa katika vituo vya muda, wakati maelfu wengine wakihifadhiwa na familia za wenyeji au katika makazi yasiyo rasmi.

OCHA pia imeripoti mashambulizi mapya matano dhidi ya huduma za afya yaliyosababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi wahudumu 19 wa afya.

Mashirika ya misaada yanatarajiwa kuzindua kesho Ijumaa ombi jipya la dharura la ufadhili ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka nchini humo.

Maafisa wa kibinadamu wameendelea kusisitiza kuwa raia, wahudumu wa afya na walinda amani wanapaswa kulindwa kwa mujibu wa sheria za kimataifa za kibinadamu.

© UNICEF/Fouad Choufany Watoto hucheza katika ua kati ya mahema katika makazi ya muda ya pamoja huko Beirut, Lebanoni.

Zaidi ya watu milioni moja wamekimbia makazi yao

Hadi sasa, ghasia hizo zimewalazimu zaidi ya watu milioni moja nchini Lebanon kuhama makazi yao huku jamii nyingi zikiendelea kuishi kwa hofu.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) limeeleza kuwa familia nyingi katika eneo la kusini mwa Beirut zimekuwa zikiogopa kubaki majumbani mwao kutokana na hofu ya kushambuliwa.

“Wengi wao wanakuja wakati wa mchana kukagua nyumba zao na kuondoka usiku,” amesema msemaji wa UNICEF, Christophe Boulierac, akizungumza na UN News.

Siku ya Jumatatu, video zilionesha maelfu ya magari yakipanga foleni kuondoka katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu Beirut baada ya kutolewa kwa onyo la mashambulizi yanayotarajiwa kufanywa na Israel dhidi ya maeneo yanayodhaniwa kuwa ngome za Hezbollah.

“Mjini Beirut pekee, inakadiriwa kuwa watu 200,000 wamekimbia vitongoji vya kusini kufuatia amri ya kuhama iliyotolewa na Jeshi la Ulinzi la Israel tarehe 1 Juni,” amesema Stéphane Dujarric, msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika taarifa yake ya Jumatano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *