Iran imepinga vikali tuhuma za Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani kwamba Tehran inataka kuwaua maafisa wa Marekani, ikiikosoa Washington kwa kujaribu kujionyesha kama mwathirika huku ikificha rekodi yake ya uhalifu wa kivita dhidi ya watu wa Iran.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baqaei, amekemea vikali madai ya Marco Rubio kwamba Iran inadaiwa kupanga njama ya kuwaua maafisa wa serikali ya Marekani, akiyataja madai hayo kama mfano mwingine wa juhudi za Washington za kupindua ukweli na kupotosha fikra za watu kuhusiana na uhalifu wake.

Afisa huyo wa Iran amesema madai hayo yasiyo na msingi yanaakisi mawazo ya mtu anayewatupia wengine matendo yake mwenyewe.

“Kila mtu anawafikiria watu wengine kwa mujibu wa imani yake,” Baqaei ameandika kwenye akaunti yake ya X jana Jumatano, akisisitiza kwamba, “Kujidhihirisha kama mwathiriwa hakuwezi kuficha uhalifu wa kivita, mauaji ya kimbari na uhalifu dhidi ya ubinadamu ambao mumeutenda dhidi ya taifa la Iran.”

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema hayo akijibu matamshi yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, katika kikao cha Bunge, ambapo mwanadiplomasia huyo mkuu wa serikali ya Washington alidai kwamba Iran inafanya mipango ya kuwalenga maafisa wa Marekani.

Haya yanakuja wakati ambapo katika vita vya uchokozi dhidi ya Iran vilivyoanza Februari 28, muungano wa kijeshi wa Marekani na Israel ulimuua shahidi Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na maafisa kadhaa wakuu na makamanda wa jeshi, na maelfu ya raia wasio na hatia kote nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *