Shirika kuu la haki za binadamu la Iran limelaani mwenendo wa jamii ya kiimataifa wa kutochukua hatua za kushughulikia uhalifu wa ukatili unaofanywa dhidi ya watoto, likitaka kutiliwa maanani kimataifa watoto wengi wasio na hatia waliouawa na Marekani na utawala wa Israel katika uchokozi wa karibuni dhidi ya Iran.

Taarifa iliyotolewa na Baraza la Haki za Binadamu la Iran imesema kwamba jamii ya kimataifa kwa kiasi kikubwa imekuwa kimya au imeshughulikia kwa ubaguzi na upendeleo uhalifu dhidi ya watoto katika migogoro mbalimbali kote duniani.

Taarifa hiyo imetolewa kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji (International Day of Innocent Children Victims of Aggression), ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 4 Juni.

“Kila mwaka, Juni 4 hutumika kama chombo cha kupima uaminifu wa taasisi za kimataifa za kutetea haki za binadamu. Ukweli ni kwamba ukimya mbele ya mauaji ya watoto si kutoegemea upande wowote, bali ni kushiriki katika uhalifu. Jamii ya kimataifa lazima sasa, kabla haijachelewa, ioanishe kauli zake za kisheria na mienendo wake ya kivitendo,” imesema taarifa hiyo.

Imesema kwamba watoto wa Iran wamekuwa waathiriwa wa vitendo vya kigaidi vya wakala au uchokozi wa moja kwa moja katika miongo mitano iliyopita, ikiongeza kuwa taasisi za haki za Umoja wa Mataifa kwa kiasi kikubwa zimenyamaza kimya au hazijali uhalifu huo.

Shirika la haki za binadamu la Iran limesema kwamba ukatili dhidi ya watoto wa Iran uliongezeka katika miaka miwili iliyopita, huku raundi mbili za uchokozi wa Marekani na Israel dhidi ya nchi hiyo zikiua au kujeruhi makumi ya watoto.

Taarifa hiyo imesema mashambulizi dhidi ya watoto wa Iran, ikiwa ni pamoja na shambulio la anga lililoua zaidi ya watoto na wafanyakazi 160 wa shule ya msingi kusini mwa Iran mnamo Februari 18, ni “uhalifu wa kivita ulio wazi chini ya Kifungu cha 8 cha Mkataba wa Roma wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai.”

Taarifa hiyo imesema kwamba utawala wa Israel na baadhi ya serikali za nchi za Magharibi pia zimefadhili na kusaidia mashambulizi ya kigaidi nchini Iran katika kipindi cha miaka 48 iliyopita ambayo yameua watoto wasio na hatia.

Pia imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuuwajibisha utawala wa Israel na makamanda wake wa kijeshi kwa uhalifu mwingi uliofanywa dhidi ya watoto huko Palestina na kwingineko.

Siku ya Kimataifa ya Watoto Wasio na Hatia Waathirika wa Unyanyasaji ilitangazwa na Umoja wa Mataifa mwaka 1982 kwa ajili ya kushughulikia mashaka ya watoto wanaosumbuliwa na unyanyasaji wa kimwili, kiakili na kiroho kufuatia hali mbaya ya watoto wa Palestina na Lebanon wanaosumbuliwa na ukatili wa utawala haramu wa Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *