Rais wa Marekani Donald Trump amesema angehisi “heshima” kukutana na Ayatullah Seyyed Mojtaba Khamenei, Kiongozi mpya aliyechaguliwa wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, iwapo makubaliano yatafikiwa ya kumaliza vita kati ya nchi hizo mbili.

“Nitahisi heshima kukutana naye,” aliwaambia waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval siku ya Alhamisi, na kuongeza kuwa, “Iwapo tutafikia makubaliano, inawezekana nikakutana naye… hilo litakuwa sawa.”

Kauli hiyo inakuja wiki chache baada ya Ayatullah Sayyid Mojtaba Khamenei kuchaguliwa kuwa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na Baraza la Wanazuoni Wataalamu la Iran, kufuatia kuuawa shahidi kwa baba yake, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika shambulio lililotekelezwa na Marekani na utawala wa Kizayuni lililolenga makazi yake mjini Tehran tarehe 28 Februari.

Utayari wa Trump kuonyesha nia ya kukutana na Kiongozi huyo mpya unaonekana kuwa mabadiliko ya mwelekeo, licha ya ukweli kwamba Washington inaendelea kuweka mzingiro wa baharini usio halali dhidi ya meli na bandari za Iran. Tehran imekuwa ikilaani hatua hiyo mara kwa mara, ikiitaja kuwa ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyoanza kutekelezwa tarehe 8 Aprili mjini Islamabad.

Kuepuka “yaliyomsibu Jimmy Carter”

Pia siku ya Alhamisi, Trump alidai kwamba awali alikuwa amefikiria lakini hatimaye akakataa operesheni ya siri ya vikosi maalumu iliyolenga kuteka akiba ya urani iliyorutubishwa ya Iran, akitaja hatari ya uwepo wa muda mrefu katika eneo la vita.

Trump alikumbusha pia operesheni ya kijeshi iliyoshindwa ya Marekani nchini Iran mwaka 1980, ambayo kwa kiasi kikubwa ilihusishwa na kuporomoka kwa kisiasa kwa Rais Jimmy Carter, kama sababu iliyomfanya ajiondoe kwenye mpango huo.

Aidha Trump amekiri kuwa: “Si kama Venezuela, unaingia, unakaa dakika chache na unatoka, na kila mtu anakupungia mkono wa kwaheri.” Ameongeza kuwa: “Unahitaji zana kubwa za kivita za kubebwa kwa ndege, na uko katika eneo la vita.”

Kauli zake zinakuja wakati Marekani ilikumbana na pigo la kimkakati mwezi Aprili kufuatia jaribio la kuwaingiza wanajeshi wake katika mji wa Isfahan mapema mwezi huo.

Kwa mujibu wa maelezo ya kipekee yaliyoripotiwa na Press TV, vikosi vya Marekani na huenda pia vya Israel vilifanya uchunguzi wa kina wa anga kabla ya uvamizi huo, ambapo vilipoteza ndege kadhaa za kijeshi. 

Kinyume na simulizi rasmi lililodai kuwa ilikuwa operesheni ya uokoaji wa rubani wa ndege ya F15 aliyedunguliwa, lengo halisi lilikuwa kupenya na kushambulia moja ya vituo vya nyuklia vya Iran katika mji wa Isfahan.

Makomandoo wa Marekani walinaswa, na operesheni hiyo ikageuka haraka kutoka jaribio la kupenya kituo cha nyuklia hadi juhudi za dharura za kuwaokoa wanajeshi waliokwama.

Askari wengi wa Marekani walikimbia huku wakiacha nyuma vifaa mbalimbali. Ndege za kivita za Marekani zilishambulia ndege zao wenyewe zilizokwama katika operesheni hiyo ili kuzuia zisiangukie mikononi mwa vikosi vya Iran.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *