Ikiwa ni katika kuendeleza siasa zake za kuwakandamiza viongozi mashuhuri wa kidini Utawala wa Al Khalifa nchini Bahrain umewatia nguvuni viongozi wengine kadhaa wa kidini.
Hatua ya utawala wa Al Khalifa ya kuwakandamiza viongozi wa kidini nchini si mbinu mpya, bali ina historia ya nusu karne, tangu kuanzishwa kwa utawala huo wa kibaraka, lakini pamoja na hayo kiwango hiki cha ukandamizaji, pamoja na idadi ya watu waliokamatwa, kilikuwa hakijawahi kushuhudiwa tena katika nchi hiyo ndogo ya kifalme.
Baqir Darwish, mkuu wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain, anasema: “Ukandamizaji huu dhidi ya Mashia haujawahi kushuhudiwa tena katika historia ya kisiasa ya Bahrain. Miongoni mwa waliokamatwa ni pamoja na wanazuoni mashuhuri, maimamu wa Swala za Ijumaa na za jamaa, wakuu wa vyuo vya kidini, wawakilishi wa maraaji wa kidini wa Najaf Ashraf na mji mtakatifu wa Qum, wahadhiri wa vyuo vya kidini, mahatibu na wahubiri wa dini ya Kiislamu na baadhi ya waanzilishi wa Baraza la Kiislamu la Wanazuoni” ambalo lilikuwa likifanya kazi chini ya uenyekiti wa Ayatullah Sheikh Isa Qassim.
Swali ni je, ni malengo gani yanafuatiliwa na utawala wa Al Khalifa katika kuwakandamiza viongozi wa kidini wa Bahrain kwa kiwango hiki?
Lengo kuu la Al Khalifa ni kuibua hofu na woga, na hivyo kuzuia kuendelea maandamano ya kupinga vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na vilevile uwepo wa wanajeshi wa Marekani nchini Bahrain. Kuenea kwa wimbi la kamatakamata ya kiholela ya utawala wa Al Khalifa dhidi ya wapinzani wake kunaonyesha kushadidi mbinu za kiusalama na kutekelezwa sera ya ukandamizaji wa kimfumo dhidi ya raia ambao wanatumia haki yao ya msingi kutoa maoni na kubainisha misimamo yao ya kisiasa kwa njia ya amani kuhusiana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran na matokeo yake ya moja kwa moja nchini Bahrain. Kwa hiyo, ukandamizaji huo mkubwa ni jaribio la kuzima malalamiko halali ya wananchi. Ili kufikia lengo hilo, kukandamizwa na kutiwa mbaroni wanazuoni mashuhuri wa kidini kumepewa kipaumbele katika ajenda ya utawala wa Al Khalifa.
Wasomi wa kidini wanaaminiwa sana na wana uungaji mkono mkubwa nchini Bahrain ambapo wana mtandao mpana wa mawasiliano nchini. Katika jamii nyingi za nchi hiyo, misikiti, Husseiniya na mimbar ni mahali ambapo maoni ya umma huundwa. Kukamatwa viongozi wa kidini kunafanywa kwa lengo la kuzuia ushawishi na upenyaji wa manazuoni katika jamii ya Bahrain.
Lengo jingine la Al Khalifa ni kufuta madhehebu ya Shia katika jamii ya nchi hiyo. Hiyo imekuwa stratijia ya muda mrefu ya utawala wa Bahrain. Kutokana na ukweli kwamba Waislamu wa madhehebu ya Shia ndio wanaunda idadi kubwa ya jamii ya watu wa Bahrain, utawala wa wa Al Khalifa katika muongo mmoja uliopita, umekuwa ukitekeleza kwa makusudi mipango ya kuvuruga muundo wa kijamii wa watu wa nchi hiyo ndogo. Ingawa unatumia vurugu za kidini dhidi ya wapinzani wake wote bila kujali Ushia wala Usuni wao, lakini viongozi wengi waliokamatwa kufikia sasa ni madhhebu ya Shia.

Baqir Darwish, Mkuu wa Jumuiya ya Haki za Binadamu ya Bahrain anasema: “Taarifa za Wizara ya Mambo ya Ndani zinazungumzia nafasi ya vyuo vya kidini, misikiti, Husseiniya, shule za kidini, taasisi za Kiislamu na hata sheria za kidini, jambo linaloonyesha wazi kuwa serikali inajiandaa kutekeleza kampeni kubwa ya kuweka vizuizi dhidi ya vituo hivyo vyote vilivyo na uhusiano na Mashia.”
Jambo la mwisho ni kwamba utawala wa Al Khalifa anaweza kuibua hali ya hofu na woga nchini humo dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia kwa kuzidisha ukandamizaji na kudhibiti kwa muda malalamiko yao, lakini bila shaka hatua hizo zitakuwa na taathira kinyume katika muda mrefu na hivyo kuzidisha mgogoro wa uhalali wa utawala huo nchini humo.